top of page

Kanisa la Laodikia ni nyakati kuanzia 1906 BK hata leo. Katika makanisa sita tuliyotazama, tumeona habari ambazo zinafanya ujue kanisa lilikopitia mpaka hapa tulipo leo. Jinsi kanisa linavyosafishwa kutoka hatua moja kwenda nyingine, na jinsi madhehebu yanavyozaliwa. 


Tumeona malaika sita waliotumwa na Mungu kwa kila kizazi. Hakuna malaika hata mmoja ambaye alienda chuo cha theolojia kisha akawa mjumbe wa Mungu kwa ujumbe wa walimu wa theolojia (ufunuo wa damu na nyama). Bali wote walikuwa na ufunuo wa Mungu.


Mambo yote yaliyoandikwa katika kanisa hili yameandikwa kwa malaika wa kanisa lililoko katika nyakati hizi za kanisa, yaani kizazi hiki tulichopo sasa. Tutazame habari za Laodikia katika ufunuo 3:14-22.


14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina,  Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.


Kama alivyoanza kusema, na kwa malaika wa kanisa liliko Laodikia, andika: maana yake ni habari ambazo zinaandikwa kwenda kwa malaika wa Laodikia ambaye ni William Seymour. Huyu anatokea Marekani, alikuja na uamsho unaojulikana kama uamsho wa mtaa wa Azusa (Azusa Street Revival). William Seymour alianza safari ya wokovu katika kanisa la Baptist, kisha Methodist, na baadae ‘Evening Light Saints’ na ‘Apostolic Faith Mission’, kisha akawa mwanzilishi wa makanisa ya kipentekoste au walokole.



YEYE ALIYE AMINA


Sifa ya Yeye anenaye imekuwa tofauti na makanisa mengine. Tofauti na kanisa la sita tulilotoka kutazama, ambalo alijitambulisha kama mtakatifu, hapa Yesu Kristo anajitambulisha kwa kizazi hiki cha saba kuwa ni Amina! Maana yake ni shahidi mwaminifu na wa kweli. Ni mwaminifu katika neno la Mungu, na wa kweli, yaani husema kweli mbele za Mungu na kuishi ile kweli kiasi cha Yeye mwenyewe kuwa ile KWELI. Maana yake ndivyo inavyopasa kanisa hili kuwa, ni kanisa ambalo anatazamia uaminifu katika neno lake na kunena au kufundisha yaliyo kweli. 


Sasa tuone jinsi alikinena kizazi hiki ikiwa kinakaa katika uaminifu na kweli kama John Wesley na wa-Methodist walivyokaa kwenye utakatifu sawasawa na jinsi Kristo alivyojitambulisha kwao.


Katika kizazi cha sita, injili ilikuwa imejikita katika utakatifu, sawasawa na ufunuo wa John Wesley. Wesley alifundisha hatua mbili za wokovu:


  1. Kuzaliwa mara ya pili (kazi ya kwanza ya neema)

  2. Utakaso kamili (kazi ya pili ya neema).


Katika utakaso kamili, Wesley alisema ndio hatua ya kupokea Roho Mtakatifu. Lakini baadaye, mjumbe wa kanisa hili la saba, William Seymour, akaja na ufunuo kuwa kupokea Roho Mtakatifu ni hatua ya tatu baada ya utakaso kamili. Hivyo, kulingana na William Seymour, inakuwa:


  1. Kuzaliwa mara ya pili (kazi ya kwanza ya neema)

  2. Utakaso kamili (kazi ya pili ya neema)

  3. Kupokea Roho Mtakatifu (utimilifu).


Hapa, Seymour alipomwomba Mungu kwa watu ambao kimsingi wametokea katika fundisho la utakaso kamili kupokea Roho Mtakatifu na karama za Rohoni, ikawa hivyo. Karama zikarudi; kunena kwa lugha, kuwekea mikono wagonjwa, n.k. Lakini pamoja na hayo, Bwana amewanena waliopokea karama hizi kama vuguvugu. Haikuonekana mbele za Bwana kuwa wamefikia utimilifu kama alivyoona William Seymour. 


Kurudi kwa karama ikawa jambo geni katikati ya waamini wengi kwa sababu zilikuwa zimekufa katika kanisa. Zilibaki hadithi tu, na kurudi kwake ikawa ishara kama ile ya Pentecoste. Tangu wakati ule, yaani mwaka 1906 BK, wapentekoste tunaowajua leo wakazaliwa. Hivyo wapentekoste ndio kanisa la saba, watu waliozaliwa baada utakaso wa tano. Kumbuka utakaso wa kwanza ulizaa kanisa la pili (smirna), utakaso wa pili ukazaa kanisa la pergamo na kuendelea. hivyo kanisa la saba linatokea baada ya utakaso wa sita.  Hivyo umesalia UTAKASO mmoja ambao ndio utakaozaa BIBI HARUSI WA KRITO.


Uamsho wa William Seymour uamsho uliochukua muda mfupi kufika ulimwengu wote kuliko nyakati zote za wajumbe hawa saba. Ujumbe wake ukachagiza ibada na mafundisho kujikita katika karama, jambo ambalo ni zuri, lakini ukazaa watu wenye kutazamia KUPOKEA kutoka kwa Mungu badala ya utakatifu. UTAKATIFU ukaendelea kiminywa hadi kudharauliwa. Likaibuka kundi kubwa la walimu na wachungaji wanaohubiri kupokea peke pake na kudharau UTAKATIFU au mwenendo wa mtu mbele za Mungu. 


Kundi hili ndio linalopendwa na watu, halikemei dhambi bali lenyewe ni kuwatumainisha watu kutazamia KUPOKEA. Kundi hili haliwafanyi watu kuwa WATAKATIFU kama Mungu alivyo mtakatifu wala nia ya Mungu haimo ndani yao bali kuwafanya watu kuwa na nia ya ulimwengu huu.  Lakini si tu kundi hili bali ndio roho iliyoanza na William Seymour na iko kila dhehebu la wapentekoste liwalo lote kote ulimwenguni. Na baadae watu wakarudia desturi zile zile zilizomfanya israel atapikwe, zile zilizomfanya katoliki atapikwe. Na kwa sababu hizo hizo Bwana Mungu akanena hukumu kwa Wapentekoste pia;


Ufunuo wa Yohana 3;


15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi  au moto.  


16  Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa  changu.



Yesu Kristo anamwambia William Seymour na watoto wake (wapentekoste) kuwa matendo yako si baridi wala moto, bali ni vuguvugu. Na kwa sababu ya uvuguvugu, Yesu Kristo anasema nitakutapika, yaani kukukataa usiwe wangu (kama alivyomtapika Israeli). Huu ndio unabii wa wapentekoste wote duniani ambao ndio fedha inayopaswa kusafishwa mara ya mwisho ili kupata iliyo safi. Bwana anasema kwamba ni vuguvugu!


Sasa, unaweza kujiuliza kwa nini William Seymour na wapentekoste ni vuguvugu wakati Seymour alichukua kilicho cha John Wesley aliyependwa na Bwana, akaja nacho hata akaleta matokeo ya karama ambazo Wesley hakuwa nazo?


Jibu ni kwamba, John Wesley alikuwa sahihi kabisa. Hata yeye mwenyewe angeomba karama zingedhihirika. Nyongeza ya William Seymour ya kusema kwamba baada ya utakaso kamili ndipo mtu anapokea Roho Mtakatifu haikuwa tafsiri sahihi. Ijapokuwa alikuwa sahihi kuzitaka karama, haikuwa sahihi kwa sababu lengo la injili au neno la Mungu kwa mwanadamu ni utakatifu (Waebrania 12:14) na si karama. 


Hivyo, hata kama karama zingemwagwa kiasi cha kuhamisha milima, bado isingeonekana ni jambo la utukufu mbele za Mungu ikiwa wazitendao hawajafikilia utakatifu.


Seymour na wapentekoste wamebatilisha injili ya John Wesley; tafsiri ya neema katika mwenendo wa injili ya John Wesley ilikuwa kwamba Neema ni msaada wa Mungu kwa mtu aliye na bidii kumtafta, lakini kwa wapentekoste imekuwa kinyume, neema imekuwa sio msaada tena bali imekuwa kazi ya lazima atakayoifanya Mungu kwa pasipo bidii yao. na kwa sababu hiyo jukumu la wao kuwa watakatifu wanamwachia Mungu. Ijapokwa William Seymour hakuanza hivi lakini mwendelezo wa injili yake ulikuwa unaelekea huko. Ndio maana hatima ya watoto wake yaani wapentekoste inakuwa kutubu ama kutapikwa.


INJILI YA WILLIAM SEYMOUR ILIZIBA MASIKIO YA KANISA (WAPENTEKOSTE)


Kulingana na William Seymour, mtu anapitia hatua kufika kamilifu; 

kuzaliwa upya, utakaswa kamili, na mwisho ni ubatizo wa Roho mtakatifu ambapo inaanza na kunena kwa lugha. Na tumetoka kuona kwamba John Wesley aliishia kwenye utakaso kamili. Tafsiri ya Seymour inawaweka wapentekoste kuwa watu wakamilifu yaani watakatifu, kwa kuwa wamepokea roho mtakatifu yaani kunena kwa lugha.  Kwa sababu wamezaliwa upya, wametakaswa na wamebatizwa kwa Roho mtakatifu. 


Hii ikawa ndio dira ya kufikia ukamilifu kwa wapentekoste, na ikawa sababu ya kuridhika na kusubiri unyakuo.  Kwa kuwa ni wakamilifu hawatazamii kusikia neno tubu wala mtu akisema tubuni, hawatazamii kufundishwa bali wao kufundisha. Hata haya maneno ya Kristo yanayotaja kuwa ni vuguvugu hawakubaliani nayo kuwa ni wao ndio wanaambiwa. Kwa sababu wanajiona kuwa ni watakatifu nao kwamba ndio wanajua Neno la Mungu na Neno la Mungu litatoka kwao, ndivyo Bwana alivyowaona pia kabla na kuzinena habari hizo;


17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa  wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.

Ufunuo 3:17


Haya ni maneno ya Kristo kwa William Seymour na wapentekoste, ni mabishano, Yeye anahubiri juu ya uvuguvugu wao na umaskini na uchi na upofu wao ili wapate kutubu, lakini kwa kiburi wanasema sisi ni matajiri, tumejitajirisha wala hawahitaji injili iwao yote isipokuwa hiyo waliyonayo, inayowanena kuwa ni wakamilifu baada kubatizwa kwa Roho mtakatifu. 


Hawa nao kama ilivyo kwa kila kanisa linapofanya dhambi, huchukia kuonywa, hukaidi sauti ya Mungu lakini midomoni mwao Mungu yupo pamoja nao. Bwana Mungu amewaona kuwa ni vuguvugu, na masikini na  vipofu na uchi, wao wanajiona kuwa ni matajiri. 


NI LINI WALISEMA KUWA WAO NI MATAJIRI?


Baada ya uamsho wa William Seymour, ulikuja uamsho wa William Branham, ambaye alihubiri toba kwa walio katika dhambi na akahubiri toba kwa wapentekoste kwa sababu ni vuguvugu, lakini wapentekoste walimpuuza, hawakuwa na haja na kitu kwa kuwa ni matajiri., nao wamekuwa mfano wa Vashti. Sauti ya ingaliko hata wakati kwa wapentekoste na kwa Wa-branhamist pia, maana nao pia wameshiriki katika dhambi ya walokole tayari. 


WAKATI WA KUFUNULIWA KWAKE


Sasa huu ni wakati wa kufunuliwa kwa uchi wake na upofu wake, na umasikini wake ili kila mtu ajue na neno la Mungu litimie. Kama Bwana alivyonena kuhusu kizazi hiki, yaani wapentekoste (pamoja na wa branhamist), kuwa nitakutapika utoke katika kinywa changu; ujue na kufahamu kuwa si yeye Bwana awatapikaye bali ninyi mmekwisha kumtapika yeye kwa mafundisho na maagizo ya wanadamu kama alivyotenda Israeli na katoliki. Naye Bwana kuikamilisha kazi mliyoianzisha yaani kutapikwa.


Ikumbukeni shilo kuwa yalikuwa makazi ya Bwana, ikumbukeni Yerusalem mji wa Daudi ilimokuwa nyumba ya Bwana; ikumbukeni Katoliki huko ambako Bwana mahali ambako Bwana aliketisha miguu yake. Naam, mwenye kutambua makosa yao ayatambue na makosa ya kizazi hiki ili asije kuwa kama moja ya miji hiyo.


Tafsiri ya Laodikia ni uongozi wa watu, yaani watu ndio wanaoongoza kanisa na sio Yesu. Wanamtaja Yesu kuwa ni kiongozi wao lakini wamemkana kila mahali. Wakamuhuzunisha na kumzimisha Roho wake Mtakatifu, matendo yake yakaondoka, yaani akaondoka, akawaacha wajiongoze.


Ndipo kila mtu na kila kanisa hutenda na kufundisha kama waonavyo sawa machoni pao. Mafundisho yao yanatokana na ufunuo wa damu na nyama, lakini kanisa la Kristo hujengwa juu ya ufunuo utokao kwa Baba ambaye amdhehebu yamemwacha wala hayataki kusikiliza neno lolote kutoka kwake. ndio maana Bwana anashauri akisema:


18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi  meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako,  upate kuona. 


19  Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.


Mstari wa 19 anamalizia akisema 'basi uwe na bidii, ukatubu', maana kutub peke kunakuja ikiwa mtu atatambua makosa. Na makosa ya kanisa hili la saba yamejikita kwenye maarifa. Wenye bidii katika maarifa ndio watakaoweza kutambua makosa na kutubu, ndio watakaoweza kuupokea ushauri wa Bwana katika mstari wa 18, watanunua dhahabu iliyosafishwa kwa moto yaani ufunuo wa Mungu, nao ufuhuo huo utawapa kuona uchi wao na upofu wao. 


ISIKILIZENI SAUTI YANGU!


Yeye Bwana anasema;


20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango,  nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.


Hii ni sauti ya Bwana Yesu Duniani, Ufunuo wa neno la Mungu kwa ajili ya Bibi harusi, ndiyo dhahabu iliyosafishwa kwa moto ambayo alishauri katika mstari wa 18 kuwa ununue kwake na kwamba kila mtu asiyeisikiliza atatapikwa. Anasimama nje ya mlango wa kila dhehebu akigonga akiwa na dhahabu hiyo iliyosafishwa kwa moto.


Ufunuo huu ni mahubiri kama ya Nuhu wakati kizazi kile kinaitwa kitubu kisije kikaangamia. Nuhu alisimama milangoni mwao lakini kila mtu alijiona ni mtakatifu, hana haja na kitu kingine. Ndivyo Kristo alivyozinena nyakati hizi akisema;


26 Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu.  


27  Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika  safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote.

Luka 17:26-27

Kula na kunywa sio kosa, bali hapa inamanisha wanafanya yaliyo mapenzi ya nafsi zao kwa sababu wanazipenda. Wamejikita kumsumbua Mungu juu ya tule nini?, tunywe nini? tuvae nini? tutapata lini gari, kazi nzuri, mme, mke, pesa, umaarufu, ukuu, uchungaji, uaskofu, ualimu, n.k. Yote haya ni matamanio ya mwanadamu, na haya ndio wanayoyasumbukia usiku na mchana. Injili yao imebeba mambo hayo; tule nini? tunywe nini? Injili yao inahubiri kuipenda nafsi yako.


Yeye aliye mwaminifu na wa kweli anasema nasimama mlangoni, lakini ndani ya kanisa wanasema Yesu Kristo anakaribia kuja kutunyakua. Ni lugha mbili tofauti kabisa. Ndio maana anasema Yeye atakayeisikia sauti yake ataingia kwake. Maana yake atalipokea dhehebu lile liwe lake. Ni injili inayowahubiri walioitwa tu, yaani wakristo hasa wapentekoste ambao ndio wanaoonywa hapa kuwa ni uzao wake lakini wamekengeuka. Hawaendi mbele, bali wanarudi nyuma. 


YEYE ASHINDAYE


21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi  nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.  


Yeye ashindaye ataketi pamoja naye katika kiti cha enzi cha Baba mbinguni. Sasa watakaoshinda ni hao watakaoisikia sauti yake, 


22  Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.


Kama asemavyo, ukatubu, naam, ukatubu!


Mawasiliano;

+255755251999

bottom of page