
Tumetangulia kuona sehemu ya kwanza uvuguvugu ni nini, na ya kwamba kanisa au wakristo katika kizazi hiki wasemao tunasubiri unyakuo mbele za Mungu ni vuguvugu na kwamba Yesu Kristo amesema atawatapika ikiwa hawatatubu.
Kama nilivyotangulia kusema Roho mtakatifu ndio moto na Neno la Mungu ni kama maji. Hivyo mtu vuguvugu ana kiwango kidogo cha joto au Roho mtakatifu. Roho mtakatifu ni mwalimu wa Neno la Mungu, naye hukua ndani ya mtu kwa maana ya ufahamu wa Mtu huongezeka. Kiwango cha kumjua Mungu ndio kiwango cha Roho mtakatifu ndani ya yule mtu. Lakini Bwana Mungu ameonya kanisa lililopo leo ni vuguvugu, naye amesema litubu, kama hawatubu atawataika watoke katika kinywa chake.
Kanisa la saba lililopo leo ndio wapentekoste, ambao leo tunatazama mafundisho yao ambayo kimsingi ndio roho ya kanisa waliyonayo ambao Bwana ameinena ni vuguvugu. Tuanze kuangalia aina ya kwanza ya mafundisho ya walokole.
Waebrania 5:10-14
10 kisha ametajwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.
11 Ambaye tuna maneno mengi ya kunena katika habari zake; na ni shida kuyaeleza kwa kuwa mmekuwa wavivu wa kusikia.
12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.
13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga..
14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya.
Hapa Paulo anashindana na kanisa la waebrania yaani wayahudi waliomwamini Kristo ambao siku nyingi zilikiwa zimepita wakiwa ndani ya neno la Kristo wala hawaongezeki katika kumjua Kristo. Nao walikuwa wamezoelea maziwa yaani mafundisho ya awali ya Kristo. Katika roho ni watoto wadogo, na kwa sababu hiyo hawaijui haki bado kwa kuwa hawana neno la haki ambalo anasema linatokana na chakula kigumu.
Neno la haki halitoki kwenye maziwa, maziwa yanamfanya mtu aamini na kuanza safari ya kumcha Mungu. Lakini mtu anakuwa kama maji yaliyowekwa jikoni, anapaswa kuendelea kuchemka kila uchao. Kutoka ubaridi kwenda uvuguvugu, kutoka uvuguvugu kwenda moto. Paulo aliliona kanisa lile kuwa limetoka kwenye ubaridi na kufikia uvuguvugu, kisha wakaridhika katika hali hiyo (kuendelea kutaka maziwa na si chakula kigumu).
Sawa na jinsi ambavyo kanisa hili (Laodikia) lililopo linavyoridhika na maziwa na mafundisho ya mali na kujiona ni matajiri kama Yesu Kristo asemavyo katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana 3:17.
14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 KWA KUWA WASEMA, MIMI NI TAJIRI, NIMEJITAJIRISHA, WALA SINA HAJA NA KITU; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
Ni tabia ile ile kama ya waebrania, hawa nao hawataki kitu kingine yaani chakula kigumu kinapokuja kwao wanakisukumia mbali, hawataki chakula kingine zaidi ya hicho walichonacho ambacho ni mafundisho ya awali ya Kristo au Maziwa.
MAFUNDISHO YA MAZIWA
Waebrania 6:1-2
1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu,
2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele.
Hapa ametaja mafundisho 6;
Kutubia kazi zisizokuwa na uhai ni mafundisho ya kuacha dhambi; mfano, kuacha uzinzi, ulevi, kutukana, kuseng'enya, kuiba, kusema uongo n.k.
Kuwa na imani kwa Mungu. Hili ni fundisho la pili katika mafundisho ya awali ya Kristo yaani maziwa. Kuwa na imani kwa Mungu ni mafundisho juu ya kumwamini Kristo, na Mungu aliyemtuma Kristo.
Mafundisho ya mabatizo; Haya ni mafundisho juu ya ubatizo sahihi ni upi? Kwa nini ubatizo, Kwa jina gani mtu anabidi abatizwe? Kipindi kile kulikuwa mkanganyiko kati ya ubatizo wa yohana na ule wa Yesu. wengine wakihoji aliyebatizwa na Yohana anapaswa tena kubatizwa akimwamini Yesu Kristo? Na majibu ya Paulo ni katika Matendo 19:1-6.
Kuwekea mikono (wagonjwa). Maana yake ni kuponya wagonjwa kwa kuwawekea mikono kwa jina la Yesu. Haya pia ni mafundisho ya mwanzo mwanzo kwa kila amwaminiye Kristo, ambayo ni maziwa.
Kufufuliwa wafu. Ni mafundisho juu ya ufufuo wa wafu waliokufa katika Kristo katika siku ya mwisho. Haya pia ni mafundisho ya awali ya Kristo yaani maziwa.
Hukumu ya milele. Haya ni mafundisho juu ya hukumu ya wafu waliokufa katika dhambi yaani nje ya Kristo. Haya nayo ni mafundisho ya awali ya Kristo, maziwa!
Haya yote ni mafundisho ya awali ya Kristo na ndio msingi ambapo kanisa lolote la Kristo linapaswa kujengwa, kumaanisha hata ukisoma nyaraka za mitume waliokuwa wakiweka msingi utaona zimejaa hayo tu yaani maziwa, na mtu aliyezoelea mafundisho haya ni mtoto mdogo asiyejua sana neno la haki.
Lakini ndio hayo hayo yanaleta uvuguvugu maana mtoto hakuzaliwa kunyonya maziwa milele bali atakula kulingana na umri. Kutoka maziwa atakunywa uji, kutoka uji atakula chakula kigumu kidogo hadi kigumu kabisa. Huyo anakuwa tayari anaelekea utu uzima kama wazazi wake.
Akiwa mtu mzima anakuwa anafanana na wazazi wake.
Ndipo kwa sababu hiyo kanisa linapaswa kufanana na Mungu na ili kufikia hatua hii lilipaswa kutoka ufunuo huu wa Mungu kwenda ufunuo mwingine ambao Bwana Mungu ameuleta kwa nyakati saba yaani Ufunuo kwa efeso, ufunuo kwa smirna, na Pergamo na Thiatira na Sardi na Filadelfia na Laodikia. Maana Bwana Mungu ameleta ufunuo kulingana na umri wa kanisa.
HATA HAYO MAZIWA HAYAFAI TENA!
Pamoja na kuwa mafundisho haya ya awali ya Kristo ni msingi ambayo kila kanisa lazima liwe nayo, bado nayo pia yamegoshiwa. Kwanza kabisa lazima ufahamu ya kuwa katika vizazi saba vya kanisa; Kizazi cha tatu ndipo yalianza kugoshiwa mafundisho ya awali ya Kristo.
Kipindi hiki mafundisho ya wanikolai ambayo nimeyaweka ya nne katika orodha ya mafundisho ya uvuvuvugu, yalianza katika kanisa. Yakaondoa yaliyo ya Mungu na kupanda yaliyo ya wanadamu. Kanisa likayapokea na kuwa mafundisho ya kanisa, mpaka Bwana alikasirika na kuliacha kanisa, naam, ndilo katoliki!
Bwana Mungu akasimama kinyume na kanisa hili kwa wajumbe wengi na yeye aliyeshinda katika kulitapika kanisa hili alikuwa MARTIN LUTHER., ndiye mjumbe wa kanisa la tano. Pamoja na kufaulu kwake bado hakufaulu kung’oa kila pando lililokuwa limepandwa na wanikolai, mafundisho ya wanikolai aliondoka nayo na yapo kwa walutheri na KKKT n.k hata leo, Kanisa la sita likaondoa baadhi lakini mengine likaendelea nayo na yapo mpaka leo.
Vivyo hivyo na kanisa la Saba, limeondoa baadhi lakini linayo mengi mpaka leo. Ndio maana hata katika mafundisho ya maziwa bado halijayajua kwa ukamilifi na bado lingali likihitaji hayo na si chakula kigumu.
Na ili kanisa litubu sawasawa na neno la Kristo, lazima liyajua hayo mafundisho yaliyosalia na kuyaacha au kuyaandoa. Lakini litayajuaje mafundisho ikiwa limeshafunga mlango? Litasikiaje ikiwa halitaki chakula kigumu? Yeye asimamae mlangoni akibisha anasema;
“Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”
Ufunuo wa Yohana 3:18 (Biblia Takatifu)
Dhahabu iliyo safishwa kwa moto ndio chakula kigumu asichokitaka laodikia. Ni ufunuo wa Mungu ambao ikiwa Laodikia ataupokea atafikilia utimilifu.
Naam, ISIKILIZE SAUTI YA BWANA wewe uliye na masikio ya kusikia, kwa kuwa ni wewe uambiwaye ya kuwa ni vuguvugu.
Somo linalofuata tutajifunza mafundisho ya Mali.
Mawasiliano
+255755 251 999