
Tumekwisha kutazama juu ya mafundisho ya maziwa ni yapi na kwa nini yanaleta uvuguvugu. Leo tuangalie mafundisho mengine ya walokole ambayo yamefanya watu wajione kuwa ni matajiri, hawataki kitu kingine kwa kuwa ni matajiri na mbele za Yeye aendaye katikati ya vinara saba wanaonekana kuwa ni vuguvugu.
MAFUNDISHO YA MALI.
Mafundisho ya mali ni yale yanayolenga kupata mali na utajiri kutoka kwa Mungu au kwenye ulimwengu huu. Mafundisho haya hayatokani na Mungu, bali yanatungwa na walimu wa madhehebu kwa ajili ya kujipatia faida. Mafundisho haya Yesu Kristo aliyanena hivi;
24 Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.
Mathayo 6:24
Neno la Yesu Kristo linasema haiwezekani kutumikia mali na Mungu, hawa ni mabwana wawili mbali mbali. Mmoja kinyume na mwingine, njia za huyu ni kinyume na njia za huyu. Neno la Mungu linalenga kuzaa watu walio watakatifu/wakamilifu kama Mungu alivyo na ili kufikia namna hii ni kwa kulitii neno lake na nia yake.
Lakini ili kanisa lisifikilie utakatifu/ukamilifu sharti ije injili nyingine itakayowatoa watu katika njia ya Mungu yaani neno la Mungu na kuwafanya bidii yao iwe katika mambo yasiyo ya Mungu. Na moja ya injili hizo ni injili ya mali. Kama njia ya kwenda mbinguni ingekuwa inaelekea kaskazini, basi njia ya injili ya mali inakuwa inaeleekea kusini.
Kwa sababu ili kuipanda injili hii ndani ya watu waendao kwa neno la Kristo aliyekataa hiyo injili, lazima kung"oa yaliyo ya Kristo. Na kung'oa huku kunakuja kimafumbo kiasi cha kuwapa sababu nzuri watu kwa nini ni sawa kuheshimu mafundisho ya mali ukamweshimu na Yesu alyeyakataa! Ni kazi ya walimu wa madhehebu kutunga uongo utakaokuwa ndio fundisho kwao.
Roho wa Mungu ananena waziwazi kwa njia ya Paulo kusema;
“Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”.
1 Timotheo 6:10
Lakini Laodikia amejipatia walimu wengi wafundishao kuipenda pesa, na kusema pesa ni sabani ya roho. Ndipo kwa sababu hii huwafundisha watu kufarakana na Mungu, wote wamemdharau Roho wa Mungu, nao wamekubaliana ni bora wafarakane na imani kuliko kuichukia pesa.
Ni wazi na bayana kuwa walimu na viongozi wa madhehebu wamemdharau Kristo na Mungu waziwazi.
Laodikia ametajirisha kwa walimu hawa na mafundisho haya. Kila neno litakalo vinywani mwa walimu wa Laodikia linaonyesha kiasi gani wanapenda fedha na nia yao ni kuwafanya watu jamii kuwa na nia kama ya kwao.
Tazama zaburi ya mtu mmoja aliyetatizwa na mafundisho haya zamani za kale;
Zaburi 73 1-18.
¹ Hakika Mungu ni mwema kwa Israeli, Kwa hao walio safi mioyo yao.
² Nami miguu yangu ilikuwa karibu na kupotoka, Hatua zangu zilikuwa karibu na kuteleza.
³ Maana naliwaonea wivu wenye kujivuna, Nilipoiona hali ya amani ya wasio haki.
⁴ Maana hawana maumivu katika kufa kwao, Na mwili wao una nguvu.
⁵ Katika taabu ya watu hawamo, Wala hawapati mapigo pamoja na wanadamu.
⁶ Hivyo kiburi kimekuwa mkufu shingoni mwao, Jeuri huwavika kama nguo.
⁷ Macho yao hutokeza kwa kunenepa, Wameipita kadiri ya mawazo ya mioyo yao.
⁸ Hudhihaki, husimulia mabaya, Husimulia udhalimu kana kwamba wako juu.
⁹ Wameweka kinywa chao mbinguni, Na ulimi wao hutanga-tanga duniani.
¹⁰ Kwa hiyo watu wake hugeuka huko, Na maji yaliyojaa humezwa nao.
¹¹ Nao husema, Mungu ajuaje? Yako maarifa kwake aliye juu?
¹² Fahamu, ndivyo walivyo wasio haki, Na kwa kustarehe sikuzote wamepata mali nyingi.
¹³ Hakika nimejisafisha moyo wangu bure, Nimenawa mikono yangu kwa kutokukosa.
¹⁴ Maana mchana kutwa nimepigwa, Na kuadhibiwa kila asubuhi.
¹⁵ Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako.
¹⁶ Nami nalifikiri jinsi ya kufahamu hayo; Ikawa taabu machoni pangu;
¹⁷ Hata nilipoingia katika patakatifu pa Mungu, Nikautafakari mwisho wao.
¹⁸ Hakika Wewe huwaweka penye utelezi, Huwaangusha mpaka palipoharibika.
Huyu ni Asafu mtumishi wa Mungu, alipitia taabu na kujitesa kwa ajili ya Bwana, lakini alichokiona ni kuwa waovu hawapati taabu kama yeye anavyopata taabu katika kumtumikia Mungu. Waovu anaowazungumzia hapa sio watu wa mataifa ambao ni nje ya Israeli; hapana, bali ni watu wa Israeli wanaokwenda kinyume na Neno la Mungu.
Watu ambao injili yao ilikuwa mali, mvivyo na kileo (Mika 2:11). Asafu alijitesa kwa maumivu mengi kuipata hekima ya Mungu lakini hawa wengine wanaimba na kucheza na kufurahia Mungu anavyowafanikisha. Mafundisho yao yalikuwa kufanikiwa, kubarikiwa, kupendwa, n.k.
Asafu alikuwa karibu na Yeye kubadili mtazamo wa namna ya ufundishaji na uimbaji wake ili awe kama moja ya walimu hawa waliokuwa maarufu wakifundisha habari za mali na mafanikio. Ndipo mstari wa 15, anasema;
¹⁵ Kama ningalisema, Nitasimulia kama hayo; Kumbe! Ningaliwadanganya kizazi cha wana wako.
Baada ya mda mrefu wa kutamani kuiga mafundisho yao, alipata ufahamu na kuelewa kuwa watu hawa si watumishi wa Mungu, bali wamepewa kutenda haya ili wapate kuharibiwa. Asafu anasema kama ningalisimulia kama hayo, NINGALIWADANGANYA KIZAZI CHA WANA WAKO!
Alipata kujua yale mafundisho ni uongo kwa sababu yanakinzana na kauli za Mungu. Na kila anayefundisha kanisa mafundisho haya anawadanganya wana wa Mungu. Na kwa sababu hiyo walimu wanaofundisha injili ya mali ni waongo yaani walimu wa uongo.
Ni kweli watu hawa wanafanikiwa, wananawili na kufanikiwa lakini njia yao ni utelezi, mara baada ya kuufurahia udhalimu wao watashuka kuzimu maana njia yao pana ndiko inakoelekea.
Kama Asafu angekosa maarifa ya kutosha, yeye pia angekuwa mwalimu wa mafundisho ya mali na kupata sifa katikati ya watu wafurahiao udhalimu. Naam, kama mwalimu mkubwa namna hii alikaribia kumezwa na mafundisho hayo? Itakuwaje kwa watoto wadogo? Maana Laodikia ni watoto wadogo katika roho, kwa sababu wanakunywa maziwa na si chakula kigumu.
Mafundisho haya yamekwisha kuteka madhabahu zote za Kristo, nayo ndiyo yanajulikana kuwa mafundisho ya Kristo kwa watu hawa, na hii ni moja ya sababu kwa nini Roho wa Mungu ameondoka ndani ya makanisa, akakaa nje na kuanza kubisha Laodikia apate kufungua mlango.
Yesu Kristo aliuliza, itamfaidia nini mtu akiupata ulimwengu wote halafu akapata hasara ya nafsi yake? Lakini walimu wa Laodikia wanataka kila mtu anayemwamini Kristo ajiulize yeye mwenyewe kuwa itamsaidia nini akimpata Kristo halafu akafa masikini?
Hivyo injili ya watu hawa inaonekana wazi kuwa, Kristo alikufa ili watu wawe matajiri, biashara zao ziinuke, wanunue magari, wasafiri kwenda ulaya, nyota zao za biashara zing’ae, biashara zikue, wapate wachumba n.k. Kwa sababu hii, Kristo wao ni tofauti na yule aliyekufa msalabani.
Ndio maana hawafati roho wa Kristo, wala kutetemeka wanaposoma maneno yake. Nao wanahubiri Kristo mwingine, na njia ya kweli wanaishambulia kwa maneno yasiyotamkika ili kuikomesha kweli mioyoni mwa watu.
Kila mtu anayesikiliza injili hizi za mali, haiwezekani tena kuipenda kweli bali ataidharau na kuichukia. Watu wasikilizao uongo huu ni watu wanaobubujikwa na tamaa za mali za ulimwengu huu, nao kwa nje huonekana wameokoka na midomoni mwao Kristo yu karibu lakini mioyoni mwao wanatafta mali na utajiri. Wat hawa ndio huwatia nguvu manabii wa uongo waendelee kuua roho za watu.
Maana imeandikwa ;
Mika 2
¹¹ Mtu akienda kwa roho ya uongo, akinena maneno ya uongo, akisema, Nitakutabiria habari ya mvinyo na kileo; mtu huyu atakuwa nabii wao watu hawa.
Watu hawa huabudu tamaa zao kwa jina la Yesu Kristo, na Yesu Kristo wamemchukia. Nae anaye wahubiria kulingana na tamaa zao ndio huwa nabii na mwalimu na mchungaji wao. Zaidi ya hao hawataki wengine, kisha baada ya kutumikia mafundisho haya hujinena ya kuwa ni watakatifu, hawana kosa na wanangoja unyakuo au kuja kwa Yesu mara ya pili.
MATOKEO YA MAFUNDISHO YA MALI.
Kama tulivyotangulia kuona kuwa injili ya mali hugeuza kila lililo la Mungu, na kuhubiri kinyume cha kila neno la Mungu. Injili hii huhubili ili kuwafanya watu kuwa matajiri na si utakatifu.
>Na kwa sababu hiyo mtu mtakatifu kwa watu hawa ni yeye aliye na mali.
>Mtumishi wa Mungu wa kweli kwa watu hawa ni yule mwenye pesa, masikini wote hawana Mungu.
>Watu wenye dhambi ni hao masikini, nao ndio wenye mapeo na kila laana.
>Mambo ya mbinguni ni upuuzi mbele ya injili ya mali, bali mbingu yao ni kuwa na hela, kiama ni kuwa maskini.
>Mungu wao na Kristo wao ni Pesa, nao wamesimama kama jeshi vitani, wakifanya vita na wana wa Mungu kwa sababu ya umasikini wao, na kuwaona hawana Mungu kama mungu wao.
Injili hii huwasifu na kuwapa haki waovu kuwa ndio wema, na wema kuwa ndio waovu. Kila asiye na pesa amelaaniwa na Mungu wao yaani miungu yao. Wanaye si Kristo mmoja bali makristo wengi wa kuwaokoa na umasikini wa Yesu Kristo ili kuwafanya wawe matajiri kama Bill gate, elon Musk, Jeff Bezos n.k, watu ambao ni malaika kwa watu wa injili hizi.
Tena, kwamba wahubiri wake wanao upanga ulao watu wema na kuwaponya waovu kama Ezekieli alivyonena akisema;
19 Nanyi mmeninajisi kati ya watu wangu, kwa ajili ya makonzi ya shayiri na vipande vya mkate, ili kuziua roho za watu ambao haiwapasi kufa, na kuzihifadhi hai roho za watu ambao haikuwapasa kuwa hai, kwa kuwaambia uongo watu wangu wasikilizao uongo.
Injili ya mali insimama inasimama kinyume na Kristo aliyeichukia, nayo inasimama kinyume na kila aendaye kwa neno la Kristo. Maana mtu muovu kwa watu wa mali ni yeye anayemchukia Mungu wao MALI.
Ndipo kwa sababu hii walimu wa injili za mali hushindana na kila neno la Mungu ili mungu mali apate kumiliki. Huwazomea wana wa Mungu wakisema yuko Mungu wenu na Kristo wenu mnayesema anawapenda? mnawezaje kusema anawapenda asipowapa mali kama sisi? Nao wanamfanya kila anayeokoka afikilie kupata utajiri kana kwamba ndio agizo la Mungu.
KANUNI YA KUBARIKIWA NA MUNGU NI HII.
Mathayo 6:31-33
31 Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini?
32 Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote.
33 Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.
Tafta kwanza ufalme wake na haki yake! Si kwamba Mungu anapenda uteseke, ulale njaa, bali kama ilivyoandikwa;
49 Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto.
Marko 9:49.
Hii ndio njia pekee kwa kila amwaminiye Yesu Kristo kuweza kufikilia ukamilifu. Kwamba atatiwa chumvi, yaani maarifa na mwenendo kwa njia ya majaribu. Utajaribiwa kwa umasikini, kukosa mme, kukosa cheo, heshima n.k Ili Mungu apate kujua ikiwa hautamtenda dhambi ama kumwacha yeye kwa sababu ya vitu hivyo unavyovitamani.
Lakini Laodikia hataki kitu kingine isipokuwa mali na utajiri na kwa sababu hiyo hajioni kuwa analo kosa bali anajiona amefanikiwa na kufikia ufunuo mzuri anaoupenda na kumtajirisha.
Baraka za Bwana zitawafuata hao walichao neno lake, ili kuwapa mema baada ya taabu yao. Naam, alaaniwe kila atakaye mshahara pasipo kufanya kazi. Maana azungukaye kutafta utajiri wala hautafti ufalme wake na haki yake ni mtu ambaye hataki kufanya kazi lakini anataka mshahara. Hataki kutafta ufalme wa mbinguni lakini anataka kuongezewa.
Ndipo kwa sababu hii walimu na manabii na mitume na wachungaji, huwaloga watu jamii kwa mafundisho ya uongo kisha wanawapatia dawa ya uongo na kujitwalia hizo mali zao.
Ndipo utasikia, wamekuloga, wamekuibia nyota, wanataka usifanikiwe, waliiba nyota yao ukiwa mtoto. Miti na mijusi imekuwa sababu ya mikosi, viumbe ambavyo vilikuwepo kabla ya umasikini wako.
Mafundisho haya ni ushirikina, hakuna aliyekuondolea nyota yako isipokuwa dhambi yako wala hakuna awezaye kukuondolea nyota isipokuwa dhambi. Kama ambavyo uzima wa milele uliondoka kwa Adamu si kwa sababu ya umasikini wala washirikina bali kwa sababu aliacha maagizo ya Bwana Mungu na kushika ya yule mwingine.
Mtu anayefundisha mafundisho haya, huyo ndiye mchawi na mlozi na mwizi wa ngota yako, huyo ndiye akutiaye laana na umasikini. Huyo ndiye akufundishaye kuabudu sanamu, naye ndiye mwalimu wa uongo na mtu akutiaye uvuguvugu na upofu usije ukajiona vuguvugu.
Naam, hakuna aendaye kwa mafundisho haya awezaye kuwa bibi harusi wa Kristo isipokuwa akitubu leo.
ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA!
Mawasiliano;
+255755 251 999.