top of page

KURUDI KWA YESU KRISTO MARA YA PILI NI PIGO LIFURIKALO

  • Writer: mashibeelias2
    mashibeelias2
  • Sep 12
  • 6 min read

Updated: Sep 15

Kurudi kwa Kristo ni kitendawili kigumu, hasa katika nyakati hizi. Kulingana na ufunuo wa damu na nyama unaoongoza kanisa la wakristo, zipo dhana za aina nyingi kuhusu kuja kwake. Lakini iliyo maarufu ni unyakuo.


Karibu tena tutazame kurudi kwake Kristo, jambo linalojulikana na watu wote kuwa atarudi.


Nasema kurudi kwa sababu alikuja mara ya kwanza katika taifa la Israeli na mambo hayakuwa kama walivyotazamia watu wale waliomngoja.


Je, leo itakuwa kama watu wanavyotazamia?


Tuone unabii wa kwanza ulivyokuwa na jinsi ulivyotimilika, kisha tuone ni kwa nini Israeli hakumtambua yeye aliyemtazamia kwa shauku kubwa. Maana Malaki alihubiri akiwataja kuwa walikuwa wakimngoja kwa hamu (malaki 3:1)


KURUDI MARA YA KWANZA


Isaya 28

¹⁴ Basi, lisikieni neno la Bwana, enyi watu wenye dharau, mnaowatawala watu hawa walio ndani ya Yerusalemu.
 ¹⁵ Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli;
 ¹⁶ kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.
 ¹⁷ Nami nitafanya hukumu kuwa ndiyo kanuni, na haki kuwa ndiyo timazi; na mvua ya mawe itachukulia mbali hilo kimbilio la maneno ya uongo, na maji yatapagharikisha mahali pa kujisitiri.
 ¹⁸ Na agano lenu mliloagana na mauti litabatilika, tena mapatano yenu mliyopatana na kuzimu hayatasimama; pigo lifurikalo litakapopita, ndipo ninyi mtakapokanyagwa nalo.
 ¹⁹ Kila wakati litakapopita litawachukueni. Maana litapita asubuhi baada ya asubuhi, wakati wa mchana na wakati wa usiku; na kuifahamu habari ile kutakuwa kitisho tu.

Sijui kama unayaelewa maandiko haya, ni mithali juu ya mithali. Ndio unabii hasa uliobeba kazi nzima ya Yesu Kristo wakati wa kuja kwake, Isaya alitabiri miaka 627 kabla ya kuja kwake. Na kama Israeli angekuwa anamsikiliza Mungu, asingejikwaa.


Isaya anasema na viongozi wa dini, makuhani, marabi, waandishi n.k ambao ndio wanaowatawala watu. Waliomfanya kila mtu awasikilize wao na si Mungu, alikuwa hasemi na wanasiasa bali viongozi wa dini, kwa kuwa walikwenda kwa ufunuo wa uongo na hawakukubali kutii Neno la Mungu ambalo Isaya na manabii wengine walikuwa wakiwahubiria ili kuwatoa katika uongo wao. Nao kwa kuupenda utukufu waliopewa na wanadamu walikaidi sauti ya Mungu.


Nao walifanikiwa kuifanya injili yao ya uongo kuaminika na watu kuwa inatoka kwa Mungu na ni kweli. Wakaendelea kutumaini wanao uzima wa milele sawa sawa na ahadi ya Mungu katika Neno lake. Ndipo kwa nini Isaya anawaambia mmefanya agano na mauti.


AGANO NA MAUTI NI NINI NA WALIINGIAJE AGANO HILO?


Siku zote agano ni makubaliano yanayopelekea kutendeka kwa jambo tarajiwa.


 Neno la Mungu ni agano kati ya Mungu na mwamini ili kwamba akiishi katika hilo atapata uzima wa milele. Ndivyo ilivyokuwa torati, agano la kwanza na ndivyo lilivyo na agano jipya. Hilo ni agano la uzima, kwamba kwa kwenda katika Neno hilo unao uzima wa milele. Lakini kwa maneno mengine umeagana na mauti kuwa hutaingia mautini.


Hivyo agano la mauti ni lile lile agano la uzima. Mtu anaesema anao uzima kupitia sheria ya torati au Yesu Kristo maana yake pia ni anasema kuwa hakuna mauti kwake kupitia torati au Yesu Kristo. Ameagana na mauti kwa lile agano kati ya Mungu na yeye.


Kwa maana Isaya anapowaambia kuwa mmefanya agano na mauti anamaanisha wanaamini wanao uzima wa milele kupitia theolojia yao (ufunuo wao wa damu na nyama).


Shida ilikuwa ni kutumainia kuwa wanao uzima wa milele kupitia ufunuo wao wa nyoka, ufunuo wa damu na nyama. Kwa ufunuo huo ni wazi kuwa agano lao lilikuwa kati ya shetani na wao, ijapokuwa wao waliendelea kutumaini kuwa bado ni agano kati ya Mungu na sisi yaani uzima, lakini kiuhalisia walimwacha Mungu wakamgeukia mwingine kama kanisa leo lilivyomwacha Mungu na kumgeukia mwingine. Wakalidharau neno la Mungu alilokuwa akihubiri Isaya na manabii wote.


Theolojia zao zikawa kitu cha kuwasitiri wakati wa dhoruba yaani Neno la Mungu lilipowaijilia. Hata wangelikemewa kiasi gani, wanatazama theolojia zao na kujiona wanao uzima. Lakini kwa kutii ile injili ya nyoka walitoka katika njia ya uzima na kuingia njia ya mauti bila kujijua, na huko wakaendelea kutumainia wanao uzima kama hapo mwanzo.


Na Mungu alipowaijiria hawakushituka kuwa wameiacha njia ya Bwana, bado wakalikaidi neno la Mungu, hawakutaka kutubu, wakachagua theolojia zao dhidi ya neno la Mungu.


Ndipo Isaya akatabiri wakati wa hukumu ya theolojia zao utakapowadia. Ufunuo wao wa uongo, ufunuo  wa damu na nyama utakapokanyagwa na kuondolewa kwa ufunuo wa Mungu. Ufunuo huo wa Mungu ulitimia, ndiko kuja kwa Yesu Kristo mara ya kwanza, akisema kila lisilopandwa na Baba yangu litang'olewa. Neno lake lilikuwa mfano wa mvua ya mawe.


Masihi waliyemngoja kwa hamu alikuja, wakamchukia kwa sababu hakuendana na sifa walizojitungia kuwa atakuwa namna hii na hii, atafanya hivi na hivi. Ufunuo wa Yesu Kristo uliharibu uongo wao ulioaminika kwa watu na kutukuka (theolojia).


Lakini yote haya yalinenwa miaka karibu 600 kabla ya kutimia wala hakufahamu mtu awaye yote, kama ilivyo katika kizazi hiki. Maana yaliyoandikwa kuhusu kizazi hiki si unyakuo bali Pigo lifurikalo.


AGANO LAO NA MAUTI LIKABATILIKA!


Yesu alipokuja aliwaambia aaminiye na kubatizwa ataokoka, asiyeamini atahukumiwa (Marko 16:16), hapa ikawa wazi kuwa hawana uzima wa milele isipokuwa wameamini na kubatizwa, Tangu wakati ule Agano lao na mauti kwamba hawataingia mautini likabatilika moja kwa moja, ikawa kwamba wao ni wa mautini isipokuwa wametubu. Mapatano yao na kuzimu yakafika mwisho, walijiona wenyeji wa mbinguni lakini sasa ikabadilika, wakawa wenyeji wa kuzimu.


Agano likabatilika, Unabii ukatimia, Ufunuo wa Mungu yaani Kristo, ukawafurikia, ukafunika theolojia zao, uongo wao. Walijitahidi kuuzuia kwa kumuua Yesu Kristo kama walivyofanya kwa manabii wote, lakini hapa ilikuwa kama kumpiga teke chura.


Kifo kile kile kikageuka kuwa ukombozi, kikawa ndio kiberiti katika msitu ulionyauka. Neno la Kristo likawa mafuriko makuu katika Israeli, naam, na katika ulimwengu wote. Habari zile zikageuka kuwa kitisho cha uhai wa waovu. Tena Isaya alimaliza kwa kusema,


¹⁹ Kila wakati litakapopita litawachukueni. Maana litapita asubuhi baada ya asubuhi, wakati wa mchana na wakati wa usiku; na kuifahamu habari ile kutakuwa kitisho tu.

Isaya anasema, pigo hilo lililowakuta wana wa Israeli halitaishia hapo tu, bali litaendelea kuja asubuhi, mchana, na usiku. Kumaanisha pigo lifurikalo ndio ambalo kanisa linapaswa kulitazamia, kwa sababu ya uovu, mafundisho ya uongo, sharti lisilo la Mungu ling'olewe. Na kila mti mbaya utoao matunda mabaya ung'olewe ndipo pigo limekwisha kuwadia, Naam, hata sasa lipo.


Madhehebu haya ambayo kila mmoja amefanya ngao yake kushindana na Mungu, Pango lake wakati wa dhoruba, kujificha ili asije akasikia na kutubu, yatayeyuka.


KURUDI MARA YA PILI


Kurudi kwa Yesu Kristo ni kuja kwa ufunuo wa Mungu ambao utang'oa kila pando asilolipanda, kila ufunuo wa damu na nyama, injili ya nyoka. Nao ni wakati wa huzuni kwa sababu kwa miaka mingi mmeufanya uongo kuwa mahali pa kujitiri, katoliki alipoijiriwa hakusikia, akajisitiri katika uongo wake, mlutheri alipoijiriwa hakujali akaendelea kujisitiri kwa vazi la buibui. Naam, na kila dhehebu limekataa kutubu kwa kutumainia gongo lao, injili yao iliyojaa ufunuo wa damu na nyama, maagizo ya wanadamu.


Basi mkitaka kumwabudu Mungu katika Roho na kweli lisilizeni Neno lake, naam, mwenye masikio na asikie neno ambalo Roho analisema. Kwa kuwa imekwisha kuandikwa kwa habari ya kizazi hiki kwamba;


Ufunuo wa Yohana 3


¹⁴ Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
¹⁵ Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
¹⁶ Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
¹⁷ Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
¹⁸ Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
¹⁹ Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
²⁰ Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

Laodikia ndio kanisa la saba, ambalo litaijiriwa, tena kwamba halitubu litatapikwa kama Israeli alivyotapikwa. Bwana ameliona kosa la kizazi lakini kwa sababu kizazi hiki ni kipofu katika roho hakioni haya.


Lakini Kondoo watafurahi na kuishangilia siku hii, naam,Huku ndiko kuja kwake Yesu mara ya pili, lakini madhehebu yanasema tunasubiri unyakuo, na yeye wanayesema atakuja na kuishia mawinguni anasema sikilizeni sauti yangu, mkafungue milango ya fahamu zenu mpate kusikia Neno la langu, nje na theolojia zenu, nje na madhehebu yenu.


Fungueni milango ya madhehebu yenu maana ndani mmemfungia shetani mkamwita Yesu, kwa jina la Mungu. Na kusema alisema tuliomwamini tuna uzima wa milele, naam mmeagana na mauti kwamba hamtaingia huko.


 Isikilizeni sauti yake, lakini kama hamtaki kuisikiliza kuingia kuzimu mtaingia. Wala siombi kwamba mpotee bali mkatubu na kupona. Wakati wa pigo lile umewadia. Na neno lake halitamrudia bure ikiwa hamtasikia leo na kutubu. Na ye atawapa dawa ya macho mpate kuyaona haya.

ree

Mawasiliano;+255755251999

 
 
 

Recent Posts

See All
NYAKATI YA PILI YA KANISA, SIMIRNA.

Leo tunatazama kanisa la pili baada ya Efeso, yaani nyakati ya pili ya kanisa. Au kutakaswa kwa kanisa la kwanza. Kumbuka kanisa la kwanza liliacha upendo wa kwanza, lakini pia watu wale mbali na mala

 
 
 
NYAKATI YA KWANZA YA KANISA, EFESO.

Ndipo kwa sababu hiyo aliuacha upendo wa kwanza, alikuwa sahihi kabisa kumkemea Petro, na kila alichokuwa anakifanya lakini naye akaanza kupoa mwishoni mwa huduma yake kama Petro. Akachukuliana na wab

 
 
 

Comments


bottom of page