top of page

Katika vizazi saba vya kanisa tulivyovitazama, Bwana Mungu katika kanisa la sita alionya kuwa inakuja saa mbaya katika ulimwengu wote; kuujaribu ulimwengu na kuuharibu. Malaika wa sita, John Wesley, alipewa unabii wa kuja hii saa, itakayoujiria ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.


Ufunuo wa Yohana 3


⁷ Na kwa malaika wa kanisa lililoko Filadelfia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye.
⁸ Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu.
⁹ Tazama, nakupa walio wa sinagogi la Shetani, wasemao kwamba ni Wayahudi, nao sio, bali wasema uongo. Tazama, nitawafanya waje kusujudu mbele ya miguu yako, na kujua ya kuwa nimekupenda.
¹⁰ Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika SAA YA KUHARIBIWA iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.

Kanisa la sita kwa ushuhuda wa John Wesley lilipitIa katika njia ya utakatifu na Bwana akalipenda kwa sababu ya bidii yao ya kuishi ndani ya neno lake. Kisha Bwana kwa kuwapenda akasema atawaepusha na saa mbaya ambayo ilikuwa mbele kidogo kuuijilia ulimwengu wote. Hapa, Bwana Mungu alisema na kanisa linalokwenda kwa ufunuo wake katika miaka ya 1750 BK hadi 1906 BK.


Baada ya kanisa la sita linafuata kanisa la saba, Laodikia! Ndio kizazi hiki, ni kanisa la mwisho. Na kwa sababu hiyo ni wakati wa mavuno, yaani kutwaliwa kwa ngano (mbengu njema) na kuwekwa katika ghala la Bwana. Kisha magugu kuchomwa moto. Maana si wote walio katika kanisa ni wa Mungu.


Sasa wakati huu ndio saa aliyoinena Bwana kwamba inakuja, kwa ajili ya kulijaribu kanisa na wote wakaao juu ya nchi na kuwaharibu wote WATENDAO MAOVU. Hapa kuna mambo mawili; KUJARIBIWA NA KUHARIBIWA.


Maneno haya yanaonesha hukumu ya Mungu juu ya ulimwengu, lakini kwanza hukumu itaanza katika kanisa lake, ndio maana kanisa la saba analiambia nasimama mlangoni (ufunuo 3:20). Anasimama kuhukumu madhehebu yote yaani kila injili inenwayo kuwa ni injili ya Yesu Kristo ataihukumu kwa kuwa hawaneni sawasawa na Roho wa Mungu. Zipo injili nyingi na idadi yake ni hayo madhehebu uyaonayo, nazo kila moja

imekwisha kujaribiwa.


Kuharibiwa kunakuja baada ya kujaribiwa, tafsiri yake ni kwamba anayeharibiwa ni yule alijaribiwa kisha akashindwa lile jaribu. Na jaribu hili ni la moja kwa moja juu ya neno la Mungu, kwamba ni jaribu linalokuja juu ya watu wanaolijua neno la Mungu ili kuwajaribu ikiwa wanampenda Mungu au la. Na ikiwa hawataenda kinyume na neno lake hawataharibiwa lakini ikiwa watashika kinyume, wataharibiwa.


Mfano mdogo ni ule wa kitabu cha Hesabu sura ya 22,23,24,na 25. Balaki mfalme wa Moabu alimwita Balaam amlaanie wana wa Israel apate kuwapiga katika vita, lakini Balaam kila alipokwenda mbele za Mungu ili apate kuwalaani, alipewa kuwabariki. Ndipo safari ya mwisho akabadili mbinu, akamfundisha Balaki mfalme wa moabu kuwashawishi wana wa Israel washike kinyume na sheria za Mungu wao. Wazini na kula katika vyakula vilivyotolewa sadaka.


Ushauri wake ulifanikisha kuharibiwa kwa wana wa Israel elfu ishirini na nne (24,000). Hawa 24,000, Kabla ya Sheria ya Mungu iliyokuja kwa njia ya Musa, watu hawa wasingeuawa. Lakini kwa sababu hawakumpenda Mungu; walilijua neno la Bwana na kulitii kwa nje tu lakini mioyo yao ilikuwa mbali naye. Ndipo Bwana Mungu alimruhusu Balaam afuatane na Wajumbe wa Balaki ili KUWAJARIBU ISRAEL ikiwa wanampenda.


Ndipo ikadhihirika si wote walimcha kwa kicho, wala kumpenda, wakaliacha neno lake Bwana Mungu upesi na kumshikia kinyume. Na kama wote wangelitenda dhambi ile, asingelibaki hata mtu mmoja siku ile.


Ndipo katika kipindi hiki leo, tunaona kuwa Bwana Mungu analeta majaribu kote ulimwenguni yaani kwa wakristo wote duniani, maana ndio waliopewa neno la Mungu yaani nuru wapate kuutia ulimwengu nuru. Lakini wakristo hawa tunawaona hivi leo ukiwalinganisha na neno la Mungu unapata watu peke yao na neno la Mungu peke yake, ni kama mafuta katika maji.


Tena Bwana Mungu ameruhusu walimu,wachungaji, mapadre, manabii, mitume, makardinali, waimbaji, na wahubiri wengi walio kama Balaam ili waseme uongo, watabiri uongo, wafundishe uongo, wabariki uongo ili kwamba aone watu jamii ikiwa wanampenda, yaani kuwachukia walimu hawa au la!


Bwana Mungu ameleta mara dufu ya injili za uongo na ufunuo wa uongo katika kizazi hili kuliko kizazi chochote hapo kabla, lakini watu jamii hawaugui kuona huu ubatili. Badala yake wanafurahi kuwa furaha yao imetimizwa kwa kupewa walimu hawa. Tena kwamba wanamshukuru Mungu makanisani kwa sababu anajibu maombi yao kupitia walimu hawa.


Yeye aliyesema hamwezi kutumikia mali na Mungu wanamshukuru kwa kuwapa walimu wazuri wa kuwatoa katika umasikini na kuwapa mali na kuwafundisha jinsi ya kupata mali, naam, LAODIKIA ametajirika kwa walimu hawa! Nao wamechagua kumdharau MUNGU na kuchagua mali. Lakini hawajui kuwa kitambo kidogo ghadhabu ya Bwana itafurika juu yao na walimu walimu wao na wachungaji wao na waimbaji wao na manabii na mitume wao, maana wamemchukia Yeye.


Ndipo unaona; Yeye aliyesema usimwite baba duniani, wala kiongozi wala mwalimu lakini kila mwalimu leo ni baba. Tena wengine hawakuishia kumwita kiongozi wao baba tu, wakaenda mbali kumwita baba mtakatifu.


Yeye aliyesema ujihadhari na manabii wa uongo, kanisa wanamshukuru kwa kuwapa walimu hao.


Yeye aliyesema ISIKILIZENI SAUTI YANGU! wamempa kisogo na kuwasikiliza walimu wa na wachungaji wao wa uongo wawaambiao “sisi ndio ile sauti yake; tusikilizeni sisi maana Mungu hatatenda neno isipokuwa kwa njia ya sisi”


Naam, wasikilizeni wao, maana hii ndio saa ile hasa mpate kujulikana mbele za Mungu kuwa mlikuwa wanafiki tangu kuzaliwa kwenu mara ya pili. Kisha itakuwa baada ya jaribu hili Mungu atawatenga walio wake na kuwavika ghadhabu iwe nguo ya kujifunika watu hawa wasemao ni wakristo nao sio.


Kama ilivyotafsiri ya LAODIKIA, kuwa ni uongozi/utawala wa watu, ndipo kanisa limechukua MAFUNDISHO YA WANADAMU kuwa ndio kicho/hofu yao mbele za Mungu. Katika vinywa vya watu makanisani, Mungu yupo karibu nao na katika mioyo yao na nia zao Mungu yuko mbali kama Kristo asemavyo;


8 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.
9 Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.

Mathayo 15:8-9


Mafundisho ya madhehebu ni maagizo ya wanadamu, maagizo ya kina balaam, maagizo ya walimu, wachungaji, mitume, manabii waliofanywa na wanadamu kuwa walimu, wachungaji, mitume, manabii n.k, ili wawe badala ya Mungu.


Kanisa lipo katika kujaribiwa nalo limempa shetani nguvu ya kutawala kwa jina la Yesu. Ili kila mwalimu au kanisa liende lionavyo sawa lenyewe. Hakuna Mungu juu ya watu hawa, Yesu Kristo yupo nje ya kanisa la kizazi hiki kwa sababu wamemkataa. Ndipo Yesu anasimama mlangoni, yaani nje ya kanisa akibisha mlango ili kuingia leo;


Ufunuo wa Yohana 3


¹⁴ Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
¹⁵ Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
¹⁶ Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
¹⁷ Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
¹⁸ Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
¹⁹ Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
²⁰ Tazama, NASIMAMA MLANGONI, NABISHA; MTU AKIISIKIA SAUTI YANGU, NA KUUFUNGU MLANGO, NITAINGIA KWAKE, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

Tazama hasa msitari wa 20, kwamba wamefunga milango (masikio yao) wasije wakasikia neno lolote zaidi ya kile dhehebu lao lisemacho. Kama ni dhehebu la kikatoliki wanataka kusikia kile tu dhehebu la katoliki linataka. Anglikana, lutheran, Wapentekoste, wasabato n.k vivyo hivyo. Yeye anagonga milango ya madhehebu, kwa maana ya kuyahubiria kutubu, na huyo aisikiae Sauti yake na kutii ndiye ambaye Yesu Kristo ataingia kwake.


Ni kuijiriwa kwa kizazi hiki kama ambavyo Kristo alivyomwijilia Israeli kwa upanga mkali. Akasimama kwao kama Adui ijapokuwa ni watu wa nyumba yake. Na hapa napo anasema NITAKUTAPIKA UTOKE KATIKA KINYWA CHANGU (mstari wa 16).


Yeye aisikiaye sauti yake atakaa ndani yake na yeye aikataaye sauti yake kwa ajili ya dhehebu lake atakuwa kama mafarisayo na masadukayo; waliotapikwa na Mungu. Nayo kazi ikiisha kutendeka yaani kuwajaribu wote waketio juu ya nchi, ndipo kazi ya kuwatenga makundi mawili itakuwa imatimilika, mbuzi huku na kondoo huku. Na kama alivyowatendea wale 24,0000 ndivyo mwisho wa madhehebu waliojaribiwa wakaanguka katika uovu wasikubali kutubu na KUITII SAUTI YAKE.


ISIKILIZIENI SAUTI YA BWANA!



Mawasiliano;

+255 755 251 999

MANABII WA UONGO, Mahali wanakotoka

MANABII, NA AINA ZA MANABII

UJUZI WA MEMA NA MABAYA NI NINI NA KWA NINI NI DHAMBI

UADUI KATI YA UZAO WA MWANAMKE NA UZAO WA NYOKA

SABABU ILIYOPELEKEA ULIMWENGU WA KWANZA KUANGAMIZWA

        CHANGIA KUPITIA

 

          NMB:       22510119402

          MOBILE: 255755 251 999

​​

             MASHIBE ELIAS NTINGINYA

Mawasiliano:

 

+255 755 251 999

Mbezi, Dar-es salaam

  • Facebook
  • Instagram
  • X
  • TikTok
bottom of page