NYAKATI YA SITA YA KANISA, FILADELFIA
- mashibeelias2

- 2 days ago
- 5 min read
Tumetoka kuona jinsi kanisa la tano au nyakati ya tano ya kanisa ambapo Katoliki (roman catholic na orthodox catholic) waliitwa kutubu, lakini walikataa kutubu ili watakaswe kwa lile neno la Mungu. Ndipo likawa dhehebu la kwanza, watu waliomkataa Kristo na kushika kuenenda kwa jinsi ya mafundisho ya wanikolai na mafundisho ya balaamu, kinyume na Kristo.
Hapa tunatazama juu ya nyakati ya sita ya kanisa au kanisa la sita, ambalo ni kipindi kutoka mwaka 1750 BK hadi 1906 BK. Neno la Mungu lilikuja kutakasa watu wa uamsho wa Martin Luther yaani wapingaji wa katoliki (Protestants) au watu waliopingana na mafundisho ya wanikolai na mafundisho ya Balaamu. Lakini hawa wapingaji (waprotestant) walionywa ya kuwa wana jina la kuwa hai lakini wamekufa, hivyo injili ya mjumbe wa sita lazima ije ili kuwafanya wawe hai katika jina lililohai walilokuwa nalo ikiwa watakubali kutubu.
Sasa tuone kile alichokisema Kristo kwa kanisa la sita katika kitabu cha ufunuo 3:7-13
⁷ Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.
Kristo anajitambulisha kuwa mtakatifu, wa kweli na mwenye ufunguo wa Daudi, akifunga hapana afungaye, akifungua hapana awezaye kufunga. Maana alitaka utakatifu kwa malaika huyu, alimpa karama hiyo ili amletee utakatifu katika kanisa, vile vile ni mwenye ufunguo wa Daudi, ufunguo huu ni kitendo kile alichokifanya Daudi cha kutaka kumjengea Mungu nyumba, ndipo Bwana akampa ahadi kuwa ufalme hautaondoka katika uzao wake milele. Bwana akafungua mlango kwa Daudi kuanzia wanawe hata Kristo ambaye ni mfalme leo na hata milele.
Vivyo hivyo na malaika huyu shauku yake ya kumfanya kila mtu awe mtakatifu kweli kweli ilifungua mlango ambao yeye anayeingia hatatoka humo kamwe (Ufunuo 3:12). Ujue na kufahamu pia ya kuwa, wapo wanaoingia kwa Bwana na kutoka, kama wayahudi walivyoingia na kutoka, na kama wakatoliki walivyoingia na kutoka, na kila dhehebu ni watu walioingia wakatoka. Lakini yeye akaaye sharti awe amepitia njia ya utakatifu.
Haya yaliandikwa kwenda kwa malaika au mjumbe wa kizazi kile aliyeitwa John Wesley, huyu ndiye mjumbe wa kanisa hili. Ni mwingereza ambaye alitokea katika kanisa la kiprotestant la Anglican. Kanisa la Anglican liliundwa baada ya kanisa la katoliki lililokuwa uingereza kujiondoa ndani ya katoliki. Hatua hii ilichagizwa na mfalme Henry wa nane kutaka kuachana na mke wake Catherine wa Aragon kutokana na sababu za uzao ili amwoe Anne Boleyn ili ampatie mrithi katika ufalme. Ombi la Hery VIII lilikataliwa na papa, hii ikachagiza kujitenga kwa wakatoliki wote waliokuwa Uingereza.
Hivyo kanisa la katoliki la uingereza lilikataa kuwa chini ya papa, pia lilikataa si kweli kuwa mkate na divai vikiingia mwilini vinageuka kuwa mwili wa Kristo na damu ya Kristo kulingana na fundisho la katoliki. Lilikataa fundisho la pagatori, uuuzwaji wa vyeti vya msamaha wa dhambi, makasisi kutoa msamaha wa dhambi n.k.
John wesley alikuwa Kasisi katika kanisa hili la Anglican na aliendelea na ukasisi huo mda wote wa maisha yake, lakini kama ilivyokuwa kwa Martin wa tours na Columban kujitenga na kanisa wakakaa katika monasteri (nyumba za watawa), ndivyo na Wesley ambavyo hakukaa kanisani kuendesha misa, bali alisafiri kuhubiri na kadiri mda ulivyozidi kwenda utakatifu wake ukawa mbali kabisa na kanisa la Anglican.
Wesley aliweka mkazo utakatifu binafsi kuanzia muonekano wa nje yaani mavazi. Alisistiza maisha ya mtu yawe kulingana na neno la Kristo, kuishi kwa vitendo neni la Mungu. Aliweka utaratibu wa kusaidia kwa vitendo walio katika shida, wagonjwa, wafungwa, n.k. Na kila kitu kilichoandikwa kwa habari ya utakatifu kilipaswa kufuatwa vivyo hivyo. John Wesley alifundisha hatua mbili za injili ya Kristo ili kufikilia ukamilifu;
1.Neema ya kwanza (Kuzaliwa mara ya pili) na
2.neema ya pili (utakaso kamili).
John wesley hakuishia kugawa elimu kisha aende zake bali alisimamia utekelezaji wa kila neno la Kristo ndipo wakajulikana kama wananjia au methodists, walikuwa na nidhamu katika neno la Kristo katika kusoma, kuhubiri, kufunga, kuomba na namna ya kuishi. Wesley aligusa moyo wa Mungu maana jumla ya maneno ya Mungu ni kuwafanya wanadamu kuwa WATAKATIFU KAMA MUNGU ALIVYO MTAKATIFU. Ndipo kwa nini kanisa hili liliitwa Filadelfia, tafsiri yake Upendo wa ndugu. Mstari wa 8 anasema;
⁸ Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.
John wesley alikuwa mwinjilishaji na mfundishaji kama Paulo, naye alipewa mlango wa kuhubiri kama ule wa Paulo, injili yake ilikwenda mataifa mengi na sehemu zilizokuwa hatari kufikiwa ijapokuwa hawakuwa na nyenzo nzuri za kuwalinda. Alitumia pia makoloni ya uingereza kufikia mataifa hayo. Alikuwa na nguvu kidogo, yaani uwezo wa kifedha ulikuwa mdogo na pia ufunuo wa neno la Mungu.
Yako mambo mengi ambayo Wesley hakuyajua katika hekima ya mbinguni ndio maana unaweza kuona alirudia mafundisho yale yale ya Martin Luther, kubatiza wachanga, kubatiza kwa kunyunyiza n.k. Alichokifanya wesley ndicho ambacho Luther alitakiwa kufanya pia, si kuishia kupinga ukatoliki pekee, bali kuelekea hatua inayofuata yaani utakatifu, hatua ambayo ilikuwa imezuiliwa na mafundisho ya wanikolai na balaamu. Na kimsingi, Walutheri walipaswa kumsikiliza Wesley, lakini walikataa, walibaki kuwa na jina la Kristo huku wamekufa. Walikataa kutakaswa, nao wanafuata njia ya katoliki, hawapo kwa ajili ya Kristo bali wapo kwa ajili ya Martin Luther.
⁹ Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda.
Hao waliokuwa wa sinagogi la shetani ni kanisa la Katoliki. Kama nilivyotangulia kusema Anglican ni wakatoliki waliojitenga kwa sababu ya Mfalme Henry VIII mwaka 1534 BK. Na John wesley akaja kuwa kasisi mwaka 1728 BK. Na Anglican walikuwa na desturi nyingi za katoliki, ndio maana hawakuweza kuendana na mafundisho ya Wesley hata ikapelekea waumini wa John Wesley kuitwa wamethodist na si wa-anglican.
¹⁰ Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.
John Wesley na waamini (wamethodist), walisifiwa mbele za Mungu, walipendwa na Mungu. Lakini pia aliwaahidi kuwatoa katika saa/wakati wa kuharibiwa unaoujiria ulimwengu wote. Kumbuka kipindi hicho ilikuwa bado kanisa moja la saba kutimia wakati huo, na bado ikawako ahadi ya kuharibiwa kwa ulimwengu wote. Saa hii hata katika kanisa la saba (Laodikia) haijatajwa kumaanisha kanisa la saba ndio saa yenyewe ya kuharibiwa.
Na kwa sababu Mungu ni Mungu wa haki, inapaswa kujua makosa yanayoleta kuharibiwa. Haya yote tutajifunza katika kanisa la saba.
¹¹ Naja upesi. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.
¹² Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, na jina la mji wa Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu, na jina langu mwenyewe, lile jipya.
Shika ulicho nacho yaani adili, imani na rehema ndicho walichokuwa nacho wakishike isije injili nyingine ikawatoa huko. Walipewa mamlaka ya kukaa nje ya ujumbe wa Malaika wa saba ambaye ni William Seymour Ijapokuwa tayari walishatoka tayari.
Maneno haya hayakuzungumzwa kwa malaika mwingine tofauti na malaika wa kanisa hili, kwa sababu huo ndio ufunguo wa uzima. Kanisa hili lilikuwa takatifu machoni pa Mungu, hawakuwa watakatifu machoni pao wenyewe kama Katoliki alivyokuwa na alivyo leo. Yesu aliwahidi ataandika jina la Mungu, na mji wa Mungu na jina lake jipya.
Swali ni kwamba hilo jina jipya unalijua? Najua halijafunuliwa kwako bado, lakini itakuwaje wakati wa kufunuliwa kwake? Maana halitakuwa lile lile la zamani, naye Bwana alikwisha kuwaahidi watu washikao njia ya utakatifu kuwa atawafunulia kiurahisi ili wasije wakalikataa.
¹³ Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.
Mawasiliano:
+255755 251 999
Comments