NYAKATI YA TATU YA KANISA, PERGAMO.
- mashibeelias2

- Nov 6
- 6 min read
Tumetoka kuona nyakati ya pili ya kanisa la Kristo, kanisa katika mateso. Mateso ambayo yalikoma mwaka 313 baada ya mtawala Costantine kuwa mkristo na kuamua kuwapa wakristo uhuru wa kukusanyika na kuabudu. Lakini pia ilikuwa ni hatua ya kwanza ya utakaso wa kanisa ambapo Bwana aliujaribu upendo wao kwake.
Na hapa tunaangalia kanisa la tatu au nyakati ya tatu ya kanisa la Kristo, ufunuo wa tatu wa Kristo kwa kanisa ili kulitakasa. Ni utakaso wa pili wa kanisa na habari za kanisa hili la tatu yaani Pergamo tunaisoma katika kitabu cha ufunuo wa Yohana 2:12-17
¹² Na kwa malaika wa kanisa lililoko Pergamo andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye na huo upanga mkali, wenye makali kuwili.
Kanisa hili la Pergamo ni nyakati kati ya mwaka 312 BK hadi mwaka 606 BK. Hapa, Yesu Kristo anajitambulisha tofauti na kanisa la Smirna na Efeso. Anaonekana kuwa ni mtu wa vita, anao upanga kwa ajili ya vita dhidi ya kanisa hili ‘Pergamo’ na upanga wake una makali kuwili yaani pande zote mbili kwa ajili ya kukata ndani ya kanisa na nje ya kanisa.
Habari hizi zinaandikwa mahususi kwenda kwa malaika wa kanisa hili yaani mjumbe wa Pergamo ambaye aliitwa Martin wa tours.
Alikuwa ni askari wa Kirumi katika ujana wake. Huyu ndiye alikata joho lake la kijeshi na kumpa nusu masikini aliyekuwa akitetemeka kwa baridi. Baadaye, Yesu alimtokea ndotoni akiwa amevaa sehemu ile ya joho, jambo lililomgusa sana Martin wa tours na kupelekea aache jeshi.
Alihubiri maisha matakatifu, yeye mwenyewe akiishi kwa mfano huo na si kuishia kusema na kufundisha. Alihubiri imani, rehema na adili kwa vitendo na kwa sehemu kubwa aliharibu miungu mingi ya wapagani katika kuhubiri kwake.
¹³ Napajua ukaapo, ndipo penye kiti cha enzi cha Shetani; nawe walishika sana jina langu, wala hukuikana imani yangu, hata katika siku za Antipa shahidi wangu, mwaminifu wangu, aliyeuawa kati yenu, hapo akaapo Shetani.
Kristo anasema napajua ukaapo, ndipo kilipo kiti cha enzi cha shetani; tafsiri yake Martin wa tours aliketi pamoja au karibu na shetani. Kumaanisha kuwa aliishi au kutumikia katika himaya ya shetani huku yeye mwenye akimheshimu Mungu wa mbinguni.
Martin alitumikia serikali ya warumi kama mwanajeshi, na serikali ilikuwa chini ya miungu ya kirumi. Kiti cha shetani ni katika miungu, na miungu tafsiri yake ni mungu wa uongo. Kiti cha shetani kilikuwa katika serikali ya kirumi, huku ndiko shetani alikuwa ameweka makao yake na mahali pake pa juu.
Antipa shahidi wa Kristo aliuawa kwa amri ya mtawala wa kirumi kwa sababu ya imani yake kwa Yesu Kristo, imani ambayo ilikuwa chukizo kwa miungu mingine maana ilikuwa kinyume na kila mungu. Martin kama askari wa kirumi alishuhudia kitendo kile cha kuuawa kwa Antipa shahidi wa Kristo.
¹⁴ Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini.
¹⁵ Vivyo hivyo wewe nawe unao watu wayashikao mafundisho ya Wanikolai vile vile.
Baadaye katika huduma yake, yaani katika kanisa lote kwa ujumla walimu wa uongo wakajitokeza wakifundisha mfano wa mafundisho ya Balaamu, yule ambaye habari zake zimeandikwa katika kitabu cha Hesabu 22,23 na 24. Balaamu alikusudia kuwalaani wana wa Israeli kwa ajili ya Balaki mfalme wa wamoabu lakini kila alipokwenda kuwalaani alipewa kuwabariki kwa amri ya Bwana. Na mara mwisho alimshauri Balaki mfalme kuwa anapaswa kuwashawishi wana wa Israeli kinyume na Mungu wao.
Kumbuka Balaamu alipokuja kuitwa na mfalme Balaki alisema hatanena neno isipokuwa alichokisema Bwana. Naye alifanya vyema kunena zile baraka alizokuwa anapewa na Bwana, lakini kwa kuwa alifikiri Mungu hutumikia wanadamu, kwamba alitaka laana iwapate Israeli sawasawa na neno la mfalme Balaki wala hakujali kuwa Mungu yu pamoja na Israeli na si Moabu.
Mwishoni akajifunza namna gani ya kuwafanya Israeli walaaniwe na Mungu, kwa maneno mengine kumfanya Mungu awalaani badala ya kuwabariki. Akajifunza sheria za wana wa Israeli na hiyo ikampa kujua namna pekee ya kuwalaani ni kuwafanya waende kinyume na sheria za Mungu.
Hivyo Balaamu mwana wa Peori alimshauri Balaki awashauri Israeli waje katika sherehe ambayo aliandaa vyakula vilivyotolewa katika sanamu, na kuwaandalia wanawake wa kimoabu wazini nao. Hapo ndipo laani ilipokuja kwa wana wa Israeli baada ya kukubali.
Sasa hapa napo wanatajwa watu walio na mafundisho kama hayo ya Balaamu, ambao wanafundisha na kuwageuza wakristo wazirudie dhambi ambazo katika kulisoma Neno la Yesu Kristo wamejifunza kuwa ni dhambi. Mafundisho ya wanikolai ambayo kanisa la kwanza la Yesu Kristo, Efeso, liliyachukia yalianza kupata nafasi.
Kumbuka namna ya kufanya mtu anayemwabudu Mungu amwabudu shetani ni kupitia neno lile lile la Mungu alilonalo, shetani haleti injili yake mwenyewe bali tafsiri au ufunuo wa uongo juu ya Neno la Mungu. Ndio lile tunda la ujuzi wa mema na mabaya, ambalo Adamu alilila kupitia mkewe, na Wana wa Israeli walilila kupitia walimu wao. Vivyo na wakristo wamelila kupitia walimu, wachungaji, maaskofu, wainjilisti, manabii na mitume wao.
Hivyo uongo huu yaani injili ya balaamu, injili ya wanikolai ilipata nafasi katika kanisa. Walimu, wachungaji, manabii n.k wa uongo waliweza kuvutia masiko ya watu. Jambo ambalo Martini anaambiwa anao watu hao tayari, si yeye bali wako katika kizazi chake ndani ya kanisa. Na Yeye mwenyewe alikuwa tayari amekubaliana na baadhi ya mafundisho ya wanikolai.
Mafundisho kama vile kuamini mkristo akifa akiwa na dhambi anaenda pagatori (Purgatory) kusubiri utakaso kupitia maombi na sadaka za walio hai. Uongo huu uliwarudisha watu kutumikia miungu. Maana kama mtu husamehewa dhambi zake baada ya kufa, basi Kristo alikosea kusema yule tajiri katika (Luka 16:19-31) ambaye alitaka mtu afufuke akawahubirie ndugu zake watubu wasije wakaenda huko aliko! badala yake alipaswa aombe mtu afufuke ili akawahimize ndugu zake wamwombee na kutoa sadaka na kufanya matendo mazuri kwa ajili yake ili asamehewe dhambi zake. Na kama huko alikokuwa huyu tajiri si pagatori basi ni sawa na kusema Yesu hakuujua ufalme wa Mungu.
Vile vile kuwaomba wafu waliokufa katika Kristo wawaombee walio hai kwa Mungu. Nayo ni ibada ya sanamu, kwa sababu Kristo alisema ombeni bila kukoma, hakusema na wafu bali walio hai. Na ikiwa wafu huomba kwa niaba ya walio hai, basi Mungu hatakiwi kuwalaumu walio hai kwa makosa yao badala yake awalaumu waliokufa kwa uzembe wao wa kuwaombea walio hai. Na ikiwa ni hivyo, injili ya Mungu yote itabatilika, haipaswi kuhubiriwa kwa walio hai bali waliokufa.
Fundisho lingine lilikuwa kumweshimu mwanadamu kana kwamba ndiye Mungu au kristo, mfano kumwita mtu baba (papa), hii ilipelekea Mungu/Kristo asiwe kiongozi wa watu bali yule mtu. Tena baada ya hapo mtu yule aliyepewa cheo hicho cha baba akapewa moja kwa moja (automatically) uweza kama wa Mungu kuwa hawezi kutenda kosa. Haya yote yanatendwa na watu wanaojua kabisa kuwa Yesu Kristo alikataa kumwita mtu baba wala kiongozi ( Mathayo 23:9). Pia ndio sababu ya kuziba masikio ya watu wasimsikilize Mungu zaidi ya yule mtu (papa) waliyemvika uungu.
Fundisho lingine lilikuwa kuheshimu wanadamu (watakatifu waliokufa) zaidi kuliko injili zao au matendo yao. Hii ilipelekea kuwatumikia wafu kwa kazi zao walipokuwa hai badala ya kumtumikia Mungu kama wao au kwa mfano wa matendo yao. Inaitwa kusujudia watakatifu waliokufa (Veneration). Maana ni sawa na mtu aliyeokota ganda la ndizi akalipanda katika nchi akitazamia litazaa ndizi. Kwa sababu yule mtakatifu aliyekufa hakupata kibali mbele za Mungu kwa kusujudia watakatifu waliokufa, na wewe humsujudii kwa sababu hiyo, imekuwaje kujiona na wewe ni mtumishi wa Mungu?
Hayo na mengine mengi ndipo Martin wa tours na kwa kanisa lote hili la Pergamo walijikwaa mbele za Mungu. Tafsiri ya Neno Pergamo ni ndoa, Ndoa hii ilikuwa kati ya mafundisho ya Balaamu, wanikolai na kanisa. Kanisa likaolewa na mungu mgeni. Yesu Kristo aliwasihi watubu.
¹⁶ Basi tubu; na usipotubu, naja kwako upesi, nami nitafanya vita juu yao kwa huo upanga wa kinywa changu.
Walipewa onyo watubu, na kama hawatatubu adhabu imekwisha kuwekwa, Yeye Mwenyewe Yesu Kristo atafanya vita na kanisa hilo. Ndio sababu alianza kujitambulisha anao upanga wenye makali kuwili. Na hapa anasema tena atafanya vita kwa huo huo upanga utokao katika kinywa chake.
Upanga utokao katika kinywa ni ufunuo wa Mungu kupinga mafundisho yao. Ufunuo huo utakuja kwa ajili ya kufanya vita, kama yeye mwenyewe alivyofanya vita na Israeli, watu ambao walikuwa na ahadi ya kuja kwa masihi lakini akaja kwa mfano wa kung’oa na kupanda. Lakini pamoja na onyo hili Kanisa halikutubu na adhabu yake tutaiona katika kizazi cha tano.
¹⁷ Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye nitampa baadhi ya ile mana iliyofichwa, nami nitampa jiwe jeupe, na juu ya jiwe hilo limeandikwa jina jipya asilolijua mtu ila yeye anayelipokea.
Yeye ashindaye ni yule atakayefaulu kuyajua mafundisho ya balaamu ni yapi na wanikolai kisha kuyashinda. Huyu atapewa kuzijua siri za ufalme wa mbingnuni zingine zilizofichwa,
Martin de tours hakufikilia baadhi ya ufunuo katika huduma yake, ndipo ikasalia mana ‘chakula cha mbinguni’ yaani Ufunuo wa Mungu katika kizazi chake. Huyo aliyeshinda ni Columban au Columbanus ambaye tutakuja kuziona habari zake katika kanisa la nne.
Mawasiliano
+255755 251 999



Comments