top of page

Manabii ni wingi wa neno nabii, na tafsiri ya neno nabii ni mtu aliye na unabii. Unabii ni ujumbe kutoka kwa Mungu, na kwa sababu hiyo nabii ni mjumbe aliye na ujumbe wa Mungu.


Hivyo ili aitwe nabii sharti awe ana ujumbe wa Mungu au ametumwa na Mungu. Lakini tunao manabii wengine wasemao ni manabii, na ujumbe wao huwa hauna joto la Mungu na wakati mwingine ni kinyume kabisa na Mungu. Na watu kwa kukosa maarifa huwatazama wanabii hawa wote kuwa manabii wa Mungu.



  1. MANABII WALIOFANYWA NA MUNGU KUWA MANABII.


Manabii wa namna hii ni wale walio na ujumbe utokao kwa Mungu. Nao wametumwa na Mungu kusema au kuhubiri kwa niaba yake. Kuna aina mbili za manabii wa Mungu.


a) Manabii walio na ujumbe mrefu kwa njia ya ufunuo.


Manabii hawa hutumwa kwa jamii au taifa au ulimwengu wote. Ujumbe wao huupata kwa njia ya ufunuo na kuuhubiri kwa kipindi kirefu katika kizazi cha uovu. Neno lao ndio Mungu na Roho wa Mungu, na ndio kazi na sauti ya Mungu kwa watu wa kizazi kile. Na wakiisha kumaliza ujumbe wao huondolewa na Mungu aidha kwa kutiwa mikononi mwa waovu, au kwa maradhi na hata ajali kulingana na njia zao zilivyokuwa.


Manabii hawa ni kama Musa, Yeremia, Isaya, Ezekieli, Yesu n.k, ambao ujumbe wao ndio Neno la Mungu. Pia wanaweza kupokea ufunuo kwa njia ya maono na ndoto. Katika agano jipya wanaitwa malaika, kwa sababu agano jipya halijatumia neno nabii kwa watu hao bali malaika. 


Tafsiri ya neno Malaika ni ile ile ya nabii ijapokuwa wengi hawafahamu hilo. Wengi huwanena wale walaika wa makanisa saba katika  ufunuo 2 na 3 kama malaika wa mbinguni. Lakini ni wanadamu na manabii kama wale wa agano la kale.


Tafsiri ya Malaika ni mjumbe aliyetumwa na Mungu, aidha ni wa mwili huu wa nyama au roho kama hao walio mbinguni. Wote hutumwa na Mungu kutimiza kuzudi lake. Lakini kwa habari ya kuhubiri, Bwana Mungu hatumi walio mbinguni bali walio chini hapa duniani.


b) Manabii walio na ujumbe mfupi kwa njia ya maono na ndoto, (manabii wadogo).


Manabii hawa huwa ndani ya ujumbe wa nabii wa ujumbe mrefu. Hawana ujumbe wa kuhubiri isipokuwa huo walioukuta, nao huwa na karama ya maono na ndoto kwa ajili ya kanisa, mfalme au mtu binafsi. Hawa walijulikana pia kama waonaji katika Israeli.


Katika agano jipya, yaani agano la pili au agano la Mungu kwa njia ya Yesu Kristo wa Nazareti, unabii unachorwa zaidi kama karama. Na nabii ni mtu mwenye karama ya unabii, anayeona maono n.k. Hii ni kwa sababu ya injili ya Paulo wakati anaelezea Karama.


11 Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; 
12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; 
Waefeso 4:11-12

Ndio maana katika agano jipya ukizungumzia nabii, masikio ya kila mtu hukimbilia kwenye aina ya karama aliyonayo kama ni uponyaji, utambuzi, uonaji n.k. Na kwa sababu hiyo wengi huchukulia moja kwa moja kuwa nabii ni mtu mwenye karama ya unabii. Lakini sivyo, karama ya unabii hasa katika agano jipya inaweza kuwa kwa mtu yeyote hata kama hajui neno vizuri, kwa sababu karama ni kama mlango katika nyumba, haina kigezo cha uzuri wa nyumba kuwepo.


Na karama hii ndio inayoongoza kuwafanya watu wengi kuwa manabii wa uongo, kwa sababu karama hiyo inapodhihirika kwao, kisha wakaenenda kwa mafundisho ya uongo kutokana na ujuzi wa mema na mabaya huwafanya waendelee kuaminika na watu kwa sababu ya maono na utabiri wanaoutoa.


Na pia kwa sababu watu huwamulika manabii hawa kama wale walio na neno la Mungu kwa njia ya ufunuo, na manabii hawa wadogo kwa kutamani heshima na ukuu huwalaghai watu kwa maneno yao kuwa wao ni manabii kama Isaya au Elia au Musa au Yeremia n.k. Hujiumusha waonekane ni manabii na mda mwingi hutumia kufundisha mafundisho ya kuwafanya watu wawaone manabii, watu wa kutukuzwa na kupewa heshima.


Lakini hawana ufunuo uwao wote kutoka kwa Mungu, bali mafundisho yao ni hayo hayo ya wengine. Kimsingi hawa sio manabii, lugha nzuri ya kutumia ni waonaji, mda wowote wanaweza kuwa kama Baalamu, wakaona maono na kuwaongoza watu katika upumbavu. Kwa sababu hawana Roho wa Mungu isipokuwa wana lango ambalo Roho wa Mungu anaweza kulitumia na shetani vile vile.

 

  1. MANABII WALIOFANYWA NA WANADAMU KUWA MANABII


Manabii hawa ni wale wanaofundishwa kuwa manabii. Hii inatokana na lile tunda la ujuzi wa mema na mabaya, uwezo wa kuumba jambo au uhusika. Mafundisho yao ni theolojia walioyofundishwa na kazi yao kubwa ni kuigiza kuwa manabii, kwa kuangalia tabia za manabii.


Kama wafanyavyo watu wa filamu, kujitengezea uhusika usio wa kwao na kuigiza kama mtu fulani. Ndivyo na manabii hawa, hutengenezwa kuvaa uhusika na karama fulani ili wawe kama manabii. Hawana ufunuo wa Mungu wala karama kama wanaowaiga, lakini wanataka kufanya matendo fulani waliyoyafanya wale.


Kama nabii au mtume aliponya mtu kwa kitambaa, na manabii hawa nao wanachukua kitambaa cha kutembea nacho wakisema kitambaa kina upako wa mtume au nabii fulani. Na hapo anakuwa ameijitengenezea karama. Anaweza kutumia chochote akakipa upako yeye mwenyewe na ukimuuliza atakuambia nabii au mtume fulani mbona alifanya. Anasema hivyo kwa sababu ameiga kwa huyo.


Tofauti yake na huyo nabii au mtume aliyemwiga ni kuwa Mungu ndiye alyetumia kitambaa na sio akili zake, wala kuiga kwa mtu au nabii au mtume fulani kabla yake. Hivyo manabii hawa hutafta sana kila mmoja kitu cha kipekee cha kuiga kiwe kana kwamba kafunuliwa. Hata wengine huenda mpaka kuzima wakitafta karama za kutengeneza. Isaya aliwanena watu watu pia akisema,


7 Umeweka kitanda chako juu ya mlima mrefu ulioinuka sana; ukaenda huko ili kutoa dhabihu.
8 Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako; kwa maana umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona.
9 Ulimwendea mfalme na mafuta ya marhamu, ukaongeza manukato yako, ukawatuma wajumbe wako waende mbali, ukajidhili sana hata kuzimu.

Isaya 57:7-9


Manabii wa namna hii wamekuwepo kila kizazi, Isaya anasema juu ya watumishi hawa kuwa wametafta nguvu za kiroho kila mahali, milimani, kwa wapagani, madhabahu za miungu na hata wamefika kuzimu wakitafta karama ili wapate heshima kwa wanadamu. Ndivyo manabii hawa walivyo kila kizazi, leo katika kizazi hiki, kuzimu wameshafanya nyumbani kwao kabisa.


Kisha wakiisha kupata uganga hurudi kufundisha upumbavu, wakijiumusha na kujivika utukufu kama wanaoupata manabii wa Mungu waliopita (ijapokuwa manabii wa Mungu hawajupata utukufu wowote nyakati zao) ili watukuzwe na watu, wapate heshima na mali. 


Wanafahamu fika hakuna nabii wa Mungu aliyepata kuwa nabii kwa kufundishwa na mtu, au kwa kuiga miujiza au karama, kama wao wanavyofanya. Lakini ujuzi wa mema na mabaya unatenda kazi na kwa sababu hiyo hawamwitaji Mungu kuwafanya wawe manabii. Kristo aliwanena;


44 Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti?

Yohana 5:44


Nabii mmoja hutengeneza maelfu ya manabii. Mmoja awe na karama hii, mwingine karama ile n.k. Na wengi huchagua wenyewe karama wanazotaka, kisha wanaanza kuzifanyia ujuzi ziongee, zitabiri n.k, kama mtu atengenezavyo sanamu na kuiomba imtabirie. Naam, ndio ibada mpya za sanamu.


  1. WANABII WALIOJIFANYA KUWA MANABII.


Hawa ndio wabunifu wa mafundisho ya uongo (Profane teachings inventors), ni walimu wabobezi katika uongo, wana vyuo vya kuzalisha walimu wengine, karama, n.k. Juu ya watu hawa hakuna Mungu isipokuwa wao wenyewe japo wanaweza wasijinene hivyo lakini ujuzi wao tu unaakisi hivyo.


Na kwa sababu ni walimu wa walimu, ni wakuu kuliko watu wote. Wanaweza kujiita nabii mkuu, mystic, general, the most high, Katapila, majestic, buldoza n.k. Mara nyingi hujiumusha kwa kujipa majina makubwa makubwa wakijionesha wao wako juu zaidi kuliko manabii wa uongo wanaoanza.


Majina haya wanajipa wenyewe na si Mungu, maana hawatafti utukufu wa Mungu bali wa wanadamu. Wala hawafanyi kazi hiyo ya utumishi kwa ajili ya Mungu, hapana, bali kwa ajili ya nafsi zao tu. 


Mungu hakuwatuma ila walikwenda kuhubiri, ndio maana hawatafti kumpendeza yeye, lakini wanatumia jina lake na kumpamba majukwaani kwa mngongo wa chupa. Ni wajumbe waliotoka na kujifunza kule alikotoka na kujifunza nyoka kabla ya kumwijia Hawa (Mwanzo 3).


Hawa wanaweza kuwa na karama yoyote wanayoitaka na mda wowote, ilimradi inaleta utukufu mkubwa kutoka kwa wanadamu. Wanaweza kubeba zaidi ya karama moja au kujisifu kwa majina zaidi ya moja. 


Njia yao ni pana, haisongi, na mtu akijaribu kuifanya isonge watamuua kwa ndimi zao na nguvu ya mikia yao, maana wanayo mikia. Manabii hawa waliofanywa na mwanadamu pamoja na wale waliojifanya kuwa manabii wanaweza kutumia ushirikina na nguvu zozote za adui kutafta utukufu wa wanadamu.


Hawa ni walimu wazuri, na huheshimiwa kuliko manabii wa Mungu siku zote, na kupewa utukufu na watu waichukiao kweli. Nao wamepewa kufanya kazi kwa mda na majiira, kisha wataangamia kwa ufunuo wa kuwepo kwao. Naam, mwenye masikio na asikie.


ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA!


Masiliano;

+255 755 251 999.

MANABII WA UONGO, Mahali wanakotoka

MANABII, NA AINA ZA MANABII

UJUZI WA MEMA NA MABAYA NI NINI NA KWA NINI NI DHAMBI

UADUI KATI YA UZAO WA MWANAMKE NA UZAO WA NYOKA

SABABU ILIYOPELEKEA ULIMWENGU WA KWANZA KUANGAMIZWA

        CHANGIA KUPITIA

 

          NMB:       22510119402

          MOBILE: 255755 251 999

​​

             MASHIBE ELIAS NTINGINYA

Mawasiliano:

 

+255 755 251 999

Mbezi, Dar-es salaam

  • Facebook
  • Instagram
  • X
  • TikTok
bottom of page