top of page
2 Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya.
3 Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.

Mwanzo 2


Bwana Mungu alifanya kazi siku sita, ya saba akapumzika kwa lugha nyingine akastarehe. Kupumzika ni kuacha kufanya kazi kwa mda, sio kwamba kazi imeisha, hapana. Bali unaacha kwa mda kisha baadae utaendelea. Pumziko hilo huwa ni kuingia kwenye raha fulani kwa sababu haufanyi kazi.


Pumziko lolote kimsingi huwa ni kuingia furahani, rahani. Mtu anayelima anapopumzika kwa dakika tano au kumi, hizo dakika tano au kumi ni dakika alizostarehe. Na siku zote kila kazi ina pumziko katika maisha ya kila siku.


ALIIBARIKI SIKU YA SABA.


Bwana Mungu alipofanya kazi ya uumbaji kwa siku sita alipumzika siku ya saba. Siku hiyo akaibariki. Kubariki ni kufurahia, kwa karamu au chochote chenye kuleta furaha. Siku ya pumzi hilo hamna kazi nyingine zaidi ile ipasayo pumziko. 


Sawa na siku ya msiba, watu huacha kila kitu isipokuwa shughuli inayohusu msiba, Ndivyo na sikukuu, kila mtu hujitia katika kazi ihusuyo sikukuu. Hivyo siku ya saba ya pumziko hamaanishi kulala, bali mtu aachapo kazi zake zote, hujitia katika kazi maalumu kwa ajili ya ile siku yenyewe au lile pumziko.


Lile pumziko ndio Sabato, tafsiri ya neno sabato ni kupumzika. Sabato sio siku bali pumziko! Lakini kwa sababu pumziko hilo liliangukia siku fulani, basi siku hiyo huitwa siku ya kupumzika (siku ya sabato au sabato).


Hivyo siku aliyopumzika Bwana Mungu ni siku ya saba, ndipo siku hiyo nzima ikaitwa Siku ya sabato au sabato! Yaani pumziko la Bwana, kuingia katika furaha ya Bwana.


Lakini pumziko hili halikuwa katika siku peke yake bali mwaka wa saba pia katika sheria za Musa ni sabato, walawi 25:1-4, 


3 Panda shamba lako miaka sita, na miaka sita lipelee shamba lako la mizabibu, na kuyachuma matunda yake; 
4 lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni SABATO ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi, ni Sabato kwa Bwana; usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako la mizabibu. 

Vivyo hivyo pia sabato nyingine ilihesabiwa baada ya sabato 7 katika nchi, yaani kila baada ya miaka 7 ni sabato, lakini baada ya sabato saba za namna hii yaani miaka 7 mara 7 ambayo ni 49, mwaka wa hamsini ukawa Sabato nyingine iitwayo Yubilee. (Walawi 25: 8-11).


Mwaka wa 49 na mwaka 50 ni miaka ya sabato yote miwili inayofuatana. Lilikuwa ni pumziko nchi yote ya Israeli, kwamba wasilime shamba wala kupelea n.k.


Hayo yote ni mapumziko au sabato zilizokuwa zimeamriwa na Bwana. Kutoka siku ya saba kwenda mwaka wa saba na hata miaka 50. Bwana alifanya hayo ili watu waingie katika pumziko la Bwana, wastarehe wao pamoja na vyote walivyonavyo, na ardhi yote kama Yeye alivyopumzika.


NINI MAANA YAKE PUMZIKO HILI


Ukiangalia vyema utagundua mapumziko haya yamekuwa si sherehe kwa watu wala kupumzika kwa furaha bali kama adhabu fulani, au kufanya kwa ajili ya Bwana tu lakini wanadamu hawakuyatenda kana kwamba ni pumziko kweli bali kwa kutii sheria tu. Ndipo swali linakuja kwa nini Sabato?


Imeandikwa kuwa mwanadamu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Kumbukumbu 8:3, Mathayo 4:4, luka 4:4, 


Naam, neno hili ‘hataishi kwa mkate tu’ maana yake ni kuwa chakula ni muhimu lakini si yote. Uzima wetu hautegemei chakula tu, bali kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu aliye na mamlaka juu ya chakula hicho pia.


Maana yake kinachompa mwanadamu ukamilifu, ni neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Kwa sababu hiyo Mungu ameweka majira mbele ya mwanadamu akumbuke hilo na kulifanya, kwamba yeye ndiye aliyemuumba, na yeye ndiye aliyekiumba chakula na mvua. Na kwa sababu hiyo anayepaswa kutegemewa ni Mungu na si chakula.


Hivyo katika siku sita akapewa kufanya kazi lakini siku ya saba, apumzike kwa kuutafta uso wa yeye aliyeviumba vyote, mwaka wa 7 na mwaka wa 49 na 50 wapumzike kwa ajili ya kuutafta uso wa Bwana, na kumtegemea yeye peke yake pasipo shaka kwa kuwa yeye ndiye chakula cha kweli.


Hivyo anapoweka Pumziko yaani Sabato, ni kwa ajili ya watu wamwadhimishe Yeye, kwa sababu kwa neno lake vyote alivifanya na neno lake anaweza kuvitowesha vyote. Hilo neno lake ni lipi wakati huo walipo? 


NENO LITOKALO KATIKA KINYWA CHA MUNGU NI LIPI?


Neno ambalo mwanadamu ataishi kwalo ni hilo litokalo katika kinywa chake. Ndio hilo ambalo kila siku ya sabato lilipaswa kufundishwa. Neno linalotoka katika kinywa cha Mungu ni ufunuo wa Mungu kwa watumishi wake.


Katika Israeli ni walawi ndio waliokuwa wanasimama siku za sabato ili kuwajulisha watu aliyoyafunua Mungu, lakini walawi hawa walibadili mambo ndani ya kanisa. Wakaacha kwenda kwa ufunuo utokao kwa Mungu, wakaenda kwa ufunuo utokao kwa wanadamu.


Wakafundisha yaliyo mapenzi yao na si mapenzi ya Mungu, wakashika roho zao na si ya Mungu kama ilivyoandikwa.


13 Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.

 

Yeremia 2:13


Huu ni ufunuo wa Mungu kwa njia Yeremia, akifunua juu ya watumishi wake walawi waliomwasi, waliwakosesha Israeli kwa makosa mawili, kwanza walimwacha Mungu aliye chemchemi maji ya uzima. 


Maji ya uzima ni neno la Mungu na chemchemi ni mahali linapotoka neno hilo. Kwa lugha rahisi waliacha ufunuo wa Mungu, kisha wakajifanyia njia nyingine ya kupata hilo neno la Mungu.


Wakajifanyia mabirika, yaani visima ambavyo watahifadhi maji ambayo ni maneno ya Mungu. Hivi ni vyuo vya kitheolojia kama kila dhehebu lilivyo hata leo. Vyuo vya kitheolojia ndiko walawi wa agano la kale na walawi wa agano jipya walivyo.


Hivyo siku ya sabato wakafundisha maneno yao wenyewe na si neno la Mungu litokalo katika kinywa chake. Ndipo kwa sabahu hiyo wakalihalifu pumziko lile la Bwana.


13 Kama ukigeuza mguu wako usihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, WALA KUSEMA MANENO YAKO MWENYEWE; 

Isaya 58:13


Hapa ni ufunuo wa Mungu uliokuja kwa Isaya mtumishi wake kuhusu uhalifu wanaoufanya siku ya pumziko la Bwana. Walimu hawa walikuja na neno lao wala si neno la Mungu litokalo katika kinywa chake, walikuja na ufunuo wa damu na nyama, theolojia!


Hivyo neno la Mungu litokalo katika kinywa chake lilifungiwa nje ya kanisa. Bwana alipokuja kwao Israeli kwa njia ya manabii, alikuwa kama mwizi katika nyumba yake mwenyewe kwa sababu walawi waliiuza kwa mungu mwingine, theolojia.


Neno hili la Mungu litokalo katika kinywa chake lilipaswa kuwa chakuka katika siku ya pumziko yaani sabato. Vile vile na mwaka wa saba na jubilee. Nalo pumziko ni kila siku ya 7, na kila mwaka wa 7 na 50.


Hivyo siku ya saba wamepewa wanadamu wamkaribie Mungu, lakini kwa sababu ya walimu, wachungaji, n.k, wamewaiba watu wasimjue Mungu kwa sababu walimu wao wameacha ufunuo wa Mungu wakafuata wa kwao. 


Na mwaka wa saba ni mwaka wa Bwana uliokubaliwa yaani sabato ya Bwana juu ya nchi, kwamba wailimayo hiyo nchi waache na kupumzika ili Bwana alete neno lake (Isaya 61:2), ili  kuwakomboa wanaotumikishwa katika dhambi. Maana yake huu ni mwaka ambao walimu, wachungaji, makuhani, manabii n.k wanapasa kuacha kazi yao na utumishi wao na kumsikiliza Bwana. 


1 Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao. 
2 KUTANGAZA MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao

Ni mwaka wa kuijiriwa kwa watumishi wake, ni mwaka kuwaondoa katika utumishi wao kwa nguvu kwa sababu ya makosa yao, na kuwaacha huru waliowafunga katika dhambi kwa maneno yao yasiyo kweli. Kuja kwake Kristo ilikuwa ni sabato juu ya nchi ya Israeli.


Na kwa sababu walimu hawakuijua sabato, walikalili siku na miaka, walikuja kupotea, hasira ya Bwana ikawa juu yao. Akawatwaa mikononi mwake walio wake na kufuta upanga nyuma yao kwa sababu hawashiki kitakatifu siku yake; kuwaachilialia huru waliowafunga katika theolojia zao.


Siku ya saba ni ya walimu na wachungaji, lakini mwaka wa saba ni wa Malaika au manabii walio na hilo neno la Mungu ambalo huja kwa hawa walimu na wachungaji kwa sababu si amina kwa Mungu wakati wote. Huanza vizuri kisha hupotea njiani kama Adamu na kufuata roho zao wenyewe.


Leo Kanisa limekuwepo katika sabato zake, nao tayari wametenda kosa lile lile la Israeli (Yeremi 2:13), na hata Bwana amekwisha kuandika nyakati saba kwao kama nilivyotangulia kufundisha. Na hata sasa ni sabato ya Bwana, lakini hawajui. Hili ndio neno la Bwana alilokwisha kutangulia kusema labla ya nyakati hizi.


14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. 
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. 
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

Ufunuo wa Yohana 3:14-16


20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. 

Ufunuo wa Yohana 3:20


Naam, mtaishika Sabato katika mwaka wa Bwana uliokubaliwa, au mtasimama katika maneno yenu kinyume na Bwana pia kama Israeli. Naam, Bwana amekwisha kuandika siku hii mbele zake kama asemavyo;


10 Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi nami nitakulinda, utoke katika saa ya KUHARIBIWA iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.

Ufunuo wa Yohana 3:10


ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA leo tena kama Paulo alivyokwisha kuagiza (Waebrania 3,4), maana sabato ya Bwana iliyosalia kwenu ndio hii.


Mawasiliano;

(+255) 0755 251 999

SIKU YA SABATO NI IPI?

SABATO NI NINI?

KUPATWA KWA JUA KUNAMAANISHA NINI KATIKA ROHO?

MATENDO YA SHERIA NI NINI NA KWA NINI HAYALETI HAKI?

NEEMA, NA MAUTI ILETWAYO NA NEEMA!

        CHANGIA KUPITIA

 

          NMB:       22510119402

          MOBILE: 255755 251 999

​​

             MASHIBE ELIAS NTINGINYA

Testaments :

+255 755 251 999

Mbezi, Dar es Salaam

  • Facebook
  • Instagram
  • X
  • TikTok
bottom of page