
Matendo ya sheria ni maagizo ambayo mtu akiyatenda hayo anahesabiwa haki mbele za Mungu. Yaani ukamilifu wa mtu utatokana na utii na kufuata hayo maagizo bila kuangusha hata moja.
Matendo haya sheria katika torati ni haya;
kutahiriwa,
kushika sabato,
kushika sheria za vyakula safi na najisi,
kutoa dhabihu kwa ya ondoleo la dhambi,
kushika sikukuu takatifu.
Hizi ni desturi za torati namna ya kuishi katika utakaso wakati wote, utii na kuishi katika haki. Hayahusishi dhambi yenyewe bali yanamwondolea hatia au kumfanya mtu asamehewe dhambi yake mbele za Mungu na kumfanya awe mwenye haki.
Kiufupi matendo hayo ndio torati yenyewe, na ndio neno la Mungu lililokuja kwa mkono wa Musa ili kuwatakasa wana wa Israeli kutoka katika dhambi, wawe watakatifu mbele za Mungu kama Yeye alivyo mtakatifu.
Lakini dhambi kama uzinzi, uasherati, wivi, kuabudu sanamu, uongo, kuua, chuki n.k si matendo ya sheria, ijapokuwa yapo katika sheria. Mtu hawezi kuyafanya haya akahesabiwa haki mahali popote na katika agano lolote. Yeye atatendaye haya ametengwa na Mungu kwa kuwa ametenda dhambi.
Na ili arudiwe na Mungu ndipo anatakiwa atakaswe kulingana na hilo agano la Mungu. Katika agano la kwanza alipaswa kushika matendo ya sheria, na katika agano jipya ni hivyo hivyo, isipokuwa matendo ya sheria yanabadilika katika agano jipya.
Matendo ya sheria yamekuwepo kwa ajili ya watu na si watu kwa ajili ya matendo ya sheria, hivyo matendo ya sheria ni mfano wa chumvi katika chakuka. Yamekuwepo kuwafanya watu wa Mungu wawe safi katika safari ya kufikilia kuwa watakatifu kama Mungu alivyo mtakatifu.
Lakini ikiwa chakula kimeharibika, itafaa nini kutia chumvi? Ndipo kwa sababu hiyo Israeli alimwacha Bwana, asiisikilize sauti yake, akajifanyia gongo lake mwenyewe kwa mikono yake liwe badala ya Mungu kama Hosea asemavyo;
12 Watu wangu hutaka shauri kwa gongo lao, na fimbo yao huwahubiri mambo; maana roho ya uzinzi imewakosesha, nao wamekwenda kuzini mbali na Mungu wao.
Hosea 4
Israeli aliliacha gongo la Mungu na kujifanyia gongo lake (theolojia), nalo likamhubiri mambo, wakaenda kinyume na maagizo ya Mungu kwa kuheshimu theolojia zao. Lakini matendo ya sheria yakabaki vile vile, na kwa sababu hiyo, chumvi itafaa nini katika chakula hiki? Yeremia kwa neno la Mungu anasema na hao walio na matendo ya sheria lakini hawaendi kwa Roho wake katika Neno lake kuwa,
25 Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapowaadhibu wote waliotahiriwa katika hali yao ya kutokutahiriwa;
Yeremia 9
Watu hao waliotahiriwa maana yake ni watu walio na matendo ya sheria lakini mioyoni mwao Mungu yupo mbali nao, wanasoma neno la Mungu na kwenda kwa roho zao wenyewe. Naam, nii vuguvugu kama walivyo wakristo leo (ufunuo 3:14-20).
Nao waliadhibiwa na kutapikwa kwa neno la Kristo na neno la mitume wake kama huyu Paulo aliyenena maneno hayo akiwaambia matendo ya sheria hayawapa haki tena hata mmoja wanu.
20 kwa sababu HAKUNA MWENYE MWILI ATAKAYEHESABIWA HAKI MBELE ZAKE KWA MATENDO YA SHERIA; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.
Warumi 3:20
Naam, ilitimia kwao kama ilivyotabiriwa, lakini andiko hili linatumika na waliopata kibali cha kuingia katika agano la pili kinyume na Roho wa Mungu, sawasawa na walivyofanya wayahudi.
Ni wazi leo kila asomaye andiko hili, nafsi yake huichukia torati mara. Na wengi adui yao amekuwa torati kwa sababu ndiko ziliko andikwa hizo sheria. Na kwa sababu hiyo Neema au Kristo kwao ni kuichukia torati, na kwamba Kristo alikuja ili kuondoa laana ya torati yaani torari yenyewe.
Tafsiri hiyo inatoka kwa wanadamu wala si kwa Mungu, kwa sababu Kristo alikwisha kusema hakuja kutangua torati bali kuitimiliza, yaani kukamilisha kilichokuwa kimebakia. Ijapokuwa Paulo katika nyaraka zake amejaribu kuonesha torati kuwa inaleta laana au sheria inafunua dhambi.
Lakini nataka nitofautiane kidogo na Paulo mtume, sio kwa sababu hayupo hapa leo, hapana. Hata angekuwepo ningepingana naye kama yeye mwenyewe alivyompinga na Petro (Wagalatia 2:14). Katika msitari hapo juu amejaribu kueleza sheria inafunua dhambi, kana kwamba ikiwa hakuna sheria hakuna dhambi (na hii imekuwa injili ya baadhi ya wakristo leo).
Lakini ikiwa hakuna sheria, hakuna mabaya wala mema. Na sababu hiyo inaondoa uwepo wa Mungu na Kristo pia, maana neno la Mungu ni juu ya mabaya na mema, ambayo hayatakiwi na yanayotakiwa, ambayo yanadhihirika kwa lile neno la Mungu. Kristo hakuja ili tuwe wapumbavu, yaani kutojua mabaya na mema.
Mungu wetu wa mbinguni ni Mungu wenye ujuzi wa mema na mabaya, kama nyoka alivyosema Mwanzo 3:5. Na ujuzi huo ndio anatufundisha uzao wake kupitia sheria zake. Hivyo kufunuliwa kwa dhambi kupitia sheria sio kuleta uovu, bali jambo takatifu ili mwanadamu ajitenge na uovu.
Maana sio sheria inayoleta maovu, bali maovu ndio huleta sheria. Watazameni watu wa ulimwengu huu katika hekima zao, hutunga sheria kila kukicha na kuzibadilisha kuendana na mbinu mpya za uovu katika jamii. Hawatungi sheria ili kuwafanya watu wawe waovu bali kuwadhirisha walio waovu wapate hukumu.
Hivyo sheria haikuwa na kosa lolote, na hata isingeletwa bado dhambi iko, kwa sababu sheria haileti dhambi bali inaleta mwanga wa kuielewa dhambi ili wapendao nuru na uzima wajitenge na dhambi. Sheria imekuja kumsaidia mwanadamu ajue yaliyo haki na yasiyo haki, achague mema na kuchukia mabaya.
Naam, katika kosa la ulimi kuna mtego kwa waovu. Na kwa sababu hiyo kila amchukiaye Mungu ndani yake, kosa la ulimi litakuwa faraja kwake. Bwana ameruhusu makosa madogo madogo kama haya ili yawe chakula cha waovu. Hivyo sheria au torati ilikuja kwa sababu ya makosa ili ayajue na kujitenga nayo.
Lakini sheria ni kama moto, inaweza kuwa ngumu kulingana na aina ya watu, moto unaopaswa kuyeyusha chuma hauwezi kuwa sawa na moto unaopaswa kuunguza majani mabichi. Vivyo hivyo na kinyume chake, na kwa sababu hiyo sheria ilikuwa ngumu kwa wana wa Israeli kwa sababu ya wingi wa makosa na mioyo migumu.
Hivyo tukirudi katika Matendo ya sheria, Paulo mtumishi wa Kristo alisema yaliyo kweli, kuwa matendo ya sheria hayawapi watu utakatifu (haki), ikiwa njia ya watu hao si ya haki. Israeli alipomwacha Bwana na kuchagua ujuzi wa mwanadamu yaani hekima za wanadamu (theolojia), alibatilisha agano zima. Na kufanya matendo ya sheria yawe bure kwao na kufanya wamwabudu Mungu bure.
7 Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema,
8 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami.
9 NAO WANIABUDU BURE, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.
Mathayo 15:7-9.
Lakini matendo ya sheria yapo kila agano, kama katika agano la pili, agano la neema linayo matendo haya mapya ya sheria, kubatizwa, kuosha miguu, kumega mkate, kunywa divai.
Hivyo kwa wayahudi, ilikuwa lazima kwao kuamwamini Kristo, ili kufanywa upya. Ilikuwa lazima kukubali kurudi katika Roho wa Mungu na kuondoka katika ujuzi wao na roho zao. Lakini niseme nini zaidi, kosa la wayahudi halipo kwetu pia? Maana hakuna hata moja walilolitenda wana wa Yakobo, lisilokuwepo kwa uzao huu wa pili.
Tazama na shoka limekwisha kuwekwa katika mashina ya miti hata sasa, ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA, msije mkaishia njiani kama Israeli, maana amesema ATAKUTAPIKA NA WEWE PIA (ufunuo 3:16).
ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA!
Mawasiliano;
(+255) 0755 251 999.