NENO LA MUNGU KWA LAODIKIA
Nalimwona mpenzi wangu, limbuko la ujana wangu. toka mbali nalimwita lakini asiitike, nikasema huenda amekuwa kiziwi nilipokuwa safari ya mbali. Nikampungia mkono apate kuniona, na kumbe ni kipofu! Nikajitia nguvu kumfuatia nipate kumrudisha, naam , nikamfikia. Na kumbe ni uchi, mavazi yake niliyompatia siku za uchumba alikuwa nayo yamechakaa, yasiweze kumsitiri uchi wake, naam ni kitanda cha buibui.
​
Nikamsemesha, mavazi na dawa ya kujipata macho yako upate kuona yapo mikononi mwangu. Naye akasema ni nani wewe? nikasema, mimi ndiye uliyeapa apa tangu ujana wako kuwa utanipenda daima, naam, nimekuja nikutwae hata nyumba ya Baba yangu. Mpenzi wangu akasema, tazama mimi sasa ni mtu mzima, nasema kama mtu mzima na wala si kijana tena, Nalikuwa masikini sasa ni tajiri, naam, ni kitu gani utanipa nisichokuwa nacho hata niambatane nawe?
​
Ijapokuwa mpenzi wangu alikuwa uchi alijiona kuwa tajiri, ijapokuwa alikuwa kipofu hakutwaa dawa ya macho mikononi mwangu. Mwenye masikio na asikie!

