KANISA LA MUNGU/KRISTO NI LIPI?
- mashibeelias2

- Oct 16
- 6 min read
Updated: Oct 17
Uwepo wa madhehebu mengi leo ni swali linalofikirisha juu ya kanisa la kweli la Mungu au Yesu Kristo ni lipi kati ya makanisa/madhehebu yote yaliyopo. Wengine husema yote ni makanisa ya Mungu; Lakini hiyo si kweli, ukisema yote ni ya kweli, basi kweli zitakuwa nyingi na si moja. Na Mungu watakuwa wengi na si mmoja, vivyo hivyo na Yesu Kristo.
Kwa sababu kila dhehebu lina kweli yake tofauti na kweli ya dhehebu lingine. Ili kujua kanisa au dhehebu lipi ni kweli mbele za Mungu na kwamba hapo ndipo kila goti la mwanadamu linapopiga linapiga mbele za Mungu, inafaa kujua mambo mawili;
Kanisa ni nini? Na dhehebu ni nini?
Kanisa ni kusanyiko la watu wanaoutafta uso wa Mungu au kumwabudu Mungu, ambao wanakubaliana katika mafundisho ya aina moja. Ikitokea kanisa hilo likatofautiana katika fundisho mojawapo, mgawanyiko hutokea na makundi mawili huzaliwa na kupelekea kutengana kila kundi na fundisho lake.
Hayo makundi mawili kila moja huitwa dhehebu. Maana yake makundi yote mawili au zaidi wana kitu kimoja wanachofanana mmoja kwa mwingine walichoanza nacho kabla ya kugawanyika. Kisha nyongeza au pungufu fulani ilipokuja ndipo inatokea wale wanaokubaliana na ile nyongeza au pungufu na wale wasiokubaliana.
Hiyo inatokea kwa sababu kila wakati kanisa linapaswa kukua kimaarifa ya ufalme wa mbinguni, na ili likue linahitaji UFUNUO. Na ufunuo ni lazima utoke kwa Mungu ndipo kanisa hilo libaki kuwa kanisa la Mungu. Lakini pia upo ufunuo usiotoka kwa Mungu, ambao unatoka kwa wanadamu ambao husema yasiyo kweli mbele za Mungu na ndio hupelekea tofauti ndani ya kanisa. Tazama ufunuo huu wa Petro juu ya swali la Kristo kwa wanafunzi wake.
Mathayo 16
¹³ Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?
¹⁴ Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii.
¹⁵ Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?
¹⁶ Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.
¹⁷ Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.
¹⁸ Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.
Hapa unaona majibu mengi katika swali moja, majibu haya yanatokana na ufunuo uliokuwepo katika madhehebu, Ulikuwepo ufunuo wa wafarisayo, wengine wa wasadukayo n.k. Lakini ni Petro ndiye aliyejibu swali kwa usahihi, na jibu lake halikutoka kwa fundisho la dhehebu fulani, kwamba ni la wafarisayo au wasadukayo au wazelote n.k. Bali ufunuo ule ulitoka kwa Mungu.
Ndipo Kristo alimwambia Petro, damu na nyama yaani wanadamu havikukufunulia hili, bali Baba yangu wa mbinguni. Damu na nyama ni ufunuo unaotoka kwa wanadamu na ufunuo huo baba yake ni Ibilisi kwa sababu hupingana na nia ya Mungu na kugeuza injili ya Mungu kuwa uongo. Ufunuo huu ndio hasa unaotengeneza mkanganyiko na kuleta mgawanyiko. Pia ufunuo huu mtu akiula(kuupokea), ni vigumu kwake kupokea ufunuo wa Mungu kwa sababu ufunuo wa Mungu utakuwa kinyume na huo ufunuo wa dhehebu lake.
Lakini ufunuo ulio kweli ni kutoka kwa Mungu na huo ndio Yesu Kristo alisema kanisa lake atalijenga juu yake. Ufunuo wa Mungu ni mmoja na kanisa lake ni moja. Ufunuo utokao kwa Mungu ndio kanisa, na ufunuo wa Mungu ndio Neno la Mungu au maneno ya Mungu.
Sasa tukiweza kuujua ufunuo wa Mungu ni upi na mahali ulipo, ndipo tutalipata kanisa la Mungu na Kristo wake.
Lakini ufunuo wa damu na nyama upo aina nyingi, hesabu yake ni hayo madhehebu uyaonayo. Lakini nataka pia ujue namna ufunuo wa Mungu unavyosababisha kanisa liwe dhehebu, kwamba ufunuo wa Mungu ujapo unakuwa nyongeza ambayo kanisa hukataa kukubaliana nao kwa sababu hauendani na mawazo yao au ufunuo wao.
UFUNUO WA MUNGU UNAVYOTENDA KAZI.
Zaburi 12
⁶ Maneno ya Bwana ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.
Daudi mtumishi wa Mungu alinena kuelezea maneno ya Mungu ni maneno safi yaani yaliyosafishwa mara saba. Ni mfano wa fedha, yaani madini ya fedha (silver) yanavyosafishwa kutoka hatua ya kwanza hadi ya saba kupata fedha iliyo safi.
Kawaida si madini ya fedha tu bali kila madini yanayochimbwa kutoka katika ardhi huwa katika dongo (mchanganyiko wa madini na udongo) yaani (ores).
Hivyo ili kupata madini safi bila udongo inapaswa lile dongo (ore) ijaribiwe kalibuni. Kalibu ni tunuru la moto, hivyo kujaribiwa katika tanuru la moto ni kuyeyusha lile dongo katika tanuru la moto (furnace) mpaka iwe uji uji. Ndipo hapo udongo hutwama chini na uji wa madini hubaki juu na kisha kumiminwa chombo kingine, ule udongo(uchafu) hutupwa, lakini yale madini yaliyosafishwa yanaenda hatua inayofuata, hatua ya pili.
Kila hatua unatoka uchafu na madini yaliyo safishwa yanaendelea hatua inayofuata, mpaka hatua ya saba, ndipo madini yaliyo safi bila udongo/uchafu wowote yanapatikana.
Katika kazi yote ya kusafisha, haya ni mambo ya kuzingatia.
Moto unaosafisha hatua ya pili ni mkali kuliko ule wa hatua ya kwanza, vivyo hivyo utakuwa mkali zaidi kadiri hatua zinavyodi kuendelea.
Kinachosafishwa hatua ya pili ni kile kilichopatikana hatua ya kwanza. Vivyo na hatua zinazofuta.
Uchafu unaopatikana hatua ya kwanza ni mwingi kuliko hatua ya pili, vivyo hivyo na hatua zinazofuta.
Ndivyo Neno la Mungu linavyosafishwa, hatua ya saba ndipo maneno safi ya Mungu hupatikana. Kila ufunuo wa Mungu huja ili kulisafisha Neno la Mungu lililotangulia. Ikiwa na maana kuwa Neno la Mungu mara ya kwanza linakuja likiwa pamoja na uchafu lakini pia katika mafumbo.
Torati ilikuja kwa mkono wa Musa, nalo lilikuwa Neno la Mungu pamoja na uchafu, akalisafisha kwa njia ya ufunuo wa manabii hata maneno ya Mungu yaliyo safi yakaja kwa nja ya Yesu Kristo.
Ufunuo wa Kristo ulikuwa ni hatua ya mwisho ya kusafishwa kwa torati, si tu kuondoa ufunuo wa damu na nyama walioupanda walimu katika kanisa, bali pia kuondoa baadhi ya mafundisho ambayo yalikuwa halali kabisa katika torati na ilikuwa ni lazima kuyatii lakini yalikuwepo ili kumfunua Yesu Kristo, hivyo wakati wa kutimia kwake yalibaki kama uchafu ambao sharti yaondoke.
Lakini Israeli hakufuata utaratibu huu kama jinsi kanisa leo halifuati utaratibu wa Mungu. Na kwa sababu hiyo mwisho wao ndiyo mwisho wa kizazi hiki ikiwa mtakuwa na masikio mazito kusikia Neno la Mungu.
KUFANYIKA KWA MADHEHEBU
Ufunuo ule wa Mungu ndio uliunda madhehebu, yaani ufunuo unapokuja huhubiriwa, kisha wanaoupokea ndio Kanisa la Mungu, na wale wanaochukizwa nao hubakia katika mafundisho yao ya awali yaani Neno la Mungu pamoja na uchafu ndani yake. Yeremia alinena kwa mfano huu akisema;
Yeremia 6
²⁹ Mifuo inafukuta kwa nguvu; risasi tu inatoka katika moto huo; mfua fedha ameyeyusha bure tu; maana wabaya hawaondolewi mbali.
³⁰ Watu watawaita taka za fedha, kwa sababu Bwana amewakataa.
Hapa anazungumzia tanuru lile lile la kusafisha fedha, kwamba moto unawaka lakini fedha haiyeyuki ili udongo/uchafu uondolewe, bali ni lisasi tu ambayo ni kichocheo(catalyst) cha kuharakisha uyeyushaji inatoka katika moto ambao kimsingi ni hao manabii. Lakini watu jamii yaani kanisa hawasafishiki.
Moto ni Neno la Mungu, Fedha ni kanisa lililo na neno la awali la Mungu, Risasi ni manabii, na mfua fedha ni Mungu. Bwana aliwakataa watu wale (Israeli) kwa sababu walikataa kusafishwa. Walikuwa dongo la fedha (Silver ore) wala si fedha.
Hivi ndivyo kanisa linageuka kuwa dhehebu, likiisha kukataa kupokea ufunuo wa Mungu, linabaki kama dongo la fedha (fedha pamoja na udongo wake). Yeremia alihubiri kanisa lile wakubali kusafishwa, waondoe uchafu wao, nao wakakataa wakijiona wanalo neno la Mungu. Lakini walikuwa kama dongo la fedha wala si fedha yenyewe, naam hawakuwa katika matumizi yoyote maana fedha isiposafishwa haina matumizi.
Hivyo kanisa likikataa kutii ufunuo wa Mungu hatua ya kwanza, linabaki kuwa dhehebu la kwanza (fedha iliyo na uchafu), na kanisa la pili ndio wale waliolisikia Neno la Mungu hatua ya kwanza. Vivyo hivyo ufunuo unakuja tena mara pili, kama fedha inavyotoka hatua ya kwanza kwenda ya pili, haiendi na uchafu wa ule wa hatua ya kwanza bali yanaenda madini yaliyosafishwa kutoka hatua ya kwanza.
Ndivyo na ufunuo mara ya pili unapokuja hauji kama ule wa kwanza, pia hauji kwa minajiri ya kusafisha waliokataa ufunuo wa kwanza bali waliokubali ili wasafishwe mara ya pili na kuwa kanisa la tattu. Ni sawa na wanafunzi walio katika shule, ukija kwa wanafunzi wa darasa la kwanza ni kwa lengo la kuwapeleka darasa la pili, kisha mara pili utakuja kwa wale wa darasa la pili ili kuwapeleka darasa la tatu na kuendelea.
Sasa, shida kubwa inakuja katika ufunuo utakaokuja kusafisha mara ya saba utakuwa mgumu kueleweka na wote isipokuwa wale walitoka kusafishwa mara ya sita. Ufunuo huu huja kuhitimisha kazi yote, kuvuna mavuno.
Kwa madhehebu ambayo kimsingi tafsiri yake ni waliokataa kusafishwa yaani kukataa ufunuo wa Mungu, ni ngumu kuelewa ufunuo wa Mungu hatua ya mwisho, ufunuo ule unakuwa kama makelele masikioni mwao. Ndipo kwa sababu hiyo Yesu kristo alitabiri akisema mtasikia sauti ya makelele nyakati hizi. (Mathayo 25:6).
Kanisa la Mungu hutoka ufunuo wa kwanza, wa pili, wa tatu mpaka wa saba, kutoka utukufu hata utukufu, kama maji yaendayo lakini dhehebu ni kama maji yaliyotuama. Ufunuo wa Mungu ni miguu ya watakatifu kuufikia ufalme wa mbinguni.
Hivyo kanisa la Mungu/Kristo katika kizazi hiki ni wale waiskiao(kuitii) SAUTI YA BWANA katika nyakati hizi. Na ufunuo huu hautakuwa mwepesi kwa madhehebu, isipokuwa wale walio na mafuta katika taa zao, ambao wamezoezwa chakula kigumu. OLE KWA WANAWALI WAPUMBAVU!
Hatua inayofuata nataka tulitazame kanisa la Kristo lilivyoanza kutakaswa hatua ya kwanza mpaka hatua ya saba, yaani leo. Hatua ambayo ndipo maneno ya Mungu yaliyo safi yatapatikana, nao walio wake watamwijia.


Comments