NYAKATI YA PILI YA KANISA, SIMIRNA.
- mashibeelias2

- Oct 17
- 3 min read
Leo tunatazama kanisa la pili baada ya Efeso, yaani nyakati ya pili ya kanisa. Au kutakaswa kwa kanisa la kwanza. Kumbuka kanisa la kwanza liliacha upendo wa kwanza, lakini pia watu wale mbali na malaika wa kanisa lile (Paulo), walikuwa wanataka maziwa yaani mafundisho ya awali ya Kristo wala si chakula kigumu kama Paulo alivyowanena katika waebrania 5:10-14.
Hivyo Bwana Yesu ili kuwatakasa kosa la kupungua kwa upendo aliwajaribu ikiwa bado wanampenda, akaruhusu mafundisho ya uongo zaidi ya yale ya wanikolai hata wakaja wengine waliojulikana kama Gnosticism kwa Kiswahili "Ugnostiki" au "Elimu ya Siri"
Sasa tutazame yale aliyoyasema Yesu Kristo kwa kanisa hili la Smirna, habari hii ni Ufunuo wa Yohana 2:8-11.
Ufunuo wa Yohana 2
⁸ Na kwa malaika wa kanisa lililoko Smirna andika; Haya ndiyo aneneyo yeye aliye wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa, kisha akawa hai.
Haya ni maneno ya Yesu Kristo kwa malaika/mjumbe wa kanisa la smirna. Malaika au Mjumbe wa kanisa hili aliitwa Ireneo (Irenaeus). Ni kanisa lile lile lililotoka kuonywa kwa habari ya kuacha upendo wa kwanza lakini hapa utendeji kazi wa Roho mtakatifu ulibadilika. Ufunuo ambao ulikuja kwa Irenaeus ni kuliweka tayari kanisa kwa mateso na dhiki. Hiki ni kipindi kutoka mwaka 170 AD hadi 312 AD.
Yesu anajitambulisha kwao kuwa wa kwanza na wa mwisho, aliyekuwa amekufa kisha akawa hai. Kufunua mateso watakayopitia hata kufa, lakini watakuwa hai kama Yeye alivyokuwa hai. Ndipo hapo maana ya jina Smirna ilipotokea, yaani harufu nzuri ya mateso.
Tafsiri ya neno smirna ni manemane, ambayo ni utomvu unaopatikana baada ya kuujeruhi mti wa manemane (myrrh tree). Utomvu hukusanywa na kusagwa kuwa katika uvumba, radha yake ni chungu lakini ina harufu nzuri. Hivyo ndio maana nikasema Smirna ni harufu nzuri ya mateso! Bwana Yesu alinena kwa habari ya smirna kuwa;
⁹ Naijua dhiki yako na umaskini wako, (lakini u tajiri) najua na matukano ya hao wasemao ya kuwa ni Wayahudi, nao sio, bali ni sinagogi la Shetani.
Ni katika kipindi ambacho kanisa lililoacha upendo wa kwanza lilipitia mateso makubwa, dhiki na Kunyanyapaliwa katika kila mahali. Tena wayahudi yaani washikao torati waliendelea kuwafuatilia, ni watu wa madhehebu yaliyotoka kutapikwa kwa sababu ya mafundisho yao ya uongo. Badala ya kutubu waliwekeza nguvu zao katika kuhakikisha wanawamaliza nguvu watu wa Yesu Kristo ili wao wapate kuwa wana wa Mungu.
Ndipo Yesu Kristo anasema watu hao wanasema kuwa ni mayahudi wakati sio. Si kwamba kweli hawakuwa wayahudi, hapana, walikuwa wayahudi kabisa kwa kuzaliwa lakini ndio waliokula ufunuo wa nyoka, wakamwita Ibilisi mungu, wakajiita uzao wa Ibrahimu lakini hawakuwa kama Ibrahimu, hawakuitii sauti ya Bwana kama Ibrahimu.
Kwa sababu hiyo ni uzao wa uongo wa ibrahimu. Ni wana wa Ibrahimu lakini hawako kama Ibrahimu, hivyo hawafanani na ibrahimu ila ibilisi. Hivyo si wayahudi kwa Mungu bali wayahudi kwa ibilisi na sinagogi lao ni sinagogi la shetani.
¹⁰ Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.
Irenaeus pamoja na wahubiri wengine katika nyakati zile, walihubiri ujasiri kwa kila mkristo mbele ya watesao, wafurahi na kuwa tayari kuzichukua chapa za Kristo. Walipaswa kusimama imara hata kifo na ndipo watu/wakristo wengi katika kizazi hiki waliuawa.
Yupo mfalme mmoja wa kirumi Diocletian (maana Rumi ilitawala kote nyakati zile), ambaye aliwatesa wakristo, akatungia hata sheria za kuwanyanyasa kama hawaheshimu miungu mingine. Aliwatesa kwa kuwafunga na kuwaua katika utawala wake kwa siku kumi yaani miaka kumi (siku moja ni mwaka mmoja), kuanzia 303 AD hadi 313 AD.
Mateso na mauaji haya ndiyo yalikuwa mauaji makubwa ya mwisho kwa wakristo. Mwaka 312 AD mfalme mpya Costantine alimkiri Kristo na mwaka mmoja baadae yaani 313 AD aliitisha baraza ili kuwapa uhuru wakristo wa kuabudu kulingana na imani yao. Ndipo mateso ya wakristo yalipokoma.
Katika Yote hayo Yesu Kristo aliwasihi wawe waaminifu kwake, wakubali kumtii yaani Neno lake hata katika mauti, Maana yeye naye alikataa kumkana Mungu kwa ajili ya injili za uongo za wafarisayo, wasadukayo n.k. hata katika mauti, naye hata hivyo alifufuka akawa hai hata leo. Kwa namna hiyo hiyo pia alimwambia Ireneo na kanisa lote wawe kama Yeye.
Kanisa lilisimama na Yesu Kristo hata katika mauti, tena walijitoa kwa furaha kuwa wanaenda kuzichukua chapa zake Yesu Kristo, naam, hawakuogopa isipokuwa wachache.
¹¹ Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.
Ni wengi walioshinda yaani kuuawa kwa sababu ya Neno la Kristo, hawa mauti ya pili yaani ziwa la moto halina nguvu kwao kwa kuwa wameshinda. Kifo kilikuwa lazima kwa sababu jaribu lao kulishinda ni kukubali kufa. Hivyo kifo kilikuwa ushindi kwa wakristo wa kizazi kile.


Comments