
Moja ya tahadhari iliyotolewa katika maandiko ni manabii wa uongo, hivyo ni sharti kuwajua na kujiepusha nao. Maana hao urithi wao ni ghadhabu ya Mungu. Na mtu akikosa maarifa akaambatana nao, basi ajue na kufahamu kuwa atakinywea kikombe chao.
Nabii ni mtu aliye na unabii, na unabii ni maneno au ujumbe kutoka kwa Mungu. Nabii wa uongo ni mtu aliye na ujumbe usiotoka kwa Mungu, ujumbe wa uongo. Lakini uongo siku zote unakuwepo baada ya ukweli kuwepo, pasipo ukweli hakuna uongo.
Hivyo mtu awaye yote hana udhuru kusema sikujua kuwa ni uongo, maana tayari ukweli uko. Uongo ni maneno yanayoelezea jambo kinyume na lilivyokuwa au lilivyo au litakavyokua. Na kwa sababu hiyo, nabii wa uongo ni mtu anayenena uongo juu ya Bwana au Neno lake.
Manabii wa uongo si kwamba ni wale wanaotumia cheo cha unabii peke yake, hapana, bali kuna walimu, wachungaji, wainjilisti, mitume, n.k. Kwa sababu kinachowafanya wawe waongo sio jina bali wanachokihubiri au ushuhuda wao.
KUTOKEA AU KUZALIWA KWAO MANABII WA UONGO.
Kwa sababu ya sifa yao kuwa ni waongo, watu wengi huamini hawakuitwa na Mungu, labda ni wachawi au wametumwa na freemason n.k. Lakini nataka ufahamu kuwa nabii wa uongo ameitwa na Mungu kama kila mtu anavyoitwa.
Na kwa sababu hiyo manabii wa uongo huitwa kama jinsi wanavyoitwa manabii wa kweli. Tofauti ni moja kwamba kweli hutangulia ndipo uongo unafuata. Nabii wa Mungu hutangulia na akiisha kuhubiri ujumbe wake ndipo wale wa uongo wanafuata.
Wakati Bwana Mungu amwitapo mtu aje kwake, naye akija hufika na kutega sikio asikie asemayo Bwana wake. Na kwa sababu neno la Mungu huja kwa njia ya ufunuo, mtu yule huketi katika baraza la Mungu kwa mda mrefu ili apate maagizo ya Bwana wake.
Baraza walilokaa manabii wa Mungu si baraza walilokaa manabii wa uongo. Zipo baraza mbili, mahali manabii hawa huketi ili kupokea ufunuo.
21 Mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.
22 LAKINI KAMA WANGALISIMAMA KATIKA BARAZA YANGU, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya, na uovu wa matendo yao.
Yeremia 23:21-22
BARAZA LA MUNGU.
Mstari wa 22 unaonyesha baraza ya Mungu mahali ambapo watumishi wake husimama ili kupokea neno lake. Mahali ambapo Isaya alisimama, Yeremia alisimama, Yesu Kristo alisimama, mitume walisimama n.k.
Katika baraza ya Bwana, neno la Mungu linaanza na maisha ya huyu nabii ili atakapotoka kwenda kuhubiri akahubiri ushuhuda wake yeye mwenyewe alioushuhudia katika baraza la Mungu. Neno aliloliona Isaya, si neno la kusimuliwa ili na yeye akasimulie. Vivyo hivyo na manabii wote wa Mungu.
Na kwa sababu hiyo hawapewi neno kuzidi uaminifu wao, na uwezo wao ili wasije wakawatwisha wengine mzigo wasioweza kujitwisha wao wenyewe. Nao hutofautiana mmoja kwa mwingine kulingana na nguvu zao katika kuketi katika baraza la Bwana. Maana baraza la Mungu ni kama kuketi motoni, nalo neno lile nabii hulipata kwa njia ya moto kama ilivyoandikwa;
49 Kwa sababu kila mtu atatiwa chumvi kwa moto.
Marko 9
Neno lao ni nyundo juu ya waovu, halitafti mambo ya ulimwengu huu bali haki, wema na hukumu.
BARAZA LA MWANADAMU.
Manabii wa uongo wanalo baraza lao, wakiisha kuitwa na Mungu, huitii sauti lakini hawaketi katika baraza lake. Badala yake huenda kwa wanadamu wakawafundishe walichopaswa kukisikia kwa Mungu. Kama Hawa alivyotoka na kumsikiliza Nyoka kisha akarudi na injili batili.
Ndipo utaona nabii wa uongo ajavyo kuhubiri, akisema Bwana anasema wakati Bwana hakusema nae, bali aliyesema na kumwagiza ni nyoka au mwalimu wake wa theolojia. Ile theolojia ndio Mungu wao na ndiye aliyewaagiza, si Mungu.
2 Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri, uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la Bwana;
3 Bwana MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala hawakuona neno lo lote!
Ezekieli 13:2-3
Kwa kuwa hawakusimama katika baraza ya Mungu, huenda katika baraza yao na kutwaa maneno pasipo yule Roho wa Mungu. Ndipo huyafasiri kwa jinsi ya roho zao na elimu zao za utafiti. Ndipo kwa sababu ya maneno yao ya kujipendekeza hupendwa na watu waipendao njia pana. Na kwa sababu hiyo huzijinajisi madhabahu za Mungu kwa uongo.
Na kunena upumbavu mbele za Mungu wa kila namna wakiisha kuwashinda watu wa Mungu. Agano jipya linawaita watu hawa WANIKOLAI, maana yake ni manabii wa uongo wanaoteka madhabahu za Mungu na wao kusimama badala ya watumishi wa Mungu katika madhabahu zile zile.
Nao wakiisha kuziteka, wamtafutao Mungu kwa kicho itawapasa kutii sheria yao na mafundisho yao ya theolojia ili wasimame kufundisha na kupata chakula maana wao hula kwa fungu la makuhani. Na hapo wanakuwa tayari wanamilikiwa na wadhalimu.
16 Zaidi ya hayo, nikaona tena chini ya jua ya kwamba, Mahali pa hukumu upo uovu, Na mahali pa haki upo udhalimu.
Mhubiri 3
Kama zilivyo serikali duniani, ambazo licha ya kwanba ni ovu lakini ndio zinatawala juu watu wa Mungu na kuwaamulia wanayopasa kufanya, ndivyo manabii hawa walioteka madhabahu za Mungu kuwa zao (walimu, wachungaji, maaskofu, mapdre, mapapa n.k) wanavyoamuru kila ajaye kutoka kwa Mungu awe chini yao.
Mfumo wao wa kiutawala waliouanzisha wameusajili kuwa ndio mfumo wa Mungu serikalini, na ajabu nabii wa Mungu anenaye kinyume na mafundisho yao, kinyume na mfumo wao, humshitaki kwa waovu wenzao yaani serikali ili kwa vyombo vya dola wadhibiti, ili asiuze wala kununua isipokuwa ametii mfumo na kuwa chini yao na kudanganya kama wadanganyavyo.
Ndivyo waliwakataa manabii wa Mungu katika kila kizazi na kuwaua kwa kuwanena kuwa wanapotosha watu wakifundisha mafundisho kinyume na mungu wao yaani theolojia zao ambazo ndio mungu wao. Na hii ndio sababu kwa nini walimuua Yesu Kristo waiyemsubiri kwa kama malaki asemavyo katika malaki 3. Alitoka kwa Mungu na si kwa wanadamu, alikuwa na kweli kutoka kwa Mungu na kazi ilikuwa kuondoa uongo yaani mafundisho yao ya theolojia. Ndipo wakamuua ili miungu yao iishi.
Neno la Mungu linapokuja hawaoni aibu kuwa walisema uongo bali hushupaza shingo zao kwa sababu waliwaaminisha kila mtu kuwa wao ndio wametumwa na Mungu na kwamba walichokinena kwao ndio roho wa Mungu.
Lakini Mungu atatuma wajumbe wakali kuliko wao, na upanga wake ulao utakuwa katika ndimi zao ili kuhumu, na kuua kwa neno kama walivyoua kwa neno kama maandiko yaseamvyo;
11 Mtu mwovu hataki neno ila kuasi tu; Kwa hiyo mjumbe mkali atatumwa kwake.
Mithali 17
Bwana Mungu atamtuma nabii mkali kwao kwa sababu hawana haya usoni wanapojulishwa dhambi yao. Ataufanya uso wa manabii wake kuwa mgumu zaidi kuliko nyuso zao, ijapokuwa ni wanadamu mpaka siku za unabii wao zitakapotimia. Ezekiel aliona ajabu baada ya kufunuliwa haya akawaogopa watu wale katika kizazi chake, lakini Bwana akasema;
8 Tazama, nimeufanya uso wako kuwa mgumu juu ya nyuso zao, na kipaji cha uso chako kuwa kigumu juu ya vipaji vya nyuso vyao.
Ezekieli 3
Manabii wa hawa pamoja na jamii waliowadanganya kwa siri, na kuwaiba kwa siri kutoka kwa Mungu wao hufanya vita na Mungu, kwa kumuua kila aliyetumwa na Mungu kwa kutumia aidha mfumo wao au mapanga na mikuki na kila silaha iliyomikononi mwao ikiwa nabii yule atauvuka mfumo na kuhatarisha utukufu wao.
ISIKILIZENI SAUTI YA BWANA, maana hakuna neno kwenu isipokuwa lililochovywa katika maji ya uchungu. Kwamba mtanyenyekea na kutubu au kwamba mtashupaza shingo zenu mpate kuharibiwa kwa huo uchungu wa maji. Hasira ya Bwana ni juu yenu, mkitaka amani na Bwana rudisheni watu wake mliowateka kwa uongo.
Zirudisheni madhabahu zake na kuondoa unajisi yaani mafundisho yenu juu ya madhabahu zake, vitoeni vyombo vyake vya madhabahu katika nyumba zenu. Acheni kudanganya kwa kutumia jina lake na kuwapora masikini unga wao kwa jina lake.
Naam, Rudini! Mtasema uongo daima? Mtu aendaye kwa miguu pasipo viatu katika nchi huchoshwa na maumivu ya miiba na mbigili, akarudi kuchukua viatu ajistiri, lakini ninyi hamkuchoka kwa maumivu aliyowapa Bwana Mungu, tangu alipoanza kuwajiria.
Ni furaha gani aipatayo mtu kwa kunywa maji machungu, asijinyenyekeshe kwa Bwana wake ili apate kibali? Lakini kwa nini kizazi hiki kimekuwa na shingo ngumu kuliko ya Kaini?
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
Ufunuo wa Yohana 3:20
Mawasiliano;
+255 755 251 999