KANISA LA MUNGU/KRISTO KATIKA NYAKATI SABA.
- mashibeelias2

- 7 days ago
- 4 min read
Updated: 2 days ago
Kama ambavyo nilitangulia kueleza katika somo lililotangulia, Kuwa kanisa la Mungu ni kama maji yatembeayo, na dhehebu ni kama maji yaliyotuama. Na tena, kanisa la Mungu ni kanisa linalokwenda kwa ufunuo wa Mungu ambao huja kulisafisha kanisa.
Kama Daudi alivyosema maneno ya safi ya Mungu ni fedha iliyojaribiwa mara saba kalibuni(tanuru la moto). Ili kuyapata maneno ya Mungu yaliyo safi, ni baada ya hatua ya saba yaani kanisa linalozaliwa kwa ufunuo wa saba ndio Kanisa litakalokuwa na maneno safi ya Mungu, nalo ndio takatifu. Yaliyobaki ni madhehebu yaani taka za fedha maana ni watu walikataa ufunuo wa Mungu, wakakataa kusafishwa.
Sasa twende tukaoitazame kanisa la Kristo katika hatua saba za utakaso na mahali lilipo leo, na madhehebu yaliyozaliwa kwa kukataa kutakaswa. Hatua saba za kanisa la Kristo zimeandikwa katika kitabu cha ufunuo, sura ya pili na ya tatu. Sura hizi mbili zinaelezea Makanisa saba, yaani Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia, na Laodikia.
Haya ni makanisa saba, ambayo yalikuwepo katika Asia ndogo katika taifa linalotambulikana kama uturuki leo. Makanisa haya yalikuwa na tabia tofauti tofauti, moja na lingine kama jinsi yalivyoandikwa. Wengi hujifunza makanisa haya kama historia, kwamba yalipita na hayapo leo. Lakini nataka nikuambie, yale makanisa saba yanabeba ufunuo wa Nyakati saba za kanisa la Kristo.
Makanisa yale ni kama jinsi Yezebeli anavyotumika katika Biblia, alitokea katika Israeli takribani miaka 900 kabla ya Kristo, lakini bado anatajwa katika kitabu cha ufunuo kana kwamba yupo. Tazama katika ufunuo;
Ufunuo wa Yohana 2:20
“Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu.”
Haya ni maneno aliyoandika mtume Yohana takribani miaka elfu baada ya Yezebeli mwenyewe. Lakini aliandika kwa kanisa la Thiatira kana kwamba Yezebeli alikuwa anaishi. Kimsingi Yezebeli aliyetajwa hapo si yeye ye yule, isipokuwa aina ya mafundisho yake ndio yale yale yaliyokuja tena katika kanisa la Thiatira. Na Yezebeli alifunua kanisa lililo na mafundisho hayo wala si Yezebeli ye yule.
Hivyo makanisa saba, katika ufunuo 2 na 3, yalikuwepo kweli kama makanisa na leo sehemu yalipokuwepo ni magofu tupu na taifa lenyewe limekwisha kutekwa na Ibilisi likamkana Kristo. Hivyo makanisa yale saba yanafunua kanisa moja la Kristo ambalo linapita katika nyakati saba katika kutakaswa kwake.
Nyakati saba hizi ndio majira ya mataifa(nje na Israel) hata mwisho, Ni nyakati saba za kumwandaa Bibi harusi wa Kristo ambaye atapatikana kwa kutakaswa mara saba. Yaani ufunuo wa Mungu utakuja mara saba kumtakasa, na baada ya mara ya saba ndipo Bibi harusi wa Kristo atakapokuwa tayari.
Hivyo makanisa saba ni nyakati saba za kanisa la Kristo, yaani kanisa moja linapita katika majira saba ya kutakaswa kwake. Kila wakati kanisa linapopokea ufunuo wa Mungu na kutoka hatua moja kwenda nyingine, linapotoka linaacha dhehebu ambalo halikuamini ufunuo wa Mungu uliokuja kuwatakasa ili kwenda hatua inayofuata.
Hivyo tunapokwenda kuangalia makanisa saba, ujue na kufahamu ya kwamba tunaenda kutazama Kanisa moja tu la Mungu/Kristo katika nyakati saba au katika hatua saba kufikilia utimilifu. Maana yake ni kama fedha iliyosafishwa mara saba, au kwa maneno mengine ni hatua saba za Mungu kulisafisha Neno lake. Kwa maneno mengine tunaenda kutazama ufunuo wa makanisa saba.
Na katika kuyatazama makanisa haya, lazima uwatambue pia malaika wa yale makanisa kama maandiko yasemavyo;
Ufunuo wa Yohana 1
¹² Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu;
¹³ na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini.
…
¹⁶ Naye alikuwa na nyota saba katika mkono wake wa kuume; na upanga mkali, wenye makali kuwili, ukitoka katika kinywa chake; na uso wake kama jua liking'aa kwa nguvu zake.
…
²⁰ Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile vinara saba ni makanisa saba.
Hapa Yohana aliona VINARA SABA ambavyo ni makanisa saba. Kimsingi ni kinara kimoja chenye matawi saba. Na pia aliona NYOTA SABA ambazo ni malaika saba.
Hivyo kila kanisa na malaika wake. Hawa sio malaika wa mbinguni, bali hapa malaika wanawakilisha wajumbe waliotumwa na Mungu yaani manabii. Lugha ya Biblia haifanani kila wakati hasa inapozungumzia jambo lile like kwa nyakati tofauti tofauti. Hawa malaika ni manabii walio na ufunuo wa Mungu kwa kanisa husika. Ufunuo ambao utawasafisha watu wale au kiazi kile.
Malaika au manabii hawa hawakutajwa majina, Inahitaji ufunuo wa Mungu kuwatambua. Na kwa wale walio na mafuta ya ziada katika taa zao leo wanawafahamu hao malaika ni akina nani mpaka sasa, lakini wanawali wapumbavu hawajui kitu. Hata hivyo nitawataja malaika hawa kulingana na kanisa husika tunapokuwa tunaliangalia baadae ili isiwepo udhuru kwa mtu awaye yote.
Makanisa haya saba ni ya mataifa, habari zote ambazo Yesu aliziandika ni kwenda kwa mataifa, Yesu Kristo hakusema neno kuhusu kanisa lilokuwa Israel, si kwamba walikuwa wakamilifu, bali ni habari ambazo ziliandikwa kama majira ya kanisa la mataifa hata mwisho. Makanisa haya saba ambayo ni nyakati saba za kanisa ni saa ya kanisa la mataifa, hata yatimie yote yaliyoandikwa.
Kanisa la Israel saa yake ilianza katika kitabu cha Danieli, saa hii ikazima baada ya kumkatilia mbali masihi. Naye Bwana akamwacha Israeli ajitaabishe kwa wingi wa uchuuzi wake. Ndipo Yesu Kristo akawageukia mataifa, naye akawatwaa badala ya Israeli kwa kuwa walimwamini.
Hivyo majira yamekwisha kuwekwa mbele juu ya kanisa hili jipya yaani wakristo. Na majira haya ni hizi nyakati saba za Kanisa kuanzia Efeso hadi Laodikia. Ndipo kwa sababu hii utaona habari za makanisa haya saba zimepangwa kutoka ya kwanza kwenda ya pili kama ambavyo tutaenda kuona.
Kisha baada ya kuja kwa Yesu Kristo mara ya pili ni hitimisho la kanisa la mataifa. Maana nao pia watapimwa kwa kipimo kile kile alichopimiwa Israeli, kwamba watamwamini au la. Lakini ikiwa hawaamini ndipo watakatiliwa mbali na kisha Yeye (Israeli) aliyeachwa ukiwa atarudiwa.
Kwa sababu hiyo twende katika hatua inayofuata kutazama hizi nyakati saba kanisa Kristo lilipopitia hadi zamani hizi tulizopo na kile akisemacho Kristo juu ya kizazi hiki.


Comments