
Tumejifunza juu ya kanisa la Kristo katika vipindi au nyakati saba na jinsi linavyosafishwa. Kanisa la Kristo linatembea kutoka ufunuo huu wa Kristo kwenda ufunuo huu. Na ufunuo wa Mungu umekuja kwa njia ya wajumbe saba. Katika hizo, madhehebu mengi yamezaliwa sawa na uchafu unavyozalishwa na mfua fedha.
Kanisa la Mungu/Kristo katika wakati huu ni hili!
Ufunuo wa Yohana 3
²⁰ Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
Hii ni sauti ya Bwana, Yeye ambaye mnamwitia jina lake leo na kumpenda. Haya maneno anayanena kwa kanisa la saba ambalo ni wakristo wa kipentekoste yaani walokole; hao ndio jamii ya mwisho katika wajumbe saba wa kitabu cha ufunuo. Anakiambia kizazi hiki nasimama nje ya madhehebu yenu, nahubiri kwenu juu ya uvuguvugu wenu. Mtu akiisikia/akiitii Sauti yangu nitaingia kwake.
Wana heri walio masikini wa Roho katika nyakati hii, naam, hao wenye kuhitaji wala hawasemi sisi ni matajiri, hatuna haja na kitu kingine; maana Yeye Yesu aliye nje na madhehebu haya ameshuhudia akisema juu ya kizazi hiki kuwa;
Ufunuo wa Yohana 3
¹⁵ Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
¹⁶ Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
¹⁷ Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
Madhehebu haya yaliyopo, hayana haja na kitu kingine. Hawasemi hivi wao kwa wao bali waisikiapo Sauti yake asimamae nje ya madhehebu yao ndipo humjibu hatuna haja na kitu kingine. Maneno HATUNA HAJA NA KITU KINGINE yanayotoka kwenye madhehebu haya ndio mlango uliofungwa.
Ni watu ambao wana hekima machoni pao wenyewe, ndio maana wanajinena kuwa ni matajiri lakini Bwana Mungu anasema ni masikini na vipofu na uchi.
Lakini haya yote watayajuaje ikiwa wamefunga mlango wa kusikia kitu kingine zaidi ya kile walichonacho? Watajuaje kuwa ni vuguvugu na masikini na vipofu, tena wamejaa mashaka juu ya ufalme wa mbinguni? Ndipo nasema tena ana heri mtu yule aliye masikini katika roho leo maana ufalme wa Mungu utakuwa wake.
Hivyo kanisa la Mungu/Kristo katika kizazi hiki ni hao WAISIKIAO SAUTI YAKE NA KUFUNGUA MLANGO. Hao ndio kanisa na watumishi wa Mungu. Hawa ndio ile ngano iliyovunwa kutoka katika shamba la Bwana ambamo magugu yalimea na kukua pamoja na hizo ngano. Lakini ni ngano ndio itakayoisikia na kuitii Sauti yake.
ADHABU YA MUNGU NI JUU YA MADHEHEBU.
“12 Kisha itakuwa wakati ule, nitauchunguza Yerusalemu kwa taa; nami nitawaadhibu watu walioganda juu ya sira zao; wasemao katika mioyo yao, Bwana hatatenda mema, wala hatatenda mabaya.”
Sefania 1:12.
Nabii sefania, alitoa unabii huu ambao ulishatimia mara ya kwanza na uko njiani kutimia tena. Katika Yerusalemu kulikuwa na hekalu la Mungu, huko ndiko kulikuwako na watu wenye kiburi rohoni, wenye hekima machoni pao wenyewe wala hawana Mungu, ambao walikwenda kwa theolojia zao (mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu).
Sefania anasema kwa ufunuo wa Mungu kuwa atauchunguza Yesurusalem kwa taa (Neno lake yaani Kristo), kisha ataawadhibu watu waliganda juu ya sira zao (Madhehebu yao). Sira ni ule uchafu unaobaki baada ya utengenezaji wa divai au pombe nyingine. Kwa kifupi sira ni makapi. Na katika kanisa sira ni madhehebu, ambamo Bwana alijitwalia kanisa lake lililo tayari kuisikiliza SAUTI YAKE.
Watu hawa walioganda juu ya sira zao yaani madhehebu yao, moyoni mwao husema Mungu ni wa wote, Mungu anapenda watu wote, Mungu habagui, Mungu ni mwenye upendo, ametuokoa, hatatuacha, hawezi kutuadhibu. Hawa ndio wana wa Israel walioingia na kutoka katika hekalu lake. Lakini hawakuwasikiliza manabii wa Mungu, hawakuisikiliza sauti ya Mungu hata wakati wa Yesu Kristo. ambaye alisimama nje ya madhehebu yao akiwaita watubu. Nao walikuwa na sira za kifarisayo au kisadukayo au kizelote n.k. wakajiona ni matajiri.
Watu hawa hatuna mda wa kueleza yaliyowapata baada ya mji wa Yerusalemu kuchunguzwa kwa taa yaani Yesu Kristo. Lakini turudi kutazama yale Yerusalem ya sasa itakayopitia.
Kama fedha inavyosafishwa ndivyo na kanisa. Uchafu unaotoka wakati kanisa linasafishwa huitwa dhehebu, yaani watu wanaoenenda kwa mafundisho yaliyokataliwa na Mungu, hekima za kibinadamu.
Hivyo hakuna dhehebu lolote lillilo au litakalokuwa sahihi au kuwa kanisa la Mungu/Yesu Kristo isipokuwa wale WAISIKIAO SAUTI YAKE NA KUITII wakati huu.
Kila aitwae mkristo leo, yupo kwenye sira fulani, na sira za leo ni nyingi mara dufu kuliko wakati wowote, yaani hayo madhehebu. Na kila mmoja anaona yupo sawa, licha ya tofauti kubwa zilizopo kati ya madhehebu, kila mmoja anajaribu kushikiria historia, kwamba makapi haya yalikuwa mzabibu, mwingine, makapi haya yalikuwa fedha, makapa haya yalikuwa ngano, makapi haya yalikuwa mahindi.
Ni kweli makapi hayo yalikuwa hivyo wasemavyo; lakini ni nani akiisha kuitwaa divai kutoka katika sira aendelea kuhifadhi sira/makapi kwa ajili ya baadae? Bali hutupwa jalalani. Lakini Bwana angali amesaza watu wake katika sira hizi, kama ilivyokuwa wakati wa Kristo.
Ndipo asemapo nasimama mlangoni, mtu akiisikia sauti yangu na kuufungua mlango nitaingia kwake. Maana yake ni wakati wa kutwaa divai yake na kuitupa sira mbali kwenye shimo la takataka; huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.
Mwenye masikio na asikie!
Mawasiliano;
+255755 251 999