UFUNUO NA INJILI YA NYOKA.
- mashibeelias2

- Aug 22
- 7 min read
Updated: Sep 15
Shalom, Karibu katika Neno la Mungu, Bwana na akujalie kula chakula kigumu, kwa kuwa nimeshuhudiwa hakika ya kuwa mngali watoto wadogo ijapokuwa ni mda mrefu umepita.
Tunatazama juu ya ufunuo au injili ya itokayo kwa nyoka, kwa kuanza, tusome katika maandiko
Mwanzo 2:16-17
16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,
17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.
Hii ni injili ya Bwana Mungu kwa Adamu na Hawa, aliwahubiri yaliyo kweli, yaletayo amani ya kweli na Uzima wa milele. Walikuwa na uzima wa milele, hakukuwa na kifo ikiwa tu wangeendelea kulitii Neno la Mungu. Neno hili lilikuwa limebeba upendo, kwamba msile msije mkafa! Bwana Mungu alitaka waishi milele.
Neno lililobeba njia mbili mbele ya mwanadamu, kwamba chagua uzima ama mauti. Adamu aliitii injili ya Bwana, vivyo hivyo na Hawa, wakachagua uzima kabla ya kuja injili nyingine iliyowaleta katika mauti.
INJILI YA NYOKA.
Mwanzo 3:1-7.
1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?
2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula;
3 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.
4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,
5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.
6 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.
7 Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.
Unaweza kujiuliza ni Nyoka yupi anazungumziwa katika hayo maandiko maana nyoka hasemi, aliwezaje kuongea na Hawa? Huyu nyoka tunayemjua leo ni baada ya kulaaniwa. Kabla ya kulaaniwa alikuwa tofauti na alivyo leo. Kabla ya kulaaniwa alikuwa mwerevu, alikuwa na miguu, alikuwa anaongea kama mwanadamu. Alikuwa msaidizi wa karibu wa Adamu na Hawa.
Hapa unaona jinsi ambavyo Hawa alipojaribiwa na yule nyoka, akasikia injili kutoka kwa nyoka ambayo ilihubiri maneno kinyume na maneno ya Mungu. Lakini kwa nje haikuonekana kuwa mbaya kwa sababu ilikuwa na tumaini zuri kwamba ukila yale matunda ambayo Mungu amekataa msile, unafanana na Mungu kwa kujua mema na mabaya.
Kwa hiyo Hawa alifikiri kuwa Bwana Mungu huenda aliwakataza wasile yale matunda kwa sababu hataki tufanane nae, ndipo akapendezwa na ufunuo wa yule nyoka. Pia nyoka aliwahakikishia kuwa hakuna kifo kwa kula hilo tunda (mstari 4).
Ufunuo wa nyoka ulionekana mzuri, ulikuwa kama chakula kwa mtu mwenye njaa. Ulileta majibu ya maswali waliyokuwa nayo, lakini ufunuo ule haukutoka kwa Mungu bali kwa ibilisi, na nyoka akawa mwinjisti na mwalimu na kuhani na nabii na padre na mtume na mchungaji wa ibilisi, hakutoka kwa Mungu. Na kwa sababu hiyo ufunuo wa nyoka ulikuja/unakuja ili kulitangua Neno la Mungu.
Tangu saa ile wote wawili wakazaliwa upya kwa yule nyoka. Wakawa wana wa yule nyoka, Neno la Mungu likafa ndani yao na la ibilisi likaishi. Wakaabudu sanamu na si Mungu, injili ya uongo!
Injili ya Nyoka huwarudisha watu kutenda yale yale waliyokatazwa na Mungu. Injili hii huja na sababu nzuri, kwanza, kukutoa hofu ya kuangamia kulingana na Neno la Mungu. Pili kukupa sababu nzuri zaidi kwa nini unapaswa kulifanya lile lile alilolikataa Bwana.
Bwana Mungu aliagiza msile matunda ya ujuzi wa mema na mabaya, mkila mtakufa hakika, ufunuo wa nyoka ukasema hamtakufa hakika bali mtafanana na Mungu kwa kujua mema na mabaya. Ni heshima kulinganishwa na Mungu sio? Ndivyo ilivyokuwa kwa Hawa, aliitwaa ile injili akamhubiria na Adamu, naye akakubaliana naye, yaani naye akala lile tunda (ufunuo wa nyoka).
Tunda la ujuzi wa mema na mabaya ni ule ufunuo usiotoka kwa Mungu, ufunuo wa ibilisi, kama utahitaji kwa undani kuhusu tunda walilokula Adamu na Hawa ni lipi, bonyeza hapa
Kila wakati Neno la Mungu linapokuja likaaminika, ndipo neno lingine huja ili kubatilisha lile la Mungu. Musa mtumishi wa Mungu alihubiri Neno la Mungu kwa Israeli wapate kuijua njia ya Bwana; kujua yapasayo na yasiyopasa. Lakini ufunuo wa nyoka, ufunuo wa damu na nyama ukaja kinyume cha lile Neno la Mungu. Neno la Mungu likafa ndani ya watu wale, nao wakaenenda kwa mafundisho yao, yale ya nyoka. Ndipo Bwana Mungu akatuma wajumbe yaani manabii ili kuwarudisha watu wale katika Neno la Mungu. Kama Yeremia nabii alivyonena kwao.
Yeremia 7.
23 lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa.
24 Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele.
Yeremia aliyekuwa na ufunuo wa Mungu alihubiri, kwamba mliyoamriwa tangu zamani ni neno moja; ISIKILIZENI SAUTI YANGU(BWANA), ili mpate kujua makosa yenu, mpate kurudi. Lakini watu wale waliwaamimi manabii wao, marabi wao, makuhani wao walio na hiyo injili ya nyoka ndipo kwa sababu hiyo ikawa vigumu kuacha mafundisho yao na kugeuka/kumwamini Yeremia na manabii. Na ufunuo wao wa damu na nyama walienda nyuma (mautini) wala si mbele (uzimani)
Yeremia akanena tena akisema;
Yeremia 8:8-9
8 Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.
9 Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la Bwana, wana akili gani ndani yao?
Torati ya Bwana walikuwa nayo kweli kama walivyodai, lakini kalamu ya uongo, tafsiri ya uongo ndio iliifanya ile torati iwe uongo. Yaani, injili ya nyoka ndio kalamu ya uongo ya waandishi, wachungaji, makuhani, manabii, marabi n.k. Kweli ikabaki kwenye torati na ndani ya mioyo ya watu ukaishi uongo.
Mstari wa 9 anasema wenye hekima wametahayari, wamefadhaika. Hawa wenye hekima ni marabi, makuhani, walimu, waandishi, ambao leo ni wachungaji, walimu, mitume, wainjilisti, maaskofu, papa, kadinali n.k. Hawa ndio hutahayari baada ya ufunuo kuja kufunua uongo wao wanaoufundisha. Hawa ndio manabii wa uongo kwa kuwa hufundisha kwa ufunuo wa wanadamu, injili ya nyoka, maagizo ya wanadamu, ufunuo upingao Neno la Mungu.
Baada ya Musa, Neno la Mungu lilikuja kwa njia ya Yesu Kristo, akahubiri ufunuo wa Mungu kisha akaondoka, Na baadae ufunuo wa nyoka umekuwepo kuwarudisha watu kutumikia hayo hayo aliyoyakataa Bwana Yesu, Na biblia imekuwa uongo kwa sababu ya kalamu za uongo za wachungaji, walimu, mitume, wainjilisti, maaskofu, papa, kadinali n.k zimechukua mahali pa Neno la Mungu. Na hofu/kicho cha watu kwa Mungu ni hayo mafundisho ya uongo, hekima ya mwanadamu.
Ufunuo huu wa nyoka tayari umekuwa kiongozi wa kanisa leo kuanzia na Katoliki aliye mama wa madhehebu, wa kwanza kupokea injili ya nyoka, na kuifanya kuwa injili ya Kristo kwake, hofu kwa Mungu aliyonayo ni hayo mafundisho ya uongo. Na madhehebu mengine kama mama yao alivyo ndivyo yanavyokwenda.
Na hata sasa neno la Mungu limefungiwa nje ya kanisa wala hakuna asikilizaye ufunuo wake kwa sababu masikio ya watu yamezoea kusikia na kuupenda uongo. HATA KWAMBA KWELI IMEKUWA ADUI YAO NAMBA MOJA.
Nitakuonesha mifano michache jinsi ambavyo Kristo alinena waziwazi lakini leo ni yale yale aliyoyakataa ndiyo yanatendeka.
1. Kristo alisema usimwite mtu Baba duniani
Mathayo 23
⁸ Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.
⁹ Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni.
¹⁰ Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.
Lakini pamoja na Kristo kukataa mtu asiitwe baba wala mwalimu, leo kila mchungaji anaitwa baba, na kila mwalimu anataka aitwe baba na zaidi ya baba, cheo hiki kilianza na dhehebu la kwanza kukengeuka yaani Katoliki, Kiongozi wa kanisa hili anaitwa papa, tafsiri yake baba. Naye katika ulimwengu huu amepewa heshima kuu na watu walio kinyume na Mungu, wafurahiao mafundisho ya uongo.
2 Mafundisho ya mali,
Mathayo 6:24 inasema hamwezi kumtumikia Mungu na mali, utamdharau huyu na kumweshimu huyu. Badala yake yake mfundishe mambo ya adili, rehema na imani (mathayo 23:23)
Lakini leo injili imekuwa ya kutafta mali, jinsi ya kufanikiwa, Sadaka ndio mafundisho yanapewa kipao mbele na mhubiri yeyote. Mara sadaka ya kupanda, kujimaliza, ukombozi n.k. Mambo ya adili na Rehema na imani yamedharauliwa. Lakini yote haya yamekuja baada ya kupokea injili ya nyoka, iliyogeuza watu wasemao ni wakristo nao sio kwa sababu wanaenda kinyume na Kristo.
3 Mwanamke kuchunga kanisa.
Simpi mwanamke ruhusa ya kufundisha, wala kumtawala mwanamume, bali awe katika utulivu.
1 Timotheo 2:12
Ni dhahiri leo utaona wachungaji wa kike kila mahali, na bado hawa wanajiita wakristo wanaomwamini Yesu na mitume wake. Ni kalamu ya uongo ya waandishi ndio imefanya biblia kuwa uongo, na uongo huo ndio wanaoutumia kuruhusu walitakalo. Maana mtu asomaye biblia leo nje na tafsiri hizi za uongo, atajawa na maswali, afuate kipi kati ya biblia na kanisa linachosema. Maana ni vitu viwili tofauti. Lakini ni kanisa ndio halipo sahihi kwa kuwa linaenda kwa ufunuo/injili ya nyoka.
4 Mtu akiipenda nafsi yake ataipoteza;
Maana ya kuipenda nafsi ni kutafta mapenzi yako, kile ambacho mwanadamu anakitamani ndicho anachokitumikia, kama ni utajiri, nguo nzuri, magari, nyumba nzuri. Kiufupi maisha mazuri. Na utumishi huo ndiko ambako mtu huipoteza nafsi yake.
Watumishi wanaofundisha haya ni watumishi waliotumwa kudanganya, kama wale manabii 400 dhidi ya mikaya (1wafalme 22). Wanafundisha watu wazipende nafsi zao kwa kutafta hayo wanayoyatamani. Maombi yao ni kulilia utajiri, ibada yao ni mali, utajiri. Masikio yao yanawasha yakitamani kusikia utajili. Naam, Bwana ameachilia maradufu ya walimu hao, si 400 tena bali maelfu ili mshibishwe uongo mnaoulilia.
Jambo la ajabu kwa walimu hawa, si tu kwamba ni waongo juu injili ya Bwana, bali pia ni waongo kwa injili zao wenyewe, kile wanachokuahidi hukipati, badala yake wao ndio wanakipata. Maneno yao ni hadaa, wao ndio wanaotaka uwape mali zako.
Kwa sababu ya nafasi na mda, hayo yanatosha kukupa kujua injili ya nyoka kanisani. Bwana akijalia huko mbeleni tutaendelea kuyasikia mengine mengi kama hayo.
Leo kila mahali na kila mchungaji, mwinjilisti, kuhani, nabii, askofu, padre, kardinali, mtume, papa n.k (kwa jina la ujumla wanaitwa walimu) anayekufundisha hatafti nafsi yako iende mbinguni, hatafti ufalme wa Mungu wala utukufu wa Mungu, bali anatafta mambo ya nafsi yake tu, ambayo ni mambo matatu; 1.Pesa, 2. Umaarufu, 3. Ngono.
Wako walimu wanasimama madhabahuni kwa ajili ya mshahara wa mwezi. Wako wanaoanzisha huduma binafsi (ministry), hawa kwa kuwaza pesa, umaarufu na ngono, huleta mafundisho yatakayo wafanya waumini walete pesa mifukoni mwao na umaarufu. Na matendo yao ya mwisho ni ngono.
Kama kila mtu anavyowafahamu wanasiasa kuwa ni wanafiki, ndivyo na walimu hawa. Yesu Kristo katika mathayo 23 aliwanena vivyo hivyo.
Bwana amewavumilia siku nyingi, akawaacha mfanye mlitakalo, kila mtu aonavyo nafsi mwake. Naam, laiti mngeliweza kuutambua wakati huu na majira haya, mngelishangilia, na kuiazimisha siku yake. Naam, Laodikia na aseme Amina.

Mawasiliano; +255 755 251 999

Comments