top of page

Wanikolai ni walimu au viongozi katika madhehebu au dini ambao huingiza fasiri za maandiko kinyume na Mungu,  maana tafsiri ya neno ‘nikolai’ ni kuteka madhabahu au ibada ya Mungu, ndio sababu kwa nini Kristo anaonekana yupo nje ya kanisa la Laodikia akibisha apate kufunguliwa mlango (ufunuo 3:20). Hivyo humwondoa Mungu ndani ya kanisa ili wao waketi yaani wasikilizwe na kuongoza.


Wanamwondoa Mungu katika ibada kwa njia ya neno, hupanda tafsiri ambazo zinarudisha mwenendo wa watu nyuma na si kwenda mbele. Tafsiri hizi zikiisha kukubalika neno la Mungu linakufa ndani ya watu. Ijapokuwa hawapingani na neno la Mungu moja kwa moja, bali kwa kutoa tafsiri zinazohalalisha yasiyo haki.


Wokovu halisi unakuwa umebatilika ijapokuwa watu wale waliosikiliza uongo wanabaki kutazamia ahadi za Mungu zitimie sawasawa na alivyonena. Ndipo hapa utaona kwa nini Bwana Mungu hulituma neno lake kwa kanisa na si kwa wale walio nje.


Siku zote imekuwepo roho isiyoonekana, isiyo dhahiri ikitenda kazi ndani ya kanisa tangu kanisa la kwanza yaani Adamu hata leo. Adamu alipewa amri asile matunda ya ujuzi wa mema na mabaya (Mwanzo 2:16-17), lakini akaja nabii wa uongo asemaye ametoka kwa Mungu, akatoa tafsiri ya maneno hayo ya Mungu kumfundisha Hawa maana yake (Mwanzo 3).


Ndipo Adamu akaanguka katika dhambi upesi baada tu ya kuachiwa neno la Mungu aishi katika hilo, maana ndimo ulimokuwa uzima wa milele.


Vivyo hivyo wana wa Israeli, walipewa agano la Mungu kwa njia ya Musa kusema msiende hivi bali nendeni hivi, msile hiki wala msishike hiki bali fanyeni yaliyo haki. Kisha baada kitambo kidogo wakaja walimu, marabi, manabii, makuhani n.k ambao tafsiri zao juu neno la Mungu ilikuwa inageuza maana halisi ya lile neno, nao wakaiondoa torati mioyoni mwa watu. 


Hao ndio manabii wa uongo, waliotafsiri neno la Mungu kama nyoka alivyotafsiri kwa Hawa. Israel akarudia uovu kama Adamu, ndipo kwa neno la Bwana akawajiria wana wa Yakobo kusema;


Hosea 6:4 Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema.
Hosea 6:7 Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana.

Israeli alidanganywa na walimu na makuhani na marabi na manabii wake waliofundishwa kusema uongo kwa jina la Bwana. Walimu wao kwa ujuzi wa kutunga uongo wakalibatilisha agano la Mungu, badala ya watu kutafta utakatifu wa Mungu wakatafta utajiri.


Pamoja na kwamba injili za walimu hawa zinatoka kwa shetani, bado wangali wanazihubiri kuwa zimetoka kwa Mungu. Na watu wanafuata uongo kwa sababu wameambiwa aliyesema ni Mungu wanayemwamini. Watu wanakuwa hawana budi kuamini uongo wasije wakamkasirisha Mungu; HUKO NDIKO KUANGAMIA KWA KUKOSA MAARIFA.


Tazama leo utakutana na mwalimu anasema ‘Mungu amesema unaenda kutajirika’ lakini maneno yale hayatoki kwa Mungu hata kidogo  bali yanatoka kwa mwalimu huyo akitumia jina la Mungu kuhalalisha uongo wake kuwa umetoka kwa Mungu na si yeye. Na watu kwa kuwa wanamwamini Mungu wanasema amen.


BAADHI YA MANENO NA TAFSIRI ZA WANIKOLAI.


》Ukikombolewa umekombolewa milele.

Fundisho hili kwa lugha ya kiingereza linajulikana kama ONCE SAVED ALWAYS SAVED. Mwanzilishi wa fundisho hili ni John Calvin (1509-1564) BK. Fundisho hili linajenga dhana kuwa wokovu haupotei, mara mtu anapomwamini Yesu Kristo amemaliza, haijalishi atarudia dhambi zake.


Ndipo wanaosikiliza uongo huu wanakuwa huru kuishi watakavyo, dhambi kwao inakuwa imekufa. Watende dhambi au wasitende hatima yao wanasema ni mbinguni. Kwa sababu hiyo fundisho hili humwondoa Kristo  ndani yao na kubaki midomoni mwao. Kwa sababu hatima ya injili ya Kristo ni kumtenga mwanadamu kutoka katika dhambi na si kumwaminisha hana dhambi angali anayo dhambi.


Lakini ukweli ni kuwa wokovu ni agano kati ya Mungu na Mwanadamu. Kwamba mwanadamu akienda sawasawa na neno la Mungu atakuwa na uzima wa milele yaani ataokoka. Adamu alipewa agano lile lile kusema hutakufa ikiwa tu hutakula matunda ya ujuzi wa mema na mabaya. Vivyo hivyo na Israeli, na katika  Kanisa la Kristo.


Hakuna ahadi ya kupata uzima wa milele pasipo kuishi katika neno la Mungu. Kuamini Msalaba hata shetani anaamini, tena si kuamini tu, alikuwepo wakati Yesu anasulubishwa. Kinachomwondoa katika uzao wa Mungu ni kusema uongo na kutokutii neno lake.


》TUMEOKOLEWA KWA NEEMA NA SI KWA MATENDO YA SHERIA.

Hili ni fundisho la Paulo kwa watu wa torati yaani wayahudi. Na Paulo alinena kwao kana kwamba kwa Kristo hamna sheria, hayo ni makosa! Maana Kristo alikuwa amekwisha kusema HAKUJA KUONDOA TORATI YAANI SHERIA BALI KUIKAMILISHA. Lakini naweza kumtetea Paulo kutokana na aina ya watu aliokuwa anashindana nao.


Watu hawa walikuwa wakiishi na tafsiri za uongo kama zile za nyoka, tafsiri kama za wanikolai, wokovu wao ukawa wa nje tu, kila mtu aonavyo vyema kujisifu lakini kiuhalisia walikuwa katika dhambi zile zile zinazokatazwa na torati.


Hivyo tofauti na mtu wa torati ukimhubiria mtu wa mataifa ambae  hakuwahi kuwa chini ya torati fundisho hilo linazaa uovu. Na hapa walimu na wachungaji ndipo wanapotia uvuguvugu na upofu kanisa. Kwa sababu tafsiri za wanikolai juu ya ‘neema na si matendo ya sheria’ zinalenga kumpa mtu kazi moja tu ya kuamini neema pekee.


Kana kwamba Kristo alikuja kuhubiri neema, wakati katika injili ya Kristo neno hilo halionekani hata mara moja. Lakini kwa sababu injili ilikuwa ni kutangaza kusamehewa dhambi bila sadaka yoyote mtu anayoleta kwa ajili ya ondoleo la dhambi, injili yake inakuwa inatafsirika kama neema.


Ndipo baadae ikajulikana na mitume kumbe Yeye mwenyewe ndio ile sadaka; Kumbe alijitoa sadaka yeye mwenyewe ili kuwa sadaka ya kila mmoja anayeamini. Lakini kanisa leo hii linaishi kwa kuamini kuwa neema hiyo inaendelea kila wanapotenda dhambi na ndipo kwa sababu hii Laodikia hataki kujitahidi kutoka katika dhambi asije akaonekana anaidharau neema ambayo ameipa jukumu la kusamehe kila dhambi anayoitenda.


Na kwa tafsiri hiyo, ili neema iwe nyingi ama kubwa kwa mtu, anapaswa kutenda zaidi dhambi, maana kama jukumu la neema ni kusamehe dhambi zake, inapaswa kuongezeka kadiri dhambi za mtu huyu zinapoongezeka. Haya yote ni ubatili na kujilisha upepo.


》Usihukumu, hubiri ulichoitiwa.

Kuna maneno maarufu kwa walokole kuwa usihukumu bali hubiri ulichoitiwa. Maneno haya yanatokana na tafsiri ya wanikolai ya andiko hili


1 Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi.
2 Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa.

Mathayo 7:1-2


Wanikolai hutumia maneno haya ili kuziba midomo ya waliyo upande wa Mungu, na kwa ujuzi wao waliona ili kuepuka kuhukumiwa, wanasema usimkanye mwingine kuwa anakosea bali mwache kwa kuwa ameitwa kufanya hicho anachokifanya.


Hayo ni maneno ya Ibilisi moja kwa moja, maana kama kuitwa ni kufanya unachokifanya bila kujali ni dhambi, inakuaje ahukumiwe anayehukumu wengine wakati na yeye ameitwa kuhukumu?


Tafsiri halisi ya maneno ya Kristo haikuwa hiyo ya wanikolai, bali ilikuwa kwamba ondoa kwanza dhambi yako mwenyewe kabla ya kukimbilia kutaka kuondoa za wengine. Maana ukikimbilia za wengine, Mungu atarejea kwako pia kukulipa sawasawa na ulivyohukumu au kuhubiri kwa wengine.


Lakini walimu wa kinikolai husema usihukumu, hubiri ulichoitiwa ili kuufanya uongo wao uishi, usije uongo wao ukakatiliwa mbali na wao pia.


》Mungu haangalii mwili bali anaangalia Roho.

Hili ni fundisho lingine la wanikolai, wapendao anasa na uzinzi na uasherati. Husema hivi ili kumpa mtu uhuru wa kutenda na kukaa na dhambi ikiwa tu mtu huyo anazitenda mwilini na yeye mwenyewe amempokea Kristo. Kwamba ikiwa mtu anampenda Yesu, inatosha, ndicho Mungu anachokitaka.


Ni kweli kuwa Roho ndio uhai ulimo, si katika mwili, maana mwanadamu ni kama Computer ilivyo, ina Software (programu) na hardware (vifaa). Roho ni kama software na mwili ni kama hardware,  lakini nani anaweza kuitumia software bila hardware. Wala hardware haina kazi yoyote pasipo software na software haina kazi yoyote pasipo hardware.


Hivyo Mungu aliunganisha mwili na roho ili matendo ya roho yadhihirike kwa njia ya mwili. Kwamba ili matendo ya roho yapate kujulikana, mwili ni lazima kuwepo. Hivyo matendo ya mwili ya mtu ndio roho yake ilivyo.


Lakini wanikolai wametenganisha, mwili unaweza kujiamulia mambo yake wenyewe, ukamchukia Mungu lakini Roho ikampenda! Ndipo wanikolai wanasema mwili ukimchukia Mungu kwa kutenda dhambi haina shida, Mungu ataangalia roho tu, na mtu huyu ataenda mbinguni. Ni mtu anayemchukia Mungu pekee na kupenda uovu anaweza kukubali injili ya namna hii, maana ni uongo wa kitoto kabisa.


》Kuungamanishwa na Madhabahu.

Hili ni fundisho la Laodikia,ni moja ya ufunuo wa wanikolai kujaribu kutoa sababu kwa nini watu hawafanikiwi licha ya kutimiza vigezo vya injili yao ya mali.  Ndipo huja na jibu kuwa hawajaungamanishwa na madhabahu, au wameungamanishwa na madhabahu isiyo na nguvu.


Fundisho hili la wanikolai ni sawa na lile lililokuwa kwa wasamaria, ambalo Yesu Kristo alitoa majibu yanayojitosheleza kama ilivyoandikwa;


19 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!

20 Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.
21 Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.
22 Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.
23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu.

Yohana 4:19-23


Bwana kupitia Yesu anaweka msingi ili kuwapata watu wamwabudie HALISI, yaani katika Roho na Kweli. Lakini mtu anaye tafta madhabahu yenye nguvu na huyu msamaria ana tofauti gani?

Wanikolai wamewarudisha watu kule kule Kristo alikowatoa. Na watu wanataka uongo uwe ndio Yesu Kristo kwao, huyo ndie wanaempenda na kumtumikia kwa mioyo yao yote na roho zao zote na akili zao zote na nguvu zao zote.


Laodikia ametajirika kwa mafundisho kama haya na mengine mengi. Ndio maana anasema SINA HAJA NA KITU KINGINE (Ufunuo 3:17). Ni kweli ametajirika, lakini ndiye maskini kuliko waliokuwa maskini kabla yake. 


Naam, ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA!


Yapo mafundisho mengi ya wanikolai, siku nyingine Bwana akijali nitaendelea kuyamulika.


Mawasiliano

+255755 251 999.

MANABII WA UONGO, Mahali wanakotoka

MANABII, NA AINA ZA MANABII

UJUZI WA MEMA NA MABAYA NI NINI NA KWA NINI NI DHAMBI

UADUI KATI YA UZAO WA MWANAMKE NA UZAO WA NYOKA

SABABU ILIYOPELEKEA ULIMWENGU WA KWANZA KUANGAMIZWA

        CHANGIA KUPITIA

 

          NMB:       22510119402

          MOBILE: 255755 251 999

​​

             MASHIBE ELIAS NTINGINYA

Mawasiliano:

 

+255 755 251 999

Mbezi, Dar-es salaam

  • Facebook
  • Instagram
  • X
  • TikTok
bottom of page