top of page

TUNDA GANI ADAMU NA HAWA WALIKULA?

  • Writer: mashibeelias2
    mashibeelias2
  • Aug 18
  • 4 min read

Updated: Sep 8

Tunda hili lilikuwa chanzo cha mauti kwa mwanadamu, Baba yetu Adamu na mama yetu Hawa walikula tunda hili wakaleta mauti duniani. Lakini tunda hili lipo hata sasa na kanisa na watu wote jamii wangali wakilila.


Shalom, Karibu tena katika Neno la Mungu. Na moja kwa moja tutazame habari hii katika kitabu cha Mwanzo 2:16-17


16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,
17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.

Hapa Bwana aliwaagiza kuwa matunda ya miti yote (maembe, mapera, matofaa, maparachichi n.k) wanaweza kula lakini tunda moja tu ambalo bado hakulitaja jina lake, hawakupaswa kulila. Na ikiwa watalila watakufa hakika.


Tunda hili linatokana na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. Tunda hili linaonekana ni mbali kabisa na matunda yale mengine au matunda tuliyoyazoea, kwa sababu matunda mengine yote tunapokula tunapata virutubisho kama protini, vitamini na madini. Lakini tunda hili ukilila unapata ujuzi wa mema na mabaya yaani maarifa ya kujua mema na mabaya.


Kwa tafsiri ya haraka ni tunda linaloshibisha kiroho na si kimwili kwa sababu huwezi kula embe ukapata ujuzi wa mema na mabaya, au chungwa au tofaa likakupa ujuzi wa mema na mabaya.  Vile vile tunda hili haliwezi kuwa tendo la ndoa, kama wengi wanavyodhani. Au ni nani kwenu afanyaye usherati kwa kutamani maarifa? Maana imeandikwa mti ule unatamanika kwa maarifa (mwanzo 3:6), kwamba kila alaye matunda yake anakula ili apate maarifa, aondoe njaa na kiu ya maarifa.


MTI HUU NI MTI GANI HASA!

Ili tuujue mti huu wa maarifa ya ujuzi wa mema na mabaya ni upi, inapasa kujua huo ujuzi wenyewe wa mema na mabaya ni upi, na ujuzi huu tuusome katika mwanzo 3:1-7.


1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?
2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula;
3 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.
4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,
5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.
6 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.
7 Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.

Tazama, ni jambo gani nyoka alilitenda, Lile agizo (mwanzo 2:16-17) alilosema Bwana Mungu, injili aliyoihubiri kwa Adamu na Hawa, walioitii na kuicha, inabatilika baada ya kusikiliza injili ya nyoka. Nyoka hakuja isipokuwa kinyume na lile Neno la Mungu.


Neno la Mungu lilikuwa katika mafumbo kama lilivyo leo katika Biblia, Hawa na Adamu hawakujua ubaya wa kupata ujuzi wa mema na mabaya wakila lile tunda ni upi. Yaani kwa nini wafe kwa kupata ujuzi wa mema na mabaya. Ijapokuwa waliitii injili ya Bwana Mungu, lakini waliihitaji majibu yenye kutosheleza nafsi zao.


Ndipo nyoka akaja na hayo majibu; kwanza akakana kifo, kwamba Mungu alisema watakufa hakika, yeye akasema hawatakufa hakika (msitari 4), Pili wakila watafanana na Mungu kwa kujua mema na mabaya.


Alichokifanya nyoka, ni kubatilisha moja kwa moja injili ya Mungu, na kumfanya Mungu kuwa muongo. Na Hawa akakubali kuwa Mungu ni muongo na nyoka ni mkweli kwa kuwa aliitii injili ya nyoka, na hata Hawa akamfuata Adamu akamhubiria maneno yale na Adamu naye akamsikiliza na kukubali injili ya Hawa itokayo kwa Nyoka.


Hivyo, mti wa ujuzi wa mema na mabaya ni yule NYOKA. Na tunda ni ule UFUNUO WA NYOKA. Unaitwa ufunuo wa nyoka kwa sababu ulitoka kwa nyoka. Ndipo kwa nini nalikuambia tunda hili lingali lipo na watu wakiendelea kulila hata leo, na kila dhehebu leo hii limejengwa juu ya ufunuo huu wa nyoka. Ndipo kwa sababu hii Kristo aliyatapika madhehebu yale katika nchi ya Israeli, mafarisayo, masadukayo n.k. kwa sababu yalijengwa juu ya ufunuo huu, wakilitangua neno la Mungu kama ilivyokuwa kwa Adamu na Hawa. Kwa jinsi hiyo ndivyo ambavyo itakuwa katika kizazi hiki kwa habari ya madhehebu ikiwa hawatatubu.


Uovu walioutenda watu wale ndio uovu alioutenda Adamu na Hawa. Na kwa kuwa Bwana alimfukuza Adamu atoke katika bustani ya Eden, ndivyo alivyomfukuza Israeli atoke katika nchi ile, hata baada ya miaka mingi kwa lile neno la ahadi amewarudisha ili kutimiza yote yaliyoandikwa.


Vivyo hivyo atakavyokitendea kizazi cha Laodikia! Ambacho kinajiona kuwa ni tajiri, kwa kuwa wamejitajirisha kwa ufunuo wa NYOKA.


Kisha Yesu Kristo ambaye ninyi mnamnena kuwa Bwana na kwamba mwampenda (lakini najua hamumpendi) kama alimvyomtapika Adamu na Israeli, ndivyo alivyonena kwenu, eeh Kanisa!


14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

Hapo Bwana Yesu akasema wazi kuwa atalitapika kanisa la mwisho ambalo ndicho kizazi hiki. Basi ikiwa hakumwonea huruma Adamu, wala Israeli, ni nani wewe hata asikutapike? Naam Bwana atakitapika kizazi hiki nacho kitakuwa fungu moja na mafarisayo na masadukayo; watu wale mliowalaumu na kuwashangaa kwa nini walimkataa yeye waliyemngoja. Kama maandiko yasemavyo;


17 Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,
18 usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.
19 Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.
20 Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.

Hakuna mtu anapaswa kuwalaumu mafarisayo wala masadukayo ambao ni matawi yaliyokatwa kwa sababu hawakuliamini Neno la Mungu walipolisikia, kwa kuwa kosa lile walilolitenda ndivyo kilivyo kizazi hiki yaani madhehebu yaliyopo sasa. Naam, saa imewadia nayo ndio sasa.

Sikia eeh Laodikia, Yeye aliye na masikio na asikie.

Nyoka na Hawa
Nyoka na Hawa

Mawasiliano;

+255 755 251 999

Comments


bottom of page