top of page

NYAKATI YA SABA YA KANISA, LAODIKIA

  • Writer: mashibeelias2
    mashibeelias2
  • 2 days ago
  • 9 min read

NYAKATI YA SABA YA KANISA, LAODIKIA.


Kanisa la Laodikia ni nyakati kuanzia 1906 BK hata leo. Katika makanisa sita tuliyotoka kutazama, tumeona habari ambazo zinafanya ujue kanisa lilikopitia mpaka hapa tulipo leo. Jinsi kanisa linavyosafishwa kutoa hatua moja kwenda nyingine, na jinsi madhehebu yanavyozaliwa. Tumeona malaika sita waliotumwa na Mungu kwa kila kizazi na hakuna malaika hata mmoja ambaye alienda chuo cha theolojia kisha akawa mjumbe wa Mungu kwa ujumbe wa walimu wa theolojia (ufunuo wa damu na nyama). Bali wote walikuwa na ufunuo wa Mungu.


Mambo yote yaliyoandikwa katika kanisa hili yameandikwa kwa malaika wa kanisa lililoko katika nyakati hizi za kanisa, yaani kizazi hiki tulichopo sasa. Tutazame habari za Laodikia katika ufunuo 3:14-22.


¹⁴ Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

 YEYE ANENAYE


Sifa ya Yeye anenaye imekuwa tofauti na makanisa mengine, tofauti na kanisa la sita tulilotoka kuangalia ambalo alijitambulisha kama mtakatifu. Kizazi hiki tulichopo sasa ndio kinachofuata baada ya kanisa la sita, kwa ufunuo wa John Wesley. Lakini hapa Yesu Kristo anajitambulisha kwa kizazi hiki cha saba kuwa ni Amina! maana yake ni shahidi mwaminifu na wa kweli. Ni mwaminifu katika neno la Mungu, na wa kweli yaani husema kweli mbele za Mungu na kuishi ile kweli hata Yeye mwenyewe kuwa ile KWELI.


Maana yake ndivyo inavyopasa kanisa hili kuwa, ni kanisa ambalo anatazamia uaminifu katika neno lake na kunena au kufundisha yaliyo kweli. Sasa tuone jinsi alivyowaona ikiwa wanakaa katika uaminifu na ukweli kama John wesley na wa-methodist walivyokaa kwenye utakatifu kama Kristo alivyomtakatifu.


Kama alivyoanza kusema kuwa, na kwa malaika wa kanisa liliko laodikia, andika: maana yake ni habari ambazo zinaandikwa kwenda kwa malaika wa Laodikia ambaye ni William Seymour. Huyu anatokea marekani, alikuja na uamsho unaojulikana kama uamsho wa mtaa wa Azusa (Azusa street revival), Marekani. William Seymour alianza safari ya wokovu katika kanisa la Baptist, kisha Methodist na baadae ‘Evening light saints’ na ‘Apostolic faith mission’.


Kumbuka injili katika kipindi hiki ilikuwa imejikita katika utakatifu, sawasawa na ufunuo wa John Wesley. Wesley alifundisha hatua mbili za wokovu; 

1. Kuzaliwa mara ya pili (kazi ya kwanza ya neema)

2.Utakaso kamili (Kazi ya pili ya neema).


Katika utakaso kamili Wesley alisema ndio hatua ya kupokea Roho mtakatifu. Lakini baadae mjumbe wa kanisa hili la saba William Seymour akaja na ufunuo kuwa kupokea Roho mtakatifu ni hatua ya tatu baada ya utakaso kamili, yaani kulingana na William Seymour inakuwa;

1. Kuzaliwa mara ya pili(kazi ya kwanza ya neema)

2. Utakaso kamili (kazi ya pili ya neema)

3.Kupokea Roho mtakatifu.(utimilifu)


Ndipo hapa Seymour alipomwomba Mungu kwa watu ambao kimsingi wametokea katika fundisho la utakaso kamili kupokea Roho mtakatifu na karama za Rohoni na ikawa hivyo. Karama zikarudi, kunena kwa Lugha, kuwekea mikono wagonjwa n.k. Lakini pamoja na hayo, Bwana amewanena waliopokea karama hizi kama vuguvugu, haikuonekana mbele za Bwana kuwa wamefikia utimilifu kama alivyoona Wiliam Seymour. Sababu tutaijua mbele kidogo.


Kurudi kwa karama ikawa jambo geni katikakati ya waamini wengi kwa sababu zilikuwa zimekufa katika kanisa, zilibaki hadithi tu, na kurudi kwake ikawa ishara kama ila ya Pentecoste. Na tangu wakati ule yaani mwaka 1906 BK, wapentekoste tunaowajua leo wakazaliwa. Uamsho huu ulichukua mda mfupi kufika ulimwengu wote kuliko nyakati zote. Hivyo kila dhehebu la kipentekoste chimbuko lake ni huyu Wiliam Seymour. Ibada na mafundisho yakatijikita katika karama.


ONYO/DHAMBI YA KANISA HILI.


Kanisa hili au kizazi hiki hakijasifiwa hata kidogo, pamoja na kurejeshwa kwa karama, haikuonekana kuwa ni jambo la kusifiwa. Na badala yake karama hizo hizo ndio hasa zimefanya Laodikia (wapentekoste), wawe vuguvugu na kiburi. Tutatazama kwa nini!


Msitari wa 15 anasema;


¹⁵ Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
¹⁶ Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

Yesu Kristo anamwambia Wiliam Seymour na watoto wake (wapentecost) kuwa matendo yako si baridi wala si moto, bali ni Vuguvugu. Na kwa sababu ya uvuguvugu Yesu Kristo anasema nitakutapika  yaani kukukataa usiwe wangu(kama alivyomtapika Israeli). Huu ndio unabii wa wapentekoste wote duniani ambao ndio fedha inayopaswa kusafishwa mara ya mwisho ili kupata iliyo safi, Bwana anasema kwamba ni vuguvugu! 


Haijalishi jinsi ujionavyo ni moto, hiyo ni jinsi ujionavyo (Nani awezaye kuyajua makosa yake mwenyewe?), lakini mbele za Mungu ni vuguvugu. Na hakuna vuguvugu atakayeingia mbinguni isipokuwa kwa kuitii sauti ya Bwana leo hii (Ufunuo 3:20).


Sasa, unaweza kujiuliza kwa nini William seymour na wapentekoste ni vuguvugu wakati Seymour alichukua kilicho cha John Wesley aliyependwa na Bwana, akaja nacho hata akaleta matokeo ya karama ambazo Wesley hakuwa nazo?


Jibu ni kwamba John Wesley alikuwa sahihi kabisa hata yeye mwenyewe angeomba karama zingedhihirika. Nyongeza ya William Seymour ya kusema kwamba baada ya utakaso kamili ndipo mtu anapokea Roho mtakatifu haikuwa tafsiri sahihi, ijapokuwa alikuwa sahihi kuzitaka karama. Haikuwa sahihi kwa sababu lengo la injili au neno la Mungu kwa mwanadamu ni utakatifu (Waebrania 12:14) na si karama. Hivyo hata kama karama zingemwagwa kiasi cha kuhamisha milima, bado isingeonekana ni jambo la utukufu mbele za Mungu ikiwa wazitendao hawajafikilia utakatifu. Seymour na wapentekoste huruka hatua mhimu kuliko hiyo waitakayo. Yaani huweka msingi chini kisha wanaanza kujiandaa kupaua pasipo kujenga nyumba yenyewe.


Wapentekoste kama ilivyokuwa kwa William seymour wana bidii ya kutafta karama na zawadi kutoka kwa Mungu kuliko utakatifu, na wanapozipata wanatukana mambo makuu ya injili yaani utakatifu. Ndipo kwa sababu hiyo wamekuja na mafundisho lukuki kujaribu kuhalalisha maisha ya uvuguvugu katika kanisa, na kujitetea kuwa wapo sahihi kuwa vuguvugu.


Mafundisho ya neema ndio hasa yalipata nafasi kwa wapentekoste, kwamba kila kitu ni neema hata kuishi maisha matakatifu kulingana na neno la Kristo haihitaji bidii bali neema nyingi (Kama wanenavyo wakatoliki). Neema ikatukuzwa kuliko Neno la Kristo. Na kumfanya kila mtu asitii na kuishi katika Neno la Kristo. Na kwa uzihirisho wa karama, ndipo mioyo ya wengi inafanywa kuamini kuwa tayari wao ni watakatifu. 


Hapa ndipo watu hawa hawajengwi kuufikilia utakatifu, yaani kuwa na bidii bali wanajengwa kuridhika kwamba hivyo walivyo ndivyo iwapasasavyo hata kama Mungu bado anawashudia hawatanyakuliwa. Injili ya walokole ni ya kuridhika katika unyonge, kujigamba. Sineni kuwachukiza walokole maana mimi pia nimekulia huko, lakini nasema kwa jinsi ya Roho wa Bwana wapate kuona makosa yao ili wapate kuyaondoa sasa kabla ya ghadhabu ya Bwana.


John Wesley alipendwa na Bwana si kwa sababu ya kunena kwa lugha wala kuona maono wala ndoto au kutoa unabii bali kulipenda na kulishika neno la Mungu/Kristo. Lakini wapentekoste ni watu wenye kujikweza, hawatafti utakatifu ndani ya neno la Kristo bali wanatafuta karama/zawadi, mafanikio, faraja n.k. Jina la Kristo limekuwa ndio nguzo yao kuliko neno lake, (wanalo jina la kuwa hai lakini wamekufa vile vile). Bwana alinishuhudia hapo kwanza kwa ukali kuchukuliana na wapentekoste kiasi cha kuniadhibu nilipokaidi. Nilipewa ishara bayana kuwa Bwana amekusudia jambo baya juu ya wapentekoste kwa kumkataa yeye alipojifunua kwao mara ya kwanza kwenye miaka ya 1945 mpaka 1965. 


John Wesley alionywa kuwa shika ulicho nacho asije mtu akaitwaa taji yako yaani asije mtu akauondoa mwenendo wenu na matendo yenu. Maana yake hawakupaswa kumsikiliza hata William seymour, maana walikuwa bora mbele za Mungu kuliko wapentekoste. Hii ni inatoa tafsiri kuwa walokole si waaminifu na wa kweli kama Kristo.  


Wapentekoste ni mfano wa mtu aliyeambiwa panda hata katika kilele cha mlima huu ndipo utakapojipatia taji, lakini wapentekoste hawakuona haja ya kupanda mlima kuitwaa ile taji bali walijifanyia taji yao wenyewe kwa mfano wa ile iliyopo mlimani, wakaivaa. Hivyo kila mtu awatazamapo huwatazama kama washindi lakini Bwana ndiye awajua ya kwamba hawana taji iwayo yote. Ndipo kwa sababu hiyo aliwaambia ni vuguvugu, yaani hawana taji ya ushindi. Tazama maneno haya;


¹⁷ Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

Ufunuo 3:17


Haya ni maneno ya Kristo kwa William Seymour na wapentekoste kwamba hawataki kutubu au kukiri ya kuwa wameghoshi wokovu na kwamba wanabishana na Yeye aliyeifanya ile taji akaiweka juu ya mlima. Wapentekoste ni watu wanaojitawala, kama ilivyokuwa kwa katoliki. 


Hawataki neno isipokuwa walilo nalo wao, hawatazamii sauti ya Mungu kwa sababu wanayo taji tayari (taji waliyojifanyia), ndipo kwa sababu hii wanabishana na Mungu ambaye anawaona kuwa ni vuguvugu, masikini na vipofu na uchi, na kuwaita watubu lakini wao wanasema, sisi tuna kila kitu; karama, tunanena kwa lugha, wagonjwa wanapona, hukumu ya Mungu tunaijua, n.k. Hivyo hawana haja na kitu kingine. Naye Bwana kwa kushindana nao anasema, wewe si tajiri bali ni maskini, na kipofu na uchi.


Sasa huu ni wakati wa kufunuliwa kwa uchi wake na upofu wake, na umasikini wake ili kila mtu ajue na neno la Mungu litimie.  


Kama Bwana alivyonena kwa habari ya kizazi hiki yaani wapentekoste, kuwa nitakutapika utoke katika kinywa changu, ujue na kufahamu kuwa si yeye Bwana awatapikaye bali ninyi mmekwisha kumtapika yeye kwa mafundisho na maagizo ya wanadamu kama alivyotenda Israeli na katoliki. Ulizeni habari za Bwana alivyoutenda Shilo, Mnalijua kosa la Shilo? Ulizeni alivyoutenda Yerusalemu, Mnalijua kosa la Yerusalem? Ulizeni alivyomtenda Katoliki, mwalijua kosa lake? Naam, kaeni chini mtafakari, kwa nini Bwana alighairi mema juu yao na kumwaga ghadhabu.


Wapentekoste wapo hatua moja kabla ya unabii kutimia, kwa sababu wana bidii ya kushika mafundisho ambayo ni dhahiri yanamchukia Mungu. Kila kitu cha Mungu wanatengeneza, wanatengeneza karama zote kwa mfano wa zile karama za Mungu. Na kwa sababu hiyo hujiona ni matajiri.


Ndio sababu kwa nini kanisa hili likaitwa Laodikia! Maana tafsiri yake ni uongozi wa watu, yaani watu ndio wanaoongoza kanisa na sio Yesu. Wanamtaja Yesu kuwa ni kiongozi wao lakini wamemkana kila mahali, wakamhuzunisha na kumzimisha Roho mtakatifu, matendo yake yakaondoka yaani akaondoka, akawaacha wajiongoze.


Ndipo utaona kila karama wanayo ijapokuwa si kweli, bali ni maigizo. Wametoka kuigiza karama hata kujitungia nyingine ambazo ni za kumtukana Mungu moja kwa moja. Na kwa ujuzi huo hawahitaji karama ya Kristo kwa kuwa wanao uwezo wa kuwa nayo bila Yeye. Nao huwezi kuwagusa kwa sababu wanajiona ni matajiri. Hata ulimwengu wanawaona hivyo lakini si Bwana, ndio maana Bwana anasema;


¹⁸ Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
¹⁹ Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

Ni wazi kuwa utajiri wanaojisifu kwao hautoki kwa Mungu, maana asingepingana nao, ni utukufu wanaorithishana wao kwa wao kutoka vyuo vya kitheolojia kwenda walimu, wachungaji, na kanisa zima.


Ndipo kwa sababu hiyo anawaambia mstari wa 18 kuwa ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto yaani maneno safi ya Mungu ili kukufanya uwe tajiri, Dhahabu iliyosafishwa kwa moto ni maneno safi ya Mungu, nayo ni ujumbe wa Mungu kwa hili kanisa ili kuwaleta katika ukamilifu (waliukataa hapo kwanza, hii ni hatua ya mwisho katika kuonywa kwenu, hamtaki kuisikia sauti igongayo mlangoni mwenu, hamtasimama, bali mtatoweshwa kama umande utowekavyo.


 Bwana anasema, ununue mavazi meupe kwake yaani ufunuo utakaokufanya uwe Amina machoni pa Bwana yaani wa kweli. Na dawa ya macho upate kuona, yaani ufunuo utakaowafanya wapate kufahama makosa yao hata watoke kujiona matajiri. Kwa kuwa Bwana angali akiwapenda anawashauri yaliyo bora kwenu.


Sasa ufunuo huo ni upi? Na uko wapi? Maana hili ni kanisa la saba na wakristo (walokole) wanangoja unyakuo yaani kumwona Kristo mawinguni, hawangoji ufunuo uwao wote. Hawangoji Neno la Mungu bali kunyakuliwa, machoni pao ni wasafi na weupe hawana haja na nguo nyeupe anazozisema Kristo; lakini wasingekuwa vipofu kama wangejiona uchi, hawana nguo. Na kwa sababu hiyo lisikieni Neno la Mungu! Na ni aibu kusema tunangoja unyakuo tangu sasa kwa kuwa wataonyakuliwa ni wale waisikiao sauti ya yeye abishae mlangoni.


Yeye Bwana anasema;


²⁰ Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.


Ufunuo huo wa Kristo (dhahabu iliyo safishwa kwa moto) wanaotakiwa kuununua hautoki mbali hata waseme nani tumtume akatuletee, bali Yeye mwenye anauleta hadi mlangoni kwao. Ndio maana anasema nabisha, mtu akiisikia sauti yangu! Ufunuo huu ni mahubiri kama ya Nuhu wakati kizazi kile kinaitwa kitubu kisije kikaangamia. Nuhu alisimama milangoni mwao lakini kila mtu alijiona ni mtakatifu, hana haja na kitu kingine. Ndivyo na Kristo alivyozinena nyakati hizi akisema;


26 Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. 


27 Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. 

Luka 17:26-27


Kuka na kunywa sio kosa bali hapa inamanisha wanafanya yaliyo mapenzi ya nafsi zao kwa sababu wanazipenda. Wamejikita kumsumbua Mungu juu ya tule nini?, tunywe nini? wavae nini? watapata lini gari, kazi nzuri, mme, mke, pesa, umaarufu, ukuu, uchungaji, uaskofu, ualimu, n.k. Yote haya ni matamanio ya mwanadamu, na haya ndio wanayoyasumbukia usiku na mchana. Injili yao imebeba mambo hayo, tule nini? tunywe nini? Injili yao inahubiri kuipenda nafsi yako.


Yeye aliye mwaminifu na wa kweli anasema nasimama mlangoni, lakini ndani ya kanisa wanasema Yesu Kristo anakaribia kuja kutunyakua. Ni lugha mbili tofauti kabisa. Ndio maana anasema Yeye atakayeisikia sauti yake ataingia kwake. Maana yake atalipokea dhehebu lile liwe lake. Ni injili inayowahubiri walioitwa tu yaani wakristo hasa wapentekoste ambao ndio wanaoonywa hapa kuwa ni uzao wake lakini wamekengeuka, hawaendi mbele bali wanarudi nyuma. Ni injili kama alivyokuja kwa wayahudi akikataa kuhubri kwa mataifa. 


²¹ Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.


Yeye ashindaye ataketi pamoja naye katika kiti cha enzi cha Baba mbinguni. Sasa watakaoshinda ni hao watakaoisikia sauti yake yaani sauti ya malaika mwingine mbali na William seymour. Unaweza kujiiliza bado kuna malaika wanakuja kuhubiri?


Ndio, wapo tena Bwana amenishuhidia neno lake litakuja kwa njia ya malaika watatu na Neno lake Ufunuo 14:6-9 litakapotimia. 


Mlipaswa kuingoja Sauti yake abishae mlangoni (Ufunuo 3:20) na si unyakuo maana huo ndio unyakuo kwenu. Mtazimia bure mkingoja unyakuo ambao hauwahusu kwa sababu ni vuguvugu. Bali lisikieni neno la Mungu ili kuondoa uvuguvugu wenu kwanza ndipo mtakuwa na haki ya kusubiri unyakuo.


²² Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. 


Kama asemavyo ukatubu, naam, ukatubu!


Mawasiliano;

+255755251999

 
 
 

Recent Posts

See All
NYAKATI YA SITA YA KANISA, FILADELFIA

Tumetoka kuona jinsi kanisa la tano au nyakati ya tano ya kanisa ambapo Katoliki (roman catholic na orthodox catholic) waliitwa kutubu, lakini walikataa kutubu ili watakaswe kwa lile neno la Mungu. Nd

 
 
 
NYAKATI YA TANO YA KANISA, SARDI

Siku ya leo tunatazama nyakati ya tano ya kanisa la Kristo, utakaso wa nne wa kanisa la Kristo. Ni kipindi baada ya kanisa la nne, kuanzia mwaka 1520 BK hadi 1750 BK. Tafsiri ya Sardi ni wale waliotor

 
 
 
NYAKATI YA NNE YA KANISA, THIATIRA

Yezebeli alikufa miaka mingi kabla ya maneno haya ya kitabu cha ufunuo kuandikwa, hivyo mwanamke huyu hana uhusiano wowote na kilichoandikwa, lakini Yezebeli anayezungumziwa hapa ni kanisa. Kwa sababu

 
 
 

Comments


bottom of page