top of page

Uvuguvugu katika hali ya kawaida ni hali ya joto kiasi au kidogo. Yaani si moto kabisa wala si baridi. Maji ya uvuguvugu mtu anaweza kuyashika au kuoga lakini si yake ya moto.


Katika hali kama hiyo, Kanisa limetajwa kuwa nayo. Kwamba si moto wala baridi bali ni vuguvugu. Na kwa sababu ni kanisa maana yake ni watu walio juu ya moto fulani na lengo la moto huo ni kuwafanya wawe moto.


Ufunuo wa Yohana 3:14-16


14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

Hili ni kanisa la saba katika yake makanisa saba kuanzia ufunuo sura 2 hadi sura ya 3. Kiufupi ni kanisa moja isipokuwa limepitia nyakati saba za kuijiriwa na Mungu. Hili la saba ni vuguvugu, si baridi wala si moto. Naye Bwana anasema kwa kuwa ni vuguvugu nitakutapika utoke katika kinywa changu.


Kutapikwa ni kuachwa, mfano mzuri ni taifa la Iraeli, hakukuwahi kuwa na taifa lenye hofu ya Mungu kama Israel, na kupendwa na Mungu kama Israel. Lakini sote tunajua leo, Mungu aliwatapika, aliwaacha mpaka watakapo mtambua Yeye walimchoma kuwa ndiye (Luka 13:35).


Hapa napo anasema kwa kuwa ni vuguvugu nitakutapita utoke katika kinywa changu, maana ni kuachwa kama alivyoachwa Israel na wala hapa hakuna ahadi ya kurudiwa. Kanisa la Laodikia ndio kizazi hiki, yaani wakristo kuanzi miaka ya 1906 hata leo. Wanalo neno la Mungu ndani yao, Neno ambalo si moto wala baridi bali vuguvugu.


Hivyo, Neno la Mungu ndio yale maji na Roho mtakatifu ndio moto. Maji yatachemka kulingana na kiasi cha moto. Moto ukiwa mdogo, maji yatachemka kidogo. Na ikiwa hakuna moto, maji yatakuwa baridi. Hivyo kanisa kuwa vuguvugu ni kuwa na moto kidogo.


Na kwa sababu moto ni Roho mtakatifu; maana yake wanaye Roho mtakatifu kidogo. Roho mtakatifu alitumwa ili kulifikisha kanisa katika ukamilifu kwa sababu aliyepaswa kuifanya kazi hiyo alipaswa aondoke yaani Yesu Kristo. Hivyo Kristo aliondoka akaliacha kanisa kama mtoto aliyetoka kuzaliwa.


Maana yake halikuwa takatifu bado, na ndipo akatuma Roho mtakatifu ili aendelee kufundisha kanisa mpaka kanisa liwe takatifu, lifikie utimilifu na kuishinda dhambi. Miaka hii elfu 2 imepita kazi ya Mungu ikiendelea kutendeka ili kuuleta utimilifu.


Yohana 16 (Biblia Takatifu)


⁷ Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.
⁸ Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.
⁹ Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi;
¹⁰ kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena;
¹¹ kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.
¹² Hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyastahimili hivi sasa.

Roho mtakatifu alianza kutenda kazi ya Yesu Kristo kana kwamba Yesu Kristo yupo, hakuongeza wala kupunguza isipokuwa kueleza yale ambayo kanisa halikupasa kuyasikia hapo awali kutoka kwa Yesu Kristo kwa kuwa bado walikuwa watoto wadogo. Ndipo Yeye anachukua nafasi kwa sababu hana mwili wa nyama kama huu tulio nao, ambao Kristo pia alikuwa nao, azije akazeeka akaondoka kwa sheria ya mwili.


Hivyo Roho mtakatifu alipewa kukaa na kufundisha vizazi vyote kwa sababu yupo nje ya sheria za huu mwili ilio chini ya hukumu ya kifo, maana Kristo angebaki angebidi asubiri kuitimiliza huduma yake miaka elfu mbili. Na mambo yaliyosalia ambayo alikuja ili kuyafundisha ni matatu; Dhambi, Haki na hukumu.


Dhambi, haki na hukumu ni vitabu vitatu ambavyo ndio Biblia. Kila kilichoandikwa katika Biblia kimeandikwa kuhusu vitabu hivyo vitatu tu. Kwamba lipasalo kutendwa yaani lililo haki, na lisilo haki (lisilopasa kuyendwa), kisha hukumu ya wale watendao dhambi, yaani yasiyo haki.


Sasa, kwa nini nimesema Dhambi, haki na hukumu ni vitabu vitatu? Ni kwa sababu unaanza ukurasa wa kwanza kwenda wa pili hata mwisho wa kitabu. Hivyo Yesu Kristo alielezea utangulizi wa vitabu hivyo. Na kanisa limepitishwa katika nyakati saba kama madarasa saba ya kujifunza dhambi, na haki na hukumu katika namna mbalimbali.


Ndio maana utaona anaonya kwa habari ya dhambi ya kila kanisa, na kanisa ambalo lilitembea kwa jinsi ya utendaji na ufunuo wa  Roho mtakatifu kipindi husika, halijaonywa kutubu. Nayo ni makanisa mawili peke yake; Smirna na Filadelfia. Mengine yote pasipo kutubu kuna hukumu kwa sababu wametenda dhambi.


Hivyo tukiacha yale mengine sita yaliyokwisha kupita, tuone dhambi ya kanisa la saba yaani LAODIKIA.


Ufunuo wa Yohana 3:17-18.


17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

Laodikia ni kanisa la mwisho, yaani nyakati ya mwisho ambayo ndio sasa. Na kanisa lililozaliwa baada ya kanisa la sita ni Wapentekoste ambao ni maarufu kwa jina la WALOKOLE. Hawa ndio walipaswa kuhitimisha kijiti cha mwisho yaani kuwa WAKAMILIFU.  Lakini hapa wanaonekana kuwa si moto wala si baridi bali ni VUGUVUGU!


》Si moto maana yake hawaijui bado dhambi, haki na hukumu katika ukamilifu wake.


》Si baridi kwa sababu wamelipokea neno la awali la Kristo na kuanza kujifunza kwa habari ya dhambi na haki na hukumu, inagawa hawavijui vitu hivyo katika utimilifu wake bado.


Na kwa bahati mbaya kanisa hili limejivika taji yake lenyewe kwamba kazi limeimaliza na limeshinda, na hivyo linasubiri Unyakuo liende mbinguni yaani linasubiri Yesu Kristo arudi alitwae mbinguni au atawale nalo hapa duniani, n.k. Wakati huo huo Bwana Yesu anasema litubu na kama halitaki kutubu kutoka katika uvuguvugu, atalitapika yaani kulitupa nje kama alivyoitupa Israel.


Uvuguvugu wa walokole (hapa nasema walokoke kwa sababu wengine wametangulia kabla yao, nao wakaonywa wasisikie) upo katika aina ya mafundisho waliyonayo. Maana injili yao ndio hasa inayowapa uvuguvugu huo, maana ndio moto uliochini yao. Ndipo hapa nataka tutazame mafundisho yao na kwa namna gani mafundisho yao ni vuguvugu, yawatiayo uvuguvugu.


Mafundisho ya Laodikia/Walokole nimeyaweka katika nyanja hizi nne ili kuelewa makosa na kwa sababu gani hawajui dhambi bado na haki na hukumu.


  1. Mafundisho ya maziwa,

  2. Mafundisho ya Mali, (kinyume na Kristo, mathayo 6:24)

  3. Mafundisho ya kuzimu.

  4. Mafundisho ya wanikolai.


Hayo ya kwanza ni mafundisho ya awali ya Kristo, ya pili si ya Kristo na ya tatu vile vile si ya Kristo ijapokuwa wanapoyafundisha husema yametoka kwa Kristo. Hizi ni Roho nne ambazo kwa pamoja zinaunda uvuguvugu.


Tutaangalia kwa undani mafundisho haya katika somo linalofuata, tukianza na mafundisho ya Awali ya Kristo. Karibu!


Mawasiliano

+255 755 251 999

MANABII WA UONGO, Mahali wanakotoka

MANABII, NA AINA ZA MANABII

UJUZI WA MEMA NA MABAYA NI NINI NA KWA NINI NI DHAMBI

UADUI KATI YA UZAO WA MWANAMKE NA UZAO WA NYOKA

SABABU ILIYOPELEKEA ULIMWENGU WA KWANZA KUANGAMIZWA

        CHANGIA KUPITIA

 

          NMB:       22510119402

          MOBILE: 255755 251 999

​​

             MASHIBE ELIAS NTINGINYA

Mawasiliano:

 

+255 755 251 999

Mbezi, Dar-es salaam

  • Facebook
  • Instagram
  • X
  • TikTok
bottom of page