top of page

Unyakuo ni tukio linalotafsiriwa kuwa ndio kuja kwa Yesu Kristo mara ya pili. Kuna mafundisho ya aina nyingi juu ya kurudi kwa Yesu Kristo mara ya pili katika madhehebu ya ki-Kristo, lakini lililo na nguvu ni moja, ambalo ndio unyakuo.


Unyakuo imetafsiriwa kuwa ni tukio la siri la kutwaliwa kwa watu kama ilivyoandikwa katika Luka 17:34-36. Lakini pia wapo wengine walio na tafsiri tofauti kidogo na hii ya kusema ni tukio la siri kama dhehebu la wasabato wa Seventh day adventist (SDA). 


Hawa hutafsiri kuwa ni tukio la wazi la kutwaliwa watu (ambao ni waadventist) kwenda mbinguni kwa miaka 1000. Hutumia kitabu cha ufunuo 1:7 kwamba kila jicho litamwona. 


Kuna madhehebu kama katoliki wasioamini juu ya unyakuo kulingana na theolojia yao, ingawa waumini wake wengi huamini unyakuo kama wanavyosikia ukihubiriwa na walokole. Kuna madhehebu yanayotafsiri huo unyakuo kuwa ni tukio la kumlaki Bwana Yesu mawinguni tu kisha wanarudi naye kuanza utawala wa miaka 1000 (ufunuo 20).


Zaidi ya wote fundisho la unyakuo, kuwa wa siri na ambao utatokea kabla ya dhiki kuu ndio fundisho jipya au ufunuo mpya, na wenye umaarufu kuliko hayo mafundisho mengine ambayo mengine yamekuwepo tangu karne ya kwanza. Hivyo Unyakuo wa siri ndio fundisho kuu kwa wapentekoste na wabranhamist ambao pia ni wapentekoste pamoja na waamini wa Kacou.


Tumetoka kuangalia makanisa saba ya ufunuo 2 hadi 3 na ujumbe wa Kristo kwa kila kanisa. Kama hujapitia masomo hayo tafadhali usiendelee kusoma hili somo, badala yake rudi ukasome ili usije ukaondoka na majibu yako kutokana mhemko wa kutetea dhehebu lako. Fungua website hii www.injiliyayesujioni.org


Tuliona jinsi ujumbe wa kanisa la saba ulivyo, kanisa ambalo limeambiwa litubu na kama halitubu litatapikwa na Bwana Yesu. Kisha Kristo anaonekana yupo nje ya kanisa akibisha mlango wa kanisa ambao umefungwa. Tuisome habari katika kitabu cha ufunuo 3:14-20;


14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. 
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. 
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. 
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. 
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. 
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. 

Bwana Yesu anasema nasimama mlangoni, mlango wa kanisa, mlango wa madhehebu maana kama alivyoanza habari hii katika mstari wa 14 kuliandikia kanisa, ndivyo anavyosimama katika mlango wa Laodikia, ambao ndio kizazi hiki.


Nimehubiri juu ya uvuguvugu ingawa kwa maneno machache, unaweza kuangalia kwenye website niliyokupa hapo juu utayapata. Uvuguvugu ndio uliomfukuza Kristo nfani ya kanisa, yupo nje na wakati huu anabisha ili apate kuingia na kama halifungui mlango basi ataenda zake. Na hivyo ndivyo litakuwa limetapikwa.


Anasimama mlangoni akipaza sauti, maana anasema mstari wa 20, mtu akiisikia sauti yangu, akimaanisha kanisa (dhehebu) au mtu binafsi akiisikia sauti yake, ndipo ataingia kwake. Hii sio sauti ya kusema nifungulie mlango kisha akaingia na kunyenyekea chini ya theolojia ya dhehebu lile, la! Hii ni sauti iletayo DHAHABU ILIYOSAFISHWA KWA MOTO (mstari wa 18) ambayo ni neno lililo moto hata kuwafanya watu hawa kuwa moto.


Ni neno ambalo ametoa ushauri kanisa linunue kwake dhahabu hiyo, ufunuo wa Mungu juu ya kizazi hiki. Ndipo mtakapogeuka na kuisikia sauti, atawarudia ninyi na kuwa watu wake. Maana hiyo ndiyo amri kuu na nyingine zimo ndani yake kuwa ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA kama alivyoihubiri Yeremia nabii.


21 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tieni sadaka zenu za kuteketezwa pamoja na dhabihu zenu, mkale nyama. 
22 Maana sikusema na baba zenu, wala sikuwaamuru kwa habari za sadaka za kuteketezwa na dhabihu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri; 
23 lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, SIKILIZENI SAUTI YANGU, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa. 

Yeremia 7:21-23.



Yeremia anasema maagizo hayo kama ya kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi hayakuwa agizo la Mungu; ijapokuwa ndiye aliyeagiza. Lakini yalikuwa ya pili baada ya amri ya kwanza kuwa ISIKILIZENI SAUTI YANGU, na sauti hiyo mojawapo ni hiyo ya Yeremia na hao manabii wengine. Na sauti hiyo ndiyo yenye maagizo na njia aitakayo Bwana mbali na akili za mwanadamu (theolojia).


Kwamba kama mtu angeleta dhabihu kwa ajili ya najisi au dhambi ili apate kuondolewa ile najisi au dhambi lakini hataki KUITII SAUTI YAKE (Hao manabii), Bwana Mungu anasema mtu huyo asidhani kuwa damu ya wale wanyama ingemwondolea najisi au dhambi. Maana anasema;


6 Maana nataka fadhili wala si sadaka; na KUMJUA MUNGU kuliko sadaka za kuteketezwa.

Hosea 6


Kumjua Mungu ni kupokea maarifa yatokayo kwake, ni kuisikia sauti yake yeye aliyetumwa na Yeye.


29 Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.

Yohana 6


Lakini Israeli hakufanya hivyo, na Kristo katika kizazi hiki yaani neno lake linasimama kinyume na wakristo yaani madhehebu kwa sababu ya uvuguvugu, hata litubu. Lakini kanisa limefunga mlango, likisema halina haja na neno lingine, lina theolojia iliyokamilika ambayo inanena mambo yote mpaka mwisho utakavyokuwa. 


Kwamba litanyakuliwa na kwenda mbinguni, wakati ambapo Kristo analiambia huendi mbinguni katika hali uliyo nayo ya uvuguvugu isipokuwa utubu. Maana amesema;

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.


Ahadi kwa kanisa hili sio unyakuo, bali mambo mawili tu, kutubu na kusafishwa kuwa moto au kukataa kutubu na kutapikwa usiwe wa kristo. Hakuna mtu atanyakuliwa katika dhehebu liwalo lote hata wabranhamist. Wote wako chini ya neno hili, ISIKILIZIENI SAUTI YANGU, na mtu akitii na kufungua mlango ataingia kwake.


Yeye Kristo atakuwa Kristo kwa kizazi hiki kama mtaisikiliza sauti yake, nanyi kuwa watu wake. Naam, imetimia kama alivyonena Isaya kusema;


8 Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema Bwana. 
9 Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. 
10 Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; 
11 ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma. 

Isaya 55:8-11.


Mawazo ya mwanadamu ni kusubiri unyakuo, mawazo ya Mungu ni kuwa hao hao wanadamu wanaomsubiria Kristo mawinguni, lakini yeye (Kristo) anagonga mlangoni kwao wapate kutubu kutoka katika mawazo yao na njia zao.

Tena kwamba kama Kristo alivyolitamka neno hili kwamba NITAKUTAPIKA UTOKE KATIKA KINYWA CHANGU kama hutatubu, naam, halitarudi kwake bila kuwatapika ikiwa hawatubu. Lakini maneno haya nayanena kwenu mpate kufahamu kuwa mmesimama mahali pa uharibifu na giza.


Nanyi badala ya kumwita Bwana alete nuru, ninyi mnasema hatuna haja na nuru, tuliyonayo inatutosha, ambayo ni mafundisho mliofundishwa na wanadamu (theolojia) Mathayo 15:7. Naam, ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA.


Mawasiliano;

(+255) 0755 251 999.

MATENDO YA SHERIA NI NINI NA KWA NINI HAYALETI HAKI?

NEEMA, NA MAUTI ILETWAYO NA NEEMA!

ANDIKO HUUA BALI ROHO HUHUISHA

WASIO HAKI HUNENAJE KWA LUGHA?

HAKUTAKUWA NA UNYAKUO JUU YA KIZAZI HIKI!

        CHANGIA KUPITIA

 

          NMB:       22510119402

          MOBILE: 255755 251 999

​​

             MASHIBE ELIAS NTINGINYA

Mawasiliano:

 

+255 755 251 999

Mbezi, Dar-es salaam

  • Facebook
  • Instagram
  • X
  • TikTok
bottom of page