
Kizazi tulichopo ni kizazi cha siku za mwisho, ni kizazi cha mwisho. Na katika kizazi hiki ndipo manabii na makristo wa uongo unaweza kuwatambua waliopo na waliokuwepo.
Ili kuweza kuwatambua sharti wewe mwenyewe utambue majira na nyakati ulizopo, lakini pia na kile anachokisema Bwana Yesu juu ya nyakati hizi au juu yako.
Bila hivyo utaishia kujihesabia haki machoni pako mwenyewe hata kama wewe mwenyewe ndio nabii wa uongo au unaketi na kufundishwa na huyu nabii wa uongo.
Nimekwisha kuweka msingi wa kanisa la Kristo katika nyakati zote saba lilizopitia kuanzia Efeso hadi Laodikia ambalo ndio kanisa la mwisho kabla ya kurudi kwake Yesu Kristo. Nataka uelewe kwanza majira haya na kanisa lilivyo ndipo tukaone hao manabii na makristo wa uongo.
Unaweza kutembelea website hii kujifunza hizo nyakati saba za Kanisa la Kristo ili twende sawa. www.injiliyayesujioni.org.
Nyakati ya saba ambayo ndio hii tuliopo ni kanisa vuguvugu, na kwa kuwa ni vuguguvugu Yesu Kristo anasema ukatubu na kama sivyo atalitapika litoke katika kinywa chake. Kanisa hili la saba au kizazi hiki kipo juu ya dhambi iitwayo uvuguvugu.
14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
Ufunuo wa Yohana 3:14-20.
Hivyo kanisa zima yaani madhehebu yote katika nyakati hizi, yapo chini ya neno hili UKATUBU! Na ni vigumu kwa wengi kuweza kuelewa kwa sababu maneno yaliyotangulia kunenwa katika kanisa leo hii ni UNYAKUO,
Hii ni kwa sababu ya kanisa kuwa kipofu, halijui majira na nyakati, hata wakanena neno ambalo si nyakati yake na kuliweka kuwa katika majira haya. Unyakuo hautakuwa kwa kanisa vuguvugu bali neno la Mungu kwa Kanisa hilo ni KUISIKILIZA HIYO SAUTI YAKE ASIMAMAYE MLANGONI.
Sasa, kwa sababu kanisa la saba (Laodikia) ambalo kimsingi ndio wapentekoste lipo chini ya dhambi ya uvuguvugu, maana yake tayari linao manabii wa uongo ndani yake, lakini hao manabii wa uongo na walio chini yao wanasubiri manabii wa uongo!
Na kwa sababu hiyo watu hawa wanapaswa kuhubiriwa wakatubu, lakini kwao ni kinyume, kila atakaye waambia kutubu ni nabii wa uongo. Na sababu kubwa ni kwamba imenenwa katika hicho kitabu cha ufunuo 3 tulichotoka kusoma, mstari wa 17.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na KIPOFU, na uchi.
Kwa sababu hiyo hata Kristo asimamae mlangoni akibisha atakuwa wa uongo kwao, maana ni vipofu, hawajihesabu kuwa ni vuguvugu bali moto, na wakamilifu. Ijapokuwa wapo pia manabii wa uongo waliowazi hata machoni pa mtoto mchanga, kama wauzao mafuta, na maji na chumvi lakini hawawezi kuwakemea kwa sababu si haki kwao.
Maana ni sawa na kuangalia kibanzi katika jicho la nduguyo na kutaka kukitoa lakini unalo borti katika jicho lako mwenyewe. Maana kanisa lote katika kizazi hiki ni vuguvugu, utasemaje hawa ni manabii wa uongo, badala ya kutoa uvuguvugu wako kwanza. Ndio maana kila anayewakemea manabii wa uongo anakuwa anapingwa na Mungu yeye mwenyewe.
Hata wengi wamefika mahali wakaona kwamba, awe nabii wa uongo au wa ukweli, tumwachie Mungu. Sisi tuhubiri tu tulichojaliwa, tuhubiri tulichoitiwa. Hivyo kila mpendekoste anayepwapinga waziwazi hawa manabii wanaotafta utajiri kwa watu hujidhuru yeye mwenyewe.
Hivyo manabii wa uongo kwa walokole ni pamoja na hao manabii wa kweli wa Mungu, na kila ambaye hataki kuwa na injili vuguvugu waliyonayo. Kwa kuwa walokole ni watu wa maziwa, kila aliye na chakula kigumu ni nabii wa uongo, sisemi kwamba kila aliye na chakula kigumu ni nabii wa kweli hapana, bali kwa walokole manabii wote hao ni mamoja.
Maana tayari imekwisha tabiriwa ya kuwa watakuwako manabii katika siku za mwisho, hao ambao Bwana Yesu aliwaita malaika, ambao kazi yao itakuwa kutenga magugu na ngano.
41 Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,
Mathayo 13:41
Hawa malaika si malaika wa mbinguni wasio na miili kama tuliyonayo, bali wale walio na miili yaani wanadamu. Malaika ni mjumbe alitumwa na Mungu, na kwa sababu hiyo anaweza kuwa yule wa mbinguni au mwanadamu aliye katika uso wa nchi. Lakini kwa habari ya kuhubiri ni malaika walio wanadamu, ambao tunawaita manabii.
Hivyo, Bwana Yesu anasema katika siku za mwisho atatuma hao manabii kuja kutenga ngano na magugu, kuondoa kila uongo usiwe kwake tena. Lakini wapentekoste hawajui hilo kwa kuwa ni vipofu.
Hawajui majira wala nyakati ya kila jambo, nao wamejifanyia njia fupi kuwa wanangoja unyakuo. Na kwa sababu hiyo malaiaka watoapo ujumbe wao watawaita manabii wa uongo.
Jambo hili limekwisha tukia tayari na linaendelea, yaani hao malaika wamekwisha kuwepo na wengine wapo kuifanya kazi ya Kristo. Lakini hao walio wateule machoni pao (walokole), na vipofu, hawajui wala hawataki kujua.
Hivyo tunapotazama manabii wa uongo, ujue na kufahamu tunatazama manabii hao ya ndani ya wapentekoste, maana ndio uzao wa mwisho wa kanisa, na makristo wa uongo ni wale walio nje ya wapentekoste.
Nitarudia tena kusema, wapentekoste ni uzao wa Mungu wa mwisho, ambao umefikia katika majira ya kujaribiwa, yaani kuijiriwa. Kama alivyoijiriwa Israeli na kama alivyoijiriwa katoliki, ndivyo kuijiriwa kwao kulivyo. Kwa sababu hiyo itakuwa kwao kama alivyo katoliki kama hawatatubu.
Maana imenenwa yakini kuwa, NITAKUTAPIKA UTOKE KATIKA KINYWA CHANGU. Basi tutaenda kuangalia manabii na makristo wa uongo katika somo linalofuata.
Mawasiliano;
(+255) 0755 251 999