top of page

UFUNUO WA DAMU NA NYAMA NA UFUNUO WA MUNGU

  • Writer: mashibeelias2
    mashibeelias2
  • Aug 6
  • 4 min read

Updated: Aug 16

Shalom, Karibu katika Neno la Mungu, hekima ya Mungu ikupayo uzima.


Kanisa au dini yoyote na hata katika Elimu ya ulimwengu huu inafanyika kwa mfumo wa ufunuo. Ufunuo ni ufahamu mpya anaoupata mtu kuhusiana na jambo fulani.


Ufahamu huo unaweza kuwa wa kweli au wa uongo kuhusu hilo jambo. Katika kukua katika huu ulimwengu utakutana na vitu vingi vigeni, na maswali mengi yatakuwa, hiki ni nini, Kwa nini hiki, lini na wapi. Majibu ya maswali hayo yatakupa ufahamu au ufunuo juu ya mambo hayo.


Majibu hayo yanaweza kuwa ya kweli au ya uongo au sahihi kiasi fulani na uongo kiasi fulani kwa sababu yanatokana na wanadamu ambao si waumbaji wa hivyo vitu bali nao wanajifunza kama wewe uliyeuliza. Hivyo majibu yaliyo sahihi ni kutoka kwa yule aliye vifanya vyote ambaye ni Mungu. Sasa, ukweli wa kila jambo au kila mtu unatoka kwa Mungu; hivyo basi Yeye anazo siri zetu na siri za kila kitu kitu katika ulimwengu wote. Yeye akizifunua hizo siri ufunuo wake ni kweli na yakini.


Sasa, Mungu anajifunua zaidi kwetu kwa habari ya ukombozi wala si mambo ya uumbaji. Kuhusu ukombozi wa mwanadamu Yeye yu karibu kusikiliza na kujibu. Na majibu yake ndio UFUNUO halisi na wa kweli kwa hao walio wake. Na kwa habari ya Neno lake upo ufunuo wa aina mbili ndani ya kanisa.


Tusome katika Mathayo 16:13-18


13 Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?

14 Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.
15 Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?
16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.
17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.
18 Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.

Hapa nataka tutazame hasa mstari wa 17, Petro alijibu sahihi au kwa lugha nyingine ufunuo wa Petro juu ya Yesu Kristo ulikuwa sahihi kabisa. Lakini Yesu Kristo anamwambia kuwa ufunuo huo hukuupata kutoka katika damu na nyama bali kutoka kwa Mungu.


DAMU NA NYAMA NI NINI?

Ukichukulia damu na nyama kwa lugha ya moja kwa moja hutaelewa hayo maandiko. Lakini damu na nyama ni lugha ya picha, damu na nyama ni mwili wa mwanadamu. Hivyo Yesu Kristo alimaanisha ufunuo ule Petro hakuutoa kwa mwanadamu ambaye ndiye damu na nyama, hakuutoa kwa mafarisayo wala masadukayo wala marabi wala waandishi wala walimu wa torati.


Jambo la kufahamu ni kuwa hata katikati ya mitume wakati ule Yesu anawauliza hakukuwa na mtume anayemfahamu Yesu Kristo kuwa ni nani isipokuwa huyu Petro. Hivyo Petro alimnena Yesu kristo kwa ujasiri kuwa ni mwana wa Mungu aliye hai si kwa ufunuo wa wanadamu bali ufunuo utokao kwa Mungu.


JUU YA MWAMBA HUU NITALIJENGA KANISA LANGU.

Katika msitari wa 17, tunaona ufunuo wa Mungu, ambao katika mstari wa 18 ufunuo ule Kristo anauita MWAMBA na katika huo kanisa lake atalijenga.  Huu mwamba ni ufunuo utokao kwa Mungu, kwa maneno mengine angeweza kusema, 'juu ya ufunuo utokao kwa Baba yangu kanisa langu nitalijenga'  Si kwa ufunuo wa damu na nyama (theolojia).


Lakini upo ufunuo wa damu na nyama kusema ule mwamba ni Petro na kwa maana kanisa la Kristo litajengwa juu ya Petro, aina hii na nyingine za tafsiri hazitoki kwa Mungu bali kwa wanadamu na kila aendaye katika ufunuo huo, hamchi Mungu bali mwanadamu na kwa sababu hiyo hana kweli ndani yake.


Hivyo ufunuo wa damu na nyama ni mafundisho ya wanadamu na yana jina maarufu, theolojia. Haya ni mafundisho na maagizo ya wanadamu ambayo yamekwisha kuteka kanisa lote kama katika Israeli, hata nyakati za Kristo ambapo alinena wazi akisema;


Mathayo 15

8 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.
9 Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.

Mafundisho haya yanatokana na ufunuo wa damu na nyama, na mafundisho haya huwekwa  katika mfumo wa shule (vyuo vya theolojia) na kuwa ndio kiongozi na muongozo wa dhehebu husika.


Mafundisho haya yameketi katika kanisa na kuzuia ufunuo wa Mungu. Hivyo Neno la Mungu linakuwa halina nafasi kwa watu hawa, wametii kilicho adui wa Neno la Mungu. Ufunuo wa Mungu na ufunuo wa damu na Nyama ni nuru na giza.


Ndipo kwa nini katika Israeli Bwana Mungu alituma manabii kama Isaya, Yeremia, Hosea, n.k Kuwahubiri jamii nzima ya Isareli ambao walikuwa  na makuhani, walimu, waandishi, marabi na manabii ili wote wapate kutubu. Manabii walikuwa na ufunuo wa Mungu na  walimu, waandishi, marabi na manabii walikuwa na ufunuo wa damu na Nyama kama ilivyo kwa kizazi hiki.


Hivyo basi kila dhehebu unaloliona leo linaenda kwa ufunuo wa damu na nyama. Na ufunuo wa Mungu hauna nafasi katika kanisa na kwa maneno mengine Roho wa Mungu hana nafasi ndani ya kanisa leo. Naam, Iko njia ionekanayo sawa machoni pa mtu lakini mwisho wake ni njia za mauti.

ree

Basi sikiliza wewe uitwaye kwa jina la Bwana; umeshindana na mwamba wako, ukayapenda yaliyomchukiza, ukachukizwa na yale ayapendayo. Naam, ndio ibada ya sanamu.


Uyatafakari moyoni mwako maneno haya, kabla Bwana hajaigeuza nuru yako kuwa giza. Kwa kuwa unaishi katika kizazi kile kile alichokikuta Bwana Yesu ambaye wewe unamnena kuwa unamependa huku ukiwa unamchukiza. Naam, lisikie Neno la Bwana, ukatubu.


Tazama pia👇


Mawasiliano; +255 755 251 999.

 
 
 

Recent Posts

See All
NYAKATI YA PILI YA KANISA, SIMIRNA.

Leo tunatazama kanisa la pili baada ya Efeso, yaani nyakati ya pili ya kanisa. Au kutakaswa kwa kanisa la kwanza. Kumbuka kanisa la kwanza liliacha upendo wa kwanza, lakini pia watu wale mbali na mala

 
 
 
NYAKATI YA KWANZA YA KANISA, EFESO.

Ndipo kwa sababu hiyo aliuacha upendo wa kwanza, alikuwa sahihi kabisa kumkemea Petro, na kila alichokuwa anakifanya lakini naye akaanza kupoa mwishoni mwa huduma yake kama Petro. Akachukuliana na wab

 
 
 

Comments


bottom of page