
Moja ya matukio ya ajabu kuwahi kutendeka katika historia ya mwanadamu ni kuangamizwa ulimwengu wa kwanza kwa gharika ya maji. Hadithi hii imekuwa ya kutisha na kuogofya hasa ikizingatiwa kuwa kuna unabii kama huo utatimilika tena kwa ulimwengu huu tulio nao.
Ulimwengu huu tuliopo umeandikiwa kuharibiwa pia kwa moto, na kwa sababu hiyo tukio lile la kwanza limeandikwa ili tupate kujifunza na kuogopa kufanya moja ya matendo ya wale watu wa ulimwengu wa kwanza lililopelekea kuharibiwa kwao.
Kosa lililopelekea kuharibiwa ulimwengu wa kwanza kwa gharika limefichwa katika fumbo. Ni kosa ambalo hata kizazi hiki au ulimwengu huu wa sasa unalitenda hata leo. Dhambi hii imeandikwa katika kitabu cha mwanzo 6.
¹ Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao,
² wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.
³ Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini.

Mpaka hapo tayari kosa liletalo uharibifu lilianza kuonekana hata Bwana Mungu akaipunguza miaka ya mwanadamu kuishi. Kosa hilo linaanza kwa uzao wa Mungu kushirikiana na kuona na uzao wa wanadamu.
Kimsingi hapa hauzungumziwi uzao wa kimwili kati ya mwanaume na mwanamke, hapana. Ijapokuwa uzao wa Mungu na uzao wa mwanadamu wote ni wanadamu waliozaliwa kimwili na mwanamke.
Kama ilivyo kwa wakristo wanavyosema kuwa wana wa Mungu kwa njia ya Kristo (ijapokuwa wameshamwacha), si kwa sababu malaika fulani walishuka wakazini na mwanadamu kisha wakazaliwa wao, hapana, bali kwa neno la Kristo.
Uzao wa Mungu inamaanisha ni watu wote waendao kwa sheria za Mungu, wamezaliwa kwa neno la Mungu. Na uzao wa mwanadamu ni wale waliozaliwa kwa mafundisho ya uongo.
Kosa la kizazi cha kwanza lilianzia pale wanadamu walipoongezeka kama inavyosema mstari wa kwanza. Uzao wa Sethi walio wana wa Mungu na uzao wa wanadamu walio uzao wa Kaini wakakutana. Uzao wa Sethi ulio wa Mungu ukatwaa binti za Kaini kuwa wakeze.
Ndipo ibada za Kaini zikaingia kwa uzao wa Mungu, Ujuzi wa mema na mabaya wakauiga wana Sethi kutoka kwa hao binti za Kaini. Jambo hili alikuwa amelikataza Bwana Mungu kwa wana wa Sethi kabla hawajakuwa karibu kama alivyowakataza wana wa Israeli kuona binti za kanaani kabla Israeli haijafika kanaani.
Baada ya kutenda kosa hili, wana wa Mungu walianza kufanana na wana wa wanadamu. Na kwa sababu giza na nuru havikai pamoja, ndipo ikazaliwa injili mpya, injili isiyo giza wala nuru, si moto wala baridi. Desturi za mataifa zikawa ndio ustaarabu wa kuigwa kwa wana wa Mungu. Waakacha kumtegeme Mungu kwa sababu walikuwa na theolojia.
Mwanzo 6
⁴ Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile;tena ,baada ya hayo ,wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu,wakazaa nao wana;hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani ,watu wenye sifa.
⁵ Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.
⁶ Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.
⁷ Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani; kwa maana naghairi ya kwamba nimewafanya.
⁸ Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.
Wanefili ni uzao wa kaini, na waliendelea kuzaliwa katika ndoa kati ya wana wa Mungu na wana wa wanadamu. Watoto waliozaliwa katika ndoa hizi ambao kimsingi walikuwa na haki ya pande zote mbili, wana wa Mungu na wana wa wanadamu pia. Ndio waliobadili majira nyakati.
Watoto hawa walikuwa kizazi kipya, ni sawa na watu wasemavyo watoto wa 2000. Tabia zao na matendo yao hayaakisi upande wowote, aidha kwa wazazi wao au kwenye Neno la Mungu. Wanaenda kwa jinsi ya roho zao.
Ndivyo walivyokuwa kizazi kile kilichozaliwa kati ya uzao wa Mungu na uzao wa mwanadamu, walikuwa hodari na wenye sifa (people of renoun). Kama tuwajuavyo watu wenye sifa leo, wanamziki, waigizaji, wachezaji wa mpira, wanasiasa, manabii wa uongo wapendao fedha n.k.
Ndani ya nyumba ya Bwana kukageuka kuwa biashara, wenye mali wakawa ndio watu wa Mungu. Wachungaji wapumbavu ndio wakaitwa waungwana na kupewa heshima mpaka serikalini. Kizazi kikaoza kuanzia nje hadi ndani ya nyumba ya Bwana.
Kila aliyejaribu kupingana na mfumo ule, kanisa lilimtupa nje, na serikali ikamwona mwenye kuleta na kusababisha vurugu. Lakini Nuhu alisimama upande wa Mungu, upande uliokuwa unachukiwa na kila mtu, dini, madhehebu na serikali.
Kila mtumishi wa Mungu aliyetumwa kuwahubiria watu hawa aliishia kula na kunywa nao, yaani kufuata njia zao za upotofu. Sio kwamba Nuhu alikuwa mhubiri peke yake aliyetumwa kwa kizazi kile, hapana, bali walikuwepo watumishi wengi ambao waliishia kumezwa katika uongo na nguvu za watu wale.
Kila mtumishi aliyetumwa na Bwana walimpiga kwa ndimi zao, na kwa sababu umma ulikuwa upande wa uongo kama ilivyo siku zote, nguvu za watumishi wa Mungu ziliyeyuka mapema.
Ndipo kwa nini Bwana Mungu akasema SITASHINDANA NA MWANADAMU MILELE. Maana yake hao watu walishindana na manabii wa Mungu wakashinda, kama Israel alivyotenda. Kwa maneno mengine uongo wao ukazidi kustawi.
Nuhu pia akahubiri kwa kanisa lipate kutubu, lakini milango yao ilikuwa imefungwa, kanisa lilikuwa halina haja na kitu kingine. Nuhu hakufanikiwa kumgeuza hata mtu mmoja aje upande wake. Hata akapewa ufunuo kutoka kwa Mungu kuwa dunia inaenda kuangamizwa, lakini wengine (madhehebu) waliendelea na mafundisho yao kupokea baraka za utajiri na biashara na kutazamia wakati wa amani na kesho yao kuwa bora.

Injili ile ya damu na nyama ndio ilifanya mioyo ya watu wale kuwa migumu. Walikuwa wasafi machoni pao, watakatifu machoni pao, wenye kumpendeza Mungu machoni pao. Maana injili yao ilikuwa kupamba kwa nje. Waliona nuru katika ulimwengu na kwamba mungu wao anaabudiwa kila sehemu katika ulimwengu, wakafirijika kwa bidii yao.
Naam, hawakutambua kuwa injili yao ilitia giza ulimwengu badala ya nuru na laana badala ya baraka. Nuhu alihubiri kinyume na ile injili, wala hakufanikiwa kuwageuza. Maana watu wale walikuwa kama wale aliotumwa Ezekieli.
3 Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali.
4 Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli ukawaambie maneno yangu.
5 Maana wewe hukutumwa kwa watu wa maneno mageni, ama wa lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli;
6 si kwa watu wa kabila nyingi wenye maneno mageni, na lugha ngumu, ambao huwezi kufahamu maneno yao. Bila shaka, kama ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza.
7 Bali nyumba ya Israeli hawatakusikiliza wewe; kwa kuwa hawanisikilizi mimi; maana nyumba yote ya Israeli wana vipaji vigumu, na mioyo yenye ukaidi.
Ezekieli 3:3-8
Watu wenye maneno mageni ni watu walio nje na biblia, wao wana dini (miungu) nyingine, Na kwa sababu nabii anatumwa kutokea katika neno la Mungu lilopotoshwa, kwenda kwa watu walioshika upotofu wa lile neno, ndipo inakuwa vigumu watu wale kuelewa neno.
Badala yake hushindana na Nabii, maana neno lake linapinga mafundisho yao ambayo kimsingi ndiyo wanahesabu kuwa ni kweli, lakini ni injili ya nyoka.
Nuhu alihubiria watu wa madhehebu, watu ambao wanayo theolojia kuwa ndiye mungu wao. Aliomba rehema na fadhili za Mungu juu ya kizazi kile, kwamba badala ya Kuwaangamiza awarehemu lakini haikuwezekana, kikombe cha hasira yake kilikuwa kimejaa tayari. Badala yake akapewa watu wa nyumbani mwake tu.
Yesu Kristo alisema jambo lile lile litajirudia katika majira haya;
26 Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu.
Luka 17
Lakini injili ya kizazi hiki (Laodikia) ni kutazamia mema na amani. Na siku hizo za Nuhu wamezifikilia tayari na kutenda yaliyo chukizo wala hawazitambui. Maana Yesu Kristo amenena juuya kizazi kuwa vipofu (Ufunuo 3:17).
ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA!
Mawasiliano;
+255 755 251 999