NYAKATI YA KWANZA YA KANISA, EFESO.
- mashibeelias2

- Oct 17
- 5 min read
Updated: Nov 6
Kanisa la Efeso ni kanisa la kwanza la Kristo, au wakati wa kwanza wa kanisa la Kristo, Ni hatua ya kwanza ya kanisa katika hatua saba litakalopitia, lakini ni kanisa ambalo ni sawa na dongo la fedha (ore); fedha ambayo haijasafishwa, imetoka kuchimbuliwa kutoka katika udongo. Tusome habari zake katika Ufunuo wa Yohana 2:1-7
¹ Kwa malaika wa kanisa lililoko Efeso andika; Haya ndiyo anenayo yeye azishikaye hizo nyota saba katika mkono wake wa kuume, yeye aendaye katikati ya vile vinara saba vya dhahabu.
Ufunuo wa Yohana 2
Haya ni maneno ya Yesu Kristo, yeye ambaye anaenda katikati ya vinara saba yaani makanisa sana. Yesu ndiye aliye shika makanisa haya katika mkono wake wa kulia/kuume.
Maneno haya yaliandikwa kwenda kwa malaika wa kanisa la Efeso, hayakuandikwa kwenda kwa kanisa au malaika wengi au watu wengi bali mtu mmoja, malaika mmoja. Na malaika anayezungumziwa hapa ni yeye aliyepewa ufunuo wa Mungu kuhubiri katika kizazi kile, ni mjumbe wa Mungu. Wengi wanajua malaika ni viumbe vya mbinguni ambavyo havina mwili kama sisi bali roho peke yake.
Hiyo siyo tafsiri ya neno malaika, bali tafsiri sahihi ni mjumbe aliyetumwa na Mungu. Kwamba awe ametoka mbinguni kwa jinsi ya roho au ametoka duniani na mwili huu wa nyama yaani mwanadamu, ikiwa ametumwa na Mungu ni malaika. Jina lingine huitwa nabii.
Hivyo malaika au mjumbe wa kanisa hili la Efeso ni Paulo; ni Paulo ye yule unayesoma nyaraka zake katika Biblia. Huyu ndiye aliyewapa mataifa haki ya kurithi ufalme wa Mungu sawa na Israel kwa ufunuo aliopewa na Yesu Kristo. Na Yesu Kristo akiipima kazi ya Paulo katika kizazi kile na kutoa jumla ya mambo yote kama ifuatavyo;
1.PONGEZI
Ufunuo wa yohana 2
² Nayajua matendo yako, na taabu yako, na subira yako, na ya kuwa huwezi kuchukuliana na watu wabaya, tena umewajaribu wale wajiitao mitume, nao sio, ukawaona kuwa waongo;
³ tena ulikuwa na subira na kuvumilia kwa ajili ya jina langu, wala hukuchoka.
Kanisa hili la Efeso ni kipindi kuanzia mwaka 53 BK hadi 170 BK, ni kipindi hasa Paulo anaanza kuhubiri kwa mataifa ili kumtwalia Kristo bibi harusi. Aliifanya kazi kwa bidii sana kuliko mitume wengine wote wa Kristo ambao ufunuo wao uliegemea kuwafanya wana wa Israel waamini.
Kristo alimwadikia Paulo pamoja na kanisa walioamini kuwa anafahamu yote wanayopitia, taabu, subira lakini pia jinsi ambavyo hawakuchukuliana au kuwavumilia watu wabaya wafanye ubaya wao katika kanisa. Hawakuchukuliana na ufunuo wa nyoka au mafundisho ya uongo hata kidogo.
Pamoja na kuudhiwa na wayahudi kama akina Iskanda na Himenayo, kuumizwa na kupigwa (Matendo 21:27-36, 2 wakorintho 11:24-27), Paulo hakuchoka, alipiga mbio za hubiri akiwa hata gerezani, hakulilia mali wala umaarufu wala kuigeuza injili ya Kristo kuwa ubatili kwa ajili ya mali.
Ndio maana injili yake imebaki kuwa kielelezo na msingi hata leo kujenga kanisa. Lakini pamoja na hayo Bwana Yesu aliona madhaifu hasa mwishoni mwa huduma yake na kanisa kwa ujumla.
ONYO
⁴ Lakini nina neno juu yako, ya kwamba umeuacha upendo wako wa kwanza.
Onyo hili lilikwenda kwa Paulo, ijapokuwa ni kwa kanisa zima. Lakini kwa kuwa kanisa linatembea kwa ufunuo wa Paulo, kwamba wote walioamini kwa ujumbe wake ni wa Paulo, anapoonywa Paulo wanaonywa wote pia. Onyo lilikuwa kuacha upendo wa kwanza, hapa ndipo tunapata tafsiri hasa ya neno Efeso. Efeso maana yake ni kuacha mema yaondoke.
ALIACHA VIPI UPENDO WA KWANZA?
Upendo unaozungumziwa hapa sio upendo wa mtu na mtu au mtu na kanisa bali ni mtu/kanisa na Mungu. Paulo katika kuhubiri alianza vizuri, hakuchukuliana na wabaya, alishindana hata na Mtume Petro kwa unafiki wa kushirikiana na mataifa lakini wakija wayahudi anajitenga nao(wagalatia 2:11-14), huku akiwa na ufunuo tayari kuwa mataifa ni warithi kama wao Israeli.
Paulo hakumsitahi Petro kwa kuwa ni mtume, alikuwa tayari kufarakana na mtu awaye yote ikiwa anaenda kinyume na ufunuo wa Mungu. Lakini jambo la ajabu ni pale mwishoni Paulo aliporudi Yerusalemu na kukutana na ndugu katika Kristo katika nyumba ya Yakobo, wakampasha kuwa wayahudi wamesikia aliyoyafundisha kwa mataifa ambayo yanaenda kinyume na torati (mfano aliruhusu wasitahiri, kula vyakula vilivyokuwa najisi katika torati n.k).
Kiufupi wayahudi walikuwa wakimtuhumu kwa kufundisha watu kuiacha torati au Musa. Wale wakristo katika nyumba ya Yakobo wakamsihi aingie katika hekalu na kufanya desturi za kiyahudi ili kuonesha anashika torati ya Musa. Paulo alikubali, akafanya kama walivyomshauri ili wayahudi wasije wakamdhuru; jambo la ajabu ni kuwa, kitendo kile kile alichomkemea Petro, yeye naye anakifanya. Maana yake yeye pia akatenda unafiki.
Ndipo kwa sababu hiyo aliuacha upendo wa kwanza, alikuwa sahihi kabisa kumkemea Petro kwa kile alichokuwa anakifanya lakini naye akaanza kupoa mwishoni mwa huduma yake kama Petro. Akachukuliana na wabaya (wayahudi) hao hao aliwahukumu hawataingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya sheria.
Pia utaona mfano mwingine Paulo alipofundisha kwa usahihi kuwa mtu asiwahukumu kwa vyakula wala mwandamo wa mwezi wala sabato ( wakolosai 2:16), lakini ni yeye yule tena akaruhusu watu wenye kuendelea kushika desturi hizo wavumiliwe kanisani (1 wakorintho 8). Maana yake alianza kuridhia chachu ikae ndani ya kanisa.
Na kwa sababu hiyo Yesu Kristo hakufurahishwa na mwenendo wa mwisho wa Paulo na kanisa. Ndipo akawataka wakumbuke ni wapi walipoanguka, kisha waparekebishe yaani kutubu.
⁵ Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu.
Yesu Kristo alimwagiza Paulo na kanisa wakafanye kama walivyoanza, kumpenda Mungu yaani Neno lake. Lakini kama hafanyi hivyo, kinara chake kitaondolewa yaani nuru yake ataizima kabisa. Na hili lilitokea, kumaanisha hakutubu. Kutubu kunakuja baada ya kuelewa umekosea wapi, kwa sababu mtu hawezi kuomba radhi pasipo kujua kosa.
Pamoja na yote hayo bado Yesu Kristo aliwaona wangali bado wakichukia mafundisho ya uongo. Kama asemavyo mstari wa 6;
⁶ Lakini unalo neno hili, kwamba wayachukia matendo ya Wanikolai, ambayo na mimi nayachukia.
MAFUNDISHO YA WANIKOLAI NI YAPI?
Mafundisho ya wanikolai ni kama yale ya nyoka aliyemfundisha Hawa akale matunda ya ujuzi wa mema na mabaya ambayo yalikuwa ukiyala unakufa. Lakini nyoka akamhuniria Hawa injili nyingine kinyume na ile ya Mungu na kumpelekea kuyala yale matunda akitazamia kufanana na Mungu.
Wanikolai ndio watu wa kwanza kabisa kuanza kuleta ufunuo wa nyoka ndani ya kanisa la Kristo. Hawa, walifundisha wamekombolewa kwa neema, hivyo matendo ya mtu kujitahidi kuishi maisha yasiyo ya dhambi ni kuidharau neema, hivyo walifundishwa kuitegemea neema na sio matendo. Walifundisha utakatifu unakuja kwa kutimiza matendo ya neema au sacramenti kama ubatizo, ekaristi (divai na mkate), kitubio n.k. Pia walifundisha kula vyakula vilivyotolewa katika sanamu kwa sababu kimwingiacho mtu hakimutii unajisi.
Ufunuo huu wa wanikolai upo hata sasa katika nyakati hizi tulizopo, isipokuwa umechukua umbile jipya la UKIKOMBOLEWA UMEKOMBOLEWA MILELE (ONCE SAVED ALWAYS SAVE). Ni fundisho linalopingana na Yesu Kristo aliyesema katika shamba lake/ufalme wake kuna ngano na magugu.
Ni fundisho lile lile kumfanya mtu awe huru kufanya lolote analoona linafaa kwa sababu ameshakombolewa milele, haitabadilika! Hivyo, Pamoja na kuwa wanikolai walimnena Yesu Kristo katika mafundisho yao, Paulo na kanisa la kwanza waliwakataa, walichukizwa na mafundisho yao.
Kisha Yesu akasema na kila mmoja yaani kanisa hata baada ya kuondoka Paulo kwamba yeye ambae ana sikio yaani anayeweza kuelewa na aelewe akatubu (kurudia upendo wa kwanza).
⁷ Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye, nitampa kula matunda ya mti wa uzima, ulio katika bustani ya Mungu.
YEYE ASHINDAYE NI NANI?
Huyo ashindaye ni yeye ambaye atafanikiwa kuelewa makosa ambayo Mungu amekwisha kuyaona katika kizazi kile. Mtu ambaye atatambua utumishi wa kwanza umefifia na karibu kuondoka kisha ahubiri hivyo kwa watu jamii kuwaleta katika upendo wa kwanza.
Mawasiliano;
+255 755 251 999

Comments