top of page

Theolojia ni elimu au ujuzi wa mema na mabaya, ni jumla ya tafsiri ya neno ya Mungu lililokuwako, lililoko na litakalokuwepo anayotoka nayo mtu asomapo maandiko. Kwamba katika tafsiri hizo hakuna Mungu isipokuwa kile ile theolojia inasema.


Neno la Mungu kimsingi linatoka katika kinywa chake, lililokuwako kabla ya sasa, lililoko wakati huu na likalokuwako.

 

4 Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ILA KWA KILA NENO LITOKALO KATIKA KINYWA CHA MUNGU.

Mathayo 4:4


Neno hilo la Mungu ndio nuru na kweli, na linapokuja kwa mara ya kwanza, ndipo wanadamu huzalisha nuru na kweli nyingine nyingi kutokana na tafsiri wanazozizalisha yaani theolojia ambazo huenda kinyume na lile neno la Mungu,  Kama asemavyo Mtumishi wa Mungu Isaya; 


10 Ni nani miongoni mwenu amchaye Bwana, aitiiye sauti ya mtumishi wake? Yeye aendaye katika giza, wala hana nuru, naye alitumainia jina la Bwana, na kumtegemea Mungu wake. 
11 Tazama, ninyi nyote mwashao moto, mjifungiao hiyo mienge; endeni ninyi katika mwali wa moto wenu, na katikati ya mienge mliyoiwasha. Mtayapata haya kwa mkono wangu; mtalala kwa huzuni. 

Isaya 50:10-11


Theolojia ni nuru kwa mfano wa taa au mwenge ambao watu hujiwashia ili kiwasaidie wakati wa giza. Lakini nuru hiyo imekuwa kana kwamba ndio tegemeo la watu hata kuwafanya kuikataa nuru halisi itokayo kwa Mungu. 


Ndio maana Isaya anawaambia madhehebu au hiyo mienge na mioto waliojiwashia (thelojia) kuwa mabaya watayapata kwa mkono wa Bwana, huyo ambaye wao kupitia mienge yao wanasema anatupenda.


Maana wameikataa nuru yake, wamemkataa Isaya na manabii wengine wakitumainia mienge yao. Katika biblia kuna neno la Mungu lilitoka kinywani mwake, hakuna theolojia. Theolojia ni roho ya mtu inayotafsiri yake maandiko, na tafsiri ile au theoloji ile itaenda kwa namna ya ile roho ya yule anayetafsiri. 


Tazama neno la Mungu na  tafsiri ya nyoka, alipotafsiri kwa Hawa.


16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, 
17 walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika. 

Mwanzo 2:16-17.


Hili ni neno la Mungu, kwa Adamu na Hawa, ni agano alilofanya na Adamu liwe kwake na uzao wake wote. Lakini Adamu alilivunja agano hilo kutokana na kumsikiliza mkewe aliyepewa na nyoka tafsiri isiyotoka kwa Mungu.


1 Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? 
2 Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; 
3 lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.
4 Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, 
5 kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. 
6 Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.

Mwanzo 3:1-6


Nyoka alikuja kama mwalimu kwa Hawa, akampa tafsiri ya maneno ya Mungu ambayo kimsingi siku zote huwa katika mafumbo, na hivyo huhitaji majibu. Hawa akakaa katika chuo cha huyu mwalimu na kujifunza ile theolojia yake, apate kuwa mwalimu. Akarudi kwa Adamu, mtu wa Mungu akamhubiria ile injili ya nyoka naye akakubaliana nayo.


Neno la Mungu kwa Adamu na Hawa likabadilika kutoka lile la Mwanzo 2:16-17, likawa hili la Mwanzo 3:4-5. Kicho/hofu yao mbele za Mungu ikawa hiyo ya pili, lakini ashukuriwe Mungu kuwa alipoiwaijiria Adamu na Hawa walitubu. 


Lakini katika vizazi vilivyofuata haviwezi kutubu kutoka kwenye ile tafsiri ya uongo (theolojia) na kutazamia kuja kwake Yeye aliyetumwa na Mungu. Kwa kuwa katika akili za watu waliopokea ile tafsiri ya uongo, huishika kuwa ndio Mungu. Na roho ile idanganyayo huwa ndio Roho wa Mungu kwao.


Theolojia ni roho kwa sababu, uongo mmoja ulioingia ndani ya neno la Mungu na kuwa ndio kicho au neno la Mungu kwa wale watu, huwa kiongozi wa namna ya kutafsiri maandiko yote yaliyobaki ili kuendena na uongo wa kwanza. Kwa sababu hiyo huendelea kusema uongo kwa kila neno la Mungu baada ya hapo.


Kile alichokisema nyoka ni mtazamo wa kweli kwake, na kila atayemwamini atakuwa na hiyo roho yaani huo msingi, au namna hiyo ya kufikiri. Ili kujenga juu ya fundisho la nyoka unahitaji kukaa shuleni ili upate ule ujuzi au ile roho na namna ya kufasiri maandiko kulingana na ile roho ya nyoka.


Maana yake mtu anayesomea theolojia, anasomea kuilewa ile roho ya ile theolojia, jinsi wao wanavyofasiri neno la Mungu ili apate kuwa mwalimu wa kuwafundisha wengine roho hiyo au namna ya kufasiri kwa jinsi ya roho hiyo. 


Kila dhehebu unaloliona duniani leo, ni roho mbalimbali za wanadamu zinazosimama kama mungu juu ya wale watu wa lile dhehebu. Na kwa sabahu hiyo kuna zaidi ya Mungu mmoja, kuna zaidi ya Kristo mmoja na zaidi ya Roho mtakatifu mmoja katikati ya watu waitwao kwa jina la Bwana.


Dhehebu hili kwa roho yao wenyewe, wako sahihi katika kila wanachokifanya, ni watakatifu kwa sababu mungu wao ni ile theolojia ambayo wameifanya wao wenyewe. Na kwa sababu haiwezi kuwaambia umekosea tubu, hawawezi kuwa na masikio ya kusikia neno la Mungu.


Ndipo neno la Mungu linapokuja kwao, huonekana ni upuuzi kwao kwa sababu tayari ni watakatifu na wenye haki kwa mjibu wa theolojia (Mungu wao). Kristo alinena neno hili juu ya theolojia.


8 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. 
9 Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu. 

Mathayo 15:8-9


Mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu ndio theolojia. Wakati Kristo  anahubiri haya alikuwa anaongea na madhehebu ya Israeli kama Wafarisayo, wasadukayo, waesene, na wazelote. Kila mmoja alikuwa na fundisho lake na ndio hofu yake mbele za Mungu. 


Kwa sababu theolojia si hekima ya Mungu bali ni ya wanadamu, na kwa kuifuata hiyo, NI KUMWABUDU MUNGU BURE, kama alivyosema;


9 Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu. 

Mathayo 15


Watazame wayahudi na theolojia zao, na jinsi walivyolikataa neno la Mungu kwa ajili ya miungu yao (theolojia zao). Au ni nani ataisikia sauti ya Kristo na kuitii akaicha miungu yake (theolojia yake?) leo, kwa sababu kila mmoja na Kristo wake, kila mmoja na roho wake mtakatifu. Je, hizo sio ibada za sanamu?


Ukishindwa kuelewa mafundisho ya katoliki ni kwa sababu huna roho mtakatifu wa katoliki, ukishindwa kuelewa mafundisho ya wasabato ni kwa sabahu huna roho mtakatifu wa wasabato. Maana kila fundisho limezaliwa kwa jinsi ya ile roho ya uongo ya dhehebu.


Dhambi inakuja pale ambapo roho hizi za wanadamu zinapewa jina la Bwana na kuitwa ni Roho wa Mungu. Kama nyoka alivyokuja kwa Hawa akiwa na roho yake mwenyewe na Hawa akamwona kuwa ni mtumishi wa Mungu. Kama Bwana angewaacha mda mrefu shingo ya Adamu na Hawa zingekuwa ngumu kuacha ile ibada ya nyoka.


Kwa sababu hiyo uzao wa theolojia ni uzao wa nyoka, ni watu waliozaliwa kwa uongo kama ule wa nyoka aliomhubiria Hawa. Ndio maana Yohana aliwaita watu wale kwa neno hilo.


7 Hata alipoona wengi miongoni mwa Mafarisayo na Masadukayo wakiujia ubatizo wake, aliwaambia, Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja? 

Mathayo 3:7


Pia Kristo aliwaita majina hayo, soma Mathayo 12:34, na Mathayo 23:33.


Basi sitaki nitumie maneno hayo mbele zenu leo ingawa ni haki kwangu, ISILIZENI SAUTI YA BWANA LEO. Theolojia ndio kizuizi kikuu cha watu kutubu, Ipo sababu nyingine iliyo sawa na hiyo inayowatesa watu wengi waliopokea neno la manabii wa Mungu na masikio yao yakaziba moja kwa moja ambayo nitasema juu yake siku nyingine Bwana akijalia.


Nitasema kama alivyosema Yeremia ambaye mnamwona kuwa ni nabii wa Mungu kwenu ijapokuwa hamtii neno lolote wala kwenda katika njia aliyoihubiri. Yeye alisema; 


8 Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati (Biblia) ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, KALAMU YENYE UONGO YA WAANDISHI imeifanya kuwa uongo.

Yeremia 8:8


Wale walikuwa na torati ninyi mnayo biblia, lakini hampo katika ile biblia bali mpo kwenye KALAMU YENU YENYE UONGO YAANI THEOLOJIA, ambayo ndiyo mnayoishi kwayo. Biblia kwenu ni ile tafsiri yaani theolojia, na kwa sababu hiyo Biblia imefanywa kuwa uongo kwa zile kalamu (tafsiri) zenye uongo (theolojia).


Je, ni nani aliye sahihi kuliko mwingine? Naam, yuko aliye bora kuliko mwingine miongoni mwenu, lakini si mbele za Mungu, maana mbele zake wote wameoza, wote wamepotoka, wote pamoja; hakuna hata mmoja aendaye kwa haki.


Wametenda mambo ya uharibifu, Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao; Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka.


Kumbukumbu la Torati 32:5.


Neno hili lilitimia kwa wana wa Israeli, limetimia na kwenu pia leo. ISIKIKIZENI SAUTI YA BWANA.


MAWASILIANO;

+255 755 251 999.

WASIO HAKI HUNENAJE KWA LUGHA?

HAKUTAKUWA NA UNYAKUO JUU YA KIZAZI HIKI!

THEOLOJIA NI NINI NA KWA NINI HULETA MAUTI?

MANABII NA MAKRISTO WA UONGO. Seh 2

MANABII NA MAKRISTO WA UONGO. Seh 1

        CHANGIA KUPITIA

 

          NMB:       22510119402

          MOBILE: 255755 251 999

​​

             MASHIBE ELIAS NTINGINYA

Mawasiliano:

 

+255 755 251 999

Mbezi, Dar-es salaam

  • Facebook
  • Instagram
  • X
  • TikTok
bottom of page