HATA SASA MNGALI MKIHITAJI MAZIWA
- mashibeelias2

- Aug 1
- 4 min read
Updated: Sep 7
Shalom, Karibu tena ewe uingiaye katika milango ya nyumba iitwayo kwa jina la Bwana, Naam, Laodikia na aseme!

Kuna mambo mawili yaliyo nistaajabisha mimi, naam, matatu yaliyo ajabu kwangu.
Paulo mtume kwa jinsi ya Roho alinena;Waebrania 5:10-14
10 kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.
11 Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.
12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.
13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga.
14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.
Paulo alililaumu kanisa la waongofu wa kiyahudi yaani Waebrania, kusema ni mda mrefu umepita tangu walipolipokea Neno la awali la Kristo ambalo kwa maneno mengine amelitaja kuwa MAZIWA, kwamba kila aliye na Neno la awali la Kristo ni sawa na mtoto anyonyae maziwa, kwa kuwa ni mtoto. lakini kama ilivyo kwa maumbile ya mwanadamu kuwa hukua kutoka kuwa mtoto hata ujana na kuwa mtu mzima; haikuwa hivyo kwa kanisa hili, walidumu kutaka kuwa watoto siku zote. Walihitajia maziwa yaani mafundisho ya awali ya Kristo. Kwa mda huu Paulo anawakemea, ilipaswa wawe watu wazima yaani walimu wa kuwafundisha watoto wanaozaliwa mafundisho hayo kwa kuwa ni watoto.
Jambo la AJABU aliloliona ni watu wazima kutaka maziwa na si chakula kigumu ambacho ni kwa watu wazima. Na kwa sababu hiyo hawana budi kuanguka katika makosa wangali na hiyo Biblia mikononi mwao. Ndipo kwa nini Bwana alinena akisema watu wangu huangamia kwa kukosa maarifa!
Paulo aliwaambia, hamlijui NENO LA HAKI, kwa kuwa Neno la haki ni kwa watu wazima waliozoezwa kula chakula kigumu, lakini ninyi mmezoelea maziwa (Maneno ya awali ya Kristo), nanyi ni watoto na pia bado mnataka kuendelea kuwa katika hali ya kitoto (Mngali mnataka maziwa).
Ajabu ya pili ni kuwa WAMEKUWA WAVIVU WA KUSIKIA, yaani masikio yao ni mazito kuelewa Neno la haki mbali na maziwa. Paulo kwa jinsi ya roho anashauri, kwamba kuendelea kunywa maziwa hakukufanyi kulijua Neno la haki na zaidi kuyataka maziwa kunafanya masikio yenu yasitake kusikia kitu kingine chochote zaidi ya maziwa (Kama katika kizazi hiki Kristo alivyokinena katika Ufunuo 3:17a).Ndipo anasema tukiyaacha kuyanena mafundisho ya awali ya Kristo yaani maziwa, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu.
Waebrania 6:1-3
1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu,
2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele.
3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.
Sasa kwa kuwa Paulo alijua lengo la injili ya Mungu na Kristo wake ni UTIMILIFU! Basi atumiaye maziwa hawezi kufikia UTIMILIFU. Hivyo basi akawashauri wayaweke kando mafundisho ya awali ya Kristo ambayo ameyataja kama sita katika waebrania 6:1-3.
Sasa, hayo maziwa/mafundisho hayo ya maziwa waliyokuwa wanayataka ni haya;
Kutubia kazi zisizokuwa na uhai yaani mafundisho ya kuacha dhambi; mfano, kuacha uzinzi, ulevi, kutukana, kuseng'enya, kuiba, kusema uongo n.k.
Kuwa na imani kwa Mungu. Hili ni la pili katika mafundisho ya awali ya Kristo yaani maziwa. Kuwa na imani kwa Mungu ni mafundisho juu ya kumwamini Kristo, na Mungu aliyemtuma Kristo.
Mafundisho ya mabatizo; Haya ni mafundisho juu ya ubatizo sahihi ni upi? Kwa nini ubatizo, Kwa jina gani mtu anabidi abatizwe? Kipindi kile kulikuwa mkanganyiko kati ya ubatizo wa yohana na ule wa Yesu. wengine wakihoji aliyebatizwa na Yohana anapaswa tena kubatizwa akimwamini Yesu Kristo? Na majibu ya Paulo ni katika Matendo 19:1-6.
Kuwekea mikono (wagonjwa). Maana yake ni kuponya wagonjwa kwa kuwawekea mikono kwa jina la Yesu. Haya pia ni mafundisho ya mwanzo mwanzo kwa kila amwaminiye Kristo, ambayo ni maziwa.
Kufufuliwa wafu. Ni mafundisho juu ya ufufuo wa wafu waliokufa katika Kristo katika siku ya mwisho. Hayo pia ni mafundisho ya awali ya Kristo yaani maziwa.
Hukumu ya milele. Haya ni mafundisho juu ya hukumu ya wafu waliokufa katika dhambi yaani nje ya Kristo. Haya nayo ni mafundisho ya awali ya Kristo, maziwa!
Sasa, haya ni mafundisho sahihi kabisa, kwa kila mtu azaliwaye mara ya pili, ni maziwa kwa watoto kwa kuwa ni haki yao kunywa maziwa. Ndio maana anayaita mafundisho ya awali kwa kila aaminiye. Lakini anapaswa kukua na kubadilika kutoka kutumia maziwa na kuanza kula chakula kigumu.
Na katika Neno hili unalolisoma na utakalolisoma ama kulisikia siku zijazo usitazamie kusikia moja ya mafundisho hayo yakitiliwa mkazo. Kama Paulo alivyosema hayo tutayafanya Bwana akijalia.
Sasa, nataka niulize, mafundisho hayo sita yapo kando leo hii sawasawa na Neno la Paulo aliposema tukiyaweka kando?
Tazama ni JAMBO LA TATU LA AJABU kwamba ndio injili ya jamii nzima ya wakristo, tena ni afadhali ya waebrania, waliokuwa na mafundisho hayo 6 ya awali ya Kristo tu, leo yapo, na yasiyo mafundisho ya awali ya Kristo kama mafundisho ya mali, ulozi, namna ya kufanya ngono, kubarikiwa kwa sadaka za wanyama, kujazwa
roho mtakatifu, kujishikamanisha na madhabahu, mafundisho ya mpenyo, Kukanyaga mafuta, chumvi, Mafundisho ya kuibiwa nyota, mafundisho ya namna ya kuwa nabii, mafundisho ya kutambua miti, mijusi ya laana n.k. Nafasi haitoshi kuendelea kuyataja.
Hata sio maziwa tena wanyayo kizazi hiki, maana ni mfano wa maji machafu.
Swali ni kuwa ni nani aliyewaloga? Ikiwa Paulo aliwalaumu watu wale kwa yale mafundisho sita yaliyo mafundisho ya kweli ya awali ya Kristo. Itawapasaje kizazi hiki? Na ikiwa kizazi kile hakikulijua Neno la haki kwa ukamilifu kwa yale maziwa, Je, HAKI yaweza kuwepo katika kizazi hiki kilicho na mafundisho yale yale, tena kwamba yameongezewa chachu? Au ni nani aweza kusafika akijitupa katika matope mara saba?
Lakini kizazi hiki kimenena tunangoja UNYAKUO kwa kuwa sisi ni bibi harusi. Naam, ni bibi harusi aliye uchi! Hata amekuwa si bibi harusi tena bali achukizaye, kwa kuwa ni uchi na kahaba! Lakini itakuwaje, ikiwa mlishindwa kumeza maji na maziwa, mtawezaje kumeza mihogo iliyo mbele yenu sasa! Naam, chakula hiki si laini, wala kuwa na majimaji.
Sisemi hivi ili kuwachukiza bali wema wapate kutakaswa na wabaya wapate kujulikana. Basi lisikie Neno la Mungu, ukatubu.
Mawasiliano:
+255755 251 999



Comments