top of page

Tumekwisha kutazama sabato  ni nini? Tena kwamba tukaona sabato sio siku ya saba tu bali mwaka wa saba na 50. Leo nataka tuone juu sabato ya kila siku ya saba.


Kwanza kabisa, Sabato sio siku, ni pumziko. Pumziko hili Bwana Mungu aliagiza liwe kila siku ya saba. Yaani siku sita fanya kazi lakini siku ya saba ni pumziko la Bwana au sabato ya Bwana. Ndipo linakuja swali kuwa siku ya saba ni ipi kati ya jumamosi au jumapili?


Katika taifa la Israeli, jumamosi ndio siku ya saba na ndio sabato kwao. Lakini wakristo walianza kukusanyika siku ya kwanza ya juma badala ya siku ya saba ya juma. Na tena katika dhehebu la wasabato, SDA hutambua kuwa jambo hilo limetokana na dhehebu la katoliki, mama wa makahaba (madhehebu).


Ndio nitakubaliana na katoliki kuwa mama wa makahaba, maana yake anao binti (madhehebu) aliowazaa kwa ukahaba wake, lakini miongoni mwa hao binti aliowazaa ni hao wasabato au SDA pia, lakini kwa sababu ni vipofu hawajui hilo.


Dhehebu la katoliki ndio dhehebu la kwanza, limetokana na kanisa la kwanza la mitume, likafanya ukahaba  mbele za Mungu kwa mafundisho ya wanikolai na mafundisho ya Balaam na kupelekea kuachwa kwake na kuwa dhehebu.


Dhehebu hili halikuwahi kubadili siku kutoka jumamosi kwenda jumapili, lakini lilijikuta likifanya hivyo yaani kwenda kanisani siku ya jumapili badala ya jumamosi tofauti na wayahudi bila kujua sababu. Swali la siku ipi ni sahihi lilipoanza, ndipo kanisa hili likaanza kuandika sababu iliyopelekea wawe wanapumzika au kwenda kanisani jumapili.


Lakini sio wao waliosema tunaacha kwenda kanisani siku ya  jumamosi kuanzia leo, badala yake tunaanza kwenda kanisani jumapili, hapana. Waliobadili siku ni mitume, kwa sababu ya ufunuo wa Mungu na si ufunuo wa damu na nyama kama huo wa wasabato.


Na sababu ya katoliki walioandika inatokana na ujuzi wao wa mema na mabaya, si sababu ya kweli iliyopelekea wawe wanaenda jumapili, si sababu ya mitume. Kwa sababu wakati wanaandika, tayari kanisa lilikuwa linaongozwa na wanikolai. Hivyo sababu ile ni ya wanikolai, haitoki kwa Mungu.


Lakini kama ningetaka kulinganisha kati ya wakatoliki na wasabato, ni bora wakatoliki. Maana chachu ya wasabato ni sumu mbaya kuliko ya wakatoliki. Hivyo wasabato wanapaswa kuangalia kwanza borti walilonalo ndipo itakapokuwa sawa kuangalia kibanzi katika jicho la katoliki.


Turudi kwenye siku sahihi ya sabato ni ipi kati jumamosi na jumapili. Sabato ya Bwana inapaswa kuwa siku ya saba tu na si vinginevyo. Lakini siku ya saba ni juma ngapi?


Siku ya saba sio jumamosi wala jumapili wala jumatatu au ijumaa. Na wala Bwana Mungu hakuagiza kwa kutaja jina la siku ya sabato hapana. Siku ya saba ilikuja kwa mwandamu kupewa siku sita za kufanya kazi zake, kisha siku ya saba apumzike na kuishika hiyo kitakatifu.


Siku sita alizoagizwa mwanadamu afanye kazi, hakuzitaja kwa majina kuwa ni jumapili hadi ijumaa, au jumatatu hadi jumamosi, hapana. Siku ya saba inategemea umeanza kuhesabu siku kuanzia lini. Ukianza kuhesabu jumatatu kuwa ndio siku ya kwanza, siku ya saba itakuwa Jumatatu. Ukianzia jumamosi, siku ya saba itakuwa jumamosi.


Hivyo kwa Israeli kama alianza kuhesabu siku tunayoiita leo jumamosi, siku ya saba lazima iwe jumamosi. 


Na wala Mungu hakuweka kanuni kuwa siku ya juma sharti ianze lini kuhesabiwa, kwamba ni jumamosi au jumapili au jumatatu, hapana. Alichokisema ni siku ya saba, ambayo inaweza kuwa siku yoyote katia siku hizo saba kulingana na siku jamii fulani au watu fulani wameanza kuhesabu.


SABATO INAPASWA KUWA SIKU TAKATIFU KWA BWANA.


Moja ya masharti ya waitaftao siku ya sabato ni siku gani ni kwa sababu ni siku takatifu. Hivyo siku nyingine yoyote haiwezi kuwa sabato kwa sababu haitakuwa takatifu.


Hayo yanatoka kwa wanadamu, lakini hakuna siku iliyo takatifu kuliko nyingine. Isipokuwa unaweza kuifanya siku yoyote kuwa takatifu kwa namna unavyoiweka. Bwana hakuifanya kuwa siku fulani kuwa takatifu, lakini aliichagua siku ya saba mwanadamu aishike kitakatifu. Akaeleza na desturi za kufanya ili kuishika kitakatifu.


Hivyo sio kwamba jumamosi ni takatifu kuliko jumapili, jumatatu, n.k, hapana. Wala jumapili sio takatifu kuliko jumatano. Bali kwa kushika desturi za lile pumziko (sabato), unaifanya siku hiyo kuwa takatifu. Hivyo hakuna siku iliyo takatifu bali lile pumziko ndio takatifu kwa Bwana.


Na pumziko hilo Israeli alilinajisi kwa kuacha mambo yafanyayo pumziko hilo kuwa takatifu. 


13 Kama ukigeuza mguu wako usihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe;

Isaya 58:13


Israeli aliihalifu sabato, siku ya utakatifu/pumziko lake. Akafundisha maneno yaliyo maagizo ya wanadamu katika kusanyiko lake na kuwadanganya watu, waliosikiliza uongo. 


4 Haya ndiyo asemayo Bwana; Kwa makosa matatu ya Yuda, naam, kwa manne, sitaizuia adhabu yake isimpate; kwa sababu wameikataa sheria ya Bwana; wala hawakuzishika amri zake; NA MANENO YAO YA UONGO YAMEWAKOSESHA, ambayo baba zao waliyafuata; 

Amosi 2:4

 

Maneno yao ya uongo ni theolojia, mafundisho yanayotokana na utafiti wao na hekima za mwandamu (ufunuo wa damu na nyama) badala ya ufunuo wa Mungu. Wakashika maneno yao ya uongo kuwa ni kweli, na ile kweli ikaonekana ni ya uongo na kuitupa chini. 


Kwa sababu hiyo wakainajisi sabato yaani hilo pumziko. Bwana akaichukia hiyo siku, yaani hiyo sabato ambayo ni makusanyiko ya dini, na kila kitu walichokifanya katika siku ya sabato.


21 Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini. 
22 Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona. 
23 Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu. 

Amosi 5:21-23


Ikawa kwamba pumziko liliponajisika, Siku nayo vile vile ikanajisika. Maana imeandikwa kuwa kitu najisi kikigusa kitu kisicho najisi, kilichoguswa nacho kimekuwa najisi. Siku ya jumamosi ikawa harufu mbaya kwa ya lile pumziko lililonajisiwa.


Ndipo kwa sababu hii, akaazimu kuondolea mbali mambo ya kwanza. Akaleta ukombozi tena kwa njia ya Yesu Kristo, na desturi mpya ili kufanya upya kila kitu. 


Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.

Isaya 65:17


Mbingu mpya ni neno la Kristo na nchi mpya ni kanisa alilolizaa katika nchi katika desturi mpya. Matendo ya sheria yakabadilika na kuwa mapya.


Mitume walipoanza kukusanyika kuomba, siku ya kwanza ya juma kwa desturi za wayahudi, yaani jumapili walishukiwa na Roho mtakatifu. Kuanzia hapo walikuwa wakikusanyika siku ya kwanza ya juma kwa desturi ya wayahudi (Matendo  20:7 na 1wakorintho 16:2). 


Hata siku Yesu  aliyowatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kwake nayo ilikuwa siku ya kwanza ya juma, ukiachilia mbali siku aliyofufuka. 


Hivyo ni Mungu ndio aliamua kuitukuza siku ya jumapili badala ya ile ya jumamosi, na mitume wakafuata nyayo hizo. Wala si binadamu awaye yote aliyesema tubadili siku, kutoka hii twende hii, hapana.


Injili ya siku gani ya sabato ni fundisho la wanikolai, na dhehebu la wasabato limeanzishwa chini ya mafundisho hayo. Na kwa sababu hiyo hawamtumikii Kristo bali wako kinyume na Kristo na Mungu aliye Baba yake. Lakini kwa sababu kila dhehebu linayo mafundisho ya kinikolai, siwahukumu wasabato bali wote! Maana wote wameoza!


Na kwa sababu hiyo ISIKILIZENI SAUTI YAKE!


Mawasiliano;

(+255) 0755 251 999

SIKU YA SABATO NI IPI?

SABATO NI NINI?

KUPATWA KWA JUA KUNAMAANISHA NINI KATIKA ROHO?

MATENDO YA SHERIA NI NINI NA KWA NINI HAYALETI HAKI?

NEEMA, NA MAUTI ILETWAYO NA NEEMA!

        CHANGIA KUPITIA

 

          NMB:       22510119402

          MOBILE: 255755 251 999

​​

             MASHIBE ELIAS NTINGINYA

Wills:

+255 755 251 999

Mbezi, Dar es Salaam

  • Facebook
  • Instagram
  • X
  • TikTok
bottom of page